AHUKUMIWA JELA KWA KUMUUA MKE WA PILI, ALIWAHI KUMUUA MKEWE WA KWANZA PIA

Mahakama Kuu Kanda ya Tabora jana
ilimuhukumu kutumikia kifungo cha kwenda jela miaka minne Lameck Essau Meza,
mkazi wa Sikonge mwenye umri wa miaka 38 baada ya kumtia hatiani kwa kosa la
kumuua bila kukusudia mkewe, Dafroza Paul.
Akisoma hukumu hiyo Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya
Tabora, Amour Khamis amesema baada ya kupitia ushahidi wa pande zote mbili
katika shauri hilo la mauaji namba 19 la mwaka 2017, mahakama imejiridhisha
pasi na shaka yoyote kwamba mshtakiwa Lameck alifanya tukio hilo la kumpiga
mkewe na kusababisha kifo chake kinyume na kifungu cha 196 Disemba 24 mwaka
2012 huko Kijiji cha Mwenge wilayani Sikonge.
Hata hivyo kabla ya kutolewa hukumu Upande wa Jamhuri ulidai
kuwa mshtakiwa hii ni mara yake ya pili kufanya mauaji ya aina hiyo ambapo
awali alimuua mke wake wa kwanza na kufikishwa mahakamani akahukumiwa kwenda
jela miaka minne baada ya kupatikana na hatia ya kuua bila kukusudia na hii
ilikuwa ni mara yake ya pili kurejea kosa la aina hiyo baada ya kumuua mkewe
huyu mwingine.
“Hii ni mara ya pili, alishawahi kumuua bila kukusudia Mkewe
wa kwanza (kwa kumpiga) na alihukumiwa kifungo cha miaka minne pia,” ilielezwa
mahakama hiyo.
Jaji mfawidhi wa mahakama hiyo kuu kanda ya Tabora alidai
kuwa mauaji hayo ameyafanya tena bila kukusudia kutokana na hasira za ghafla za
mshtakiwa zilizotokana na mwanamke huyo kuchelewa kurudi nyumbani na ndipo
akawa anamuonya kwa kumpiga mateke, ngumi na vipande vya tofali.
Lameck Meza amehukumiwa kutumikia kifungo cha miaka minne
Jela huku mahakama ikiacha milango wazi ya kukata rufaa.

Post a Comment