UKIONA WANASHANGILIA ANGUKO LAKO, UJUE KUNA SHIDA



 KUNA watu wapo mitaani wanashangilia kitendo cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan, kumsimamisha kazi aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya ili kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili.

Tuhuma zinazomkabili hazijawekwa wazi. Chereko za wanaoshangilia jambo hilo unaziona wazi kule mitandaoni, kuanzia Twitter, Instagram, Facebook, Jamii Forum na hata kwenye makundi mbalimbali ya WhatssAp.

Kwa nini wanashangilia? Wanashangilia kwa sababu aliwaalika wafanye hivyo siku ya anguko lake. Yes, aliwatengeneza watu na akawaweka tayari kushangilia siku kama ya jana ilivyotokea. Lakini siyo wanaoshangilia tu, aliwatengeneza hata wale walioguswa na kujisikia vibaya baada ya uamuzi huo kuchukuliwa.

Sabaya alipewa nafasi ya ukuu wa dola wa wilaya. Ni cheo kikubwa kinachomfanya kuwa ndiye muamuzi wa mwisho katika mambo yote yanayohusu wilaya yake. Ndiyo maana, kuthibitisha ukubwa wa nafasi yake, yeye ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wilayani mwake, wakimaanisha awe mtu wa mwisho kuamua linapokuja suala la usalama.

Matumizi ya nafasi yake hiyo, ndiyo yanayowafanya watu leo washangilie, bila kujali kuwa hajafutwa kazi, isipokuwa amewekwa tu pembeni kwa muda ili tuhuma zake zichunguzwe, zikithibitika ndipo maamuzi zaidi yachukuliwe, lakini akionekana hana hatia, anarejea katika nafasi yake.


President Samia suspends Hai DC Ole Sabaya - The Citizen





Maana halisi ya wale wanaoshangilia ni kuwa mambo aliyokuwa anayafanya, hayakuwapendeza. Ni yapi hayo? Ni ngumu kujua kwa sababu ukiwa katika nafasi ya kuwa muamuzi, siyo kila utakachoamua kitawapendeza watu wote, wapo watakaoumizwa na wale watakaonufaika.

Kimaadili, kiongozi anatakiwa achukiwe na wanaopenda kupindisha mambo, kwa manufaa yao. Hawa wanaweza kuwa wabadhilifu, wezi, wanaotumia vibaya ofisi za umma na watu wa aina hiyo, ambao kimsingi, huwa ni wachache katika taasisi.

Inapotokea watu wengi wakachukizwa na matendo yako ukiwa ofisini, maana nyepesi ni kuwa wewe kiongozi ndiye unayefanya mambo yasiyokubalika.

Sabaya ni mmoja kati ya vijana walioaminiwa na kupendwa na hayati Rais wa Awamu ya Tano, John Pombe Magufuli. Pengine kwa maagizo au kwa kujikomba, alitekeleza majukumu yake kwa namna isiyopendeza, akihubiri ubaguzi kwa itikadi za kisiasa. Wapinzani badala ya kuonekana kama wakosoaji wenye nia nje na nchi yao, wakageuzwa adui.

Lakini siyo tu aliwabagua wapinzani, pia alizidisha mikogo na jeuri za mamlaka, akiwajibu aliowaongoza kwa namna alivyotaka. Hata kwenye majukwaa ya kawaida, alipenda uongozi wa kuamrisha badala ya ule wa kushirikisha.

Sabaya aliuchukulia uteuzi wake wa kuwa Mkuu wa Wilaya kama kukabidhiwa rungu. Lugha nzuri zaidi hapa ni kusema cheo kilimfanya akengeuke. Na hapa, vijana kadhaa waliwaangusha wenzao mitaani, wakionekana kuwa malimbukeni wa uongozi, kwani badala ya wao kuongoza kisasa na kuwaonyesha wazee kuwa WANAWEZA, wenyewe ndiyo wakaja kuwa kikwazo na hatari kwa dunia ya utandawazi.

Hapa hakuwa Sabaya peke yake. Paul Makonda, Ally Hapi, Mrisho Gambo, Richard Kasesera na Albert Chalamila nao wanaingia katika kundi hili. Waliwaangusha sana vijana kwa kushindwa kukidhi matakwa ya zama zao.

Tulizoea kuwaona wazee ndiyo wakiishi na dhana ya kuamini katika vyeo vyao vya umma, lakini hawa wakaleta ujana kuwa kero kwa wenzao. Fikiria mkuu wa mkoa, tena kijana, anaenda kwenye kituo cha redio akiwa na askari wenye silaha, kisa jambo lake, NASISITIZA, jambo lake halikwenda alivyotaka.

Ni heri kituo hicho kingekuwa kimekwamisha maendeleo ya mkoa wake, ingawa nayo pia haikumstaili kukifuata na silaha. Angalia ulimbukeni wa vyeo, akakataa hata kuomba radhi kwa kosa hilo la dhahiri la kimaadili!

Hata hivyo, kulikuwa na vijana kadhaa pia walifanya vizuri katika zama hizohizo za Magufuli na wamebakia kuwa mifano hadi sasa. John Mtaka, Jokate Mwegelo na Godwin Gondwe wanawakilisha.

Hawa hawakuwahi kuripotiwa kuwa na uongozi wa kuwazidi kichwani ingawa kwenye maeneo yao ya utawala kulikuwepo wapinzani na watu wasiokubaliana nao.

Hakuna kijana mwenye akili timamu, awe ndani ya CCM au Upinzani, kama hana maslahi binafsi ya moja kwa moja, anayependa kumuona Makonda akirejea kwenye uongozi ndani ya nchi hii. Mrisho Gambo hali kadhalika.

Na huku nje, watu wanasubiri anguko la hawa wengine waliobaki huko, ambao wanaamini wao wamekuwa viongozi kwa sababu wameumbwa tofauti na wenzao, wakisahau kwamba nafasi hizo za kisiasa hazina mwenyewe.

 

No comments