UFUTA EKARI TANO YA SHAMBA DARASA LASHINDWA KUVUNWA NAMTUMBO


Makutika Da Farm - *KILIMO BORA CHA UFUTA* Hili zao linalolimwa kwa wingi  katika mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma, Pwani, Morogoro, Dodoma, Tanga na  ukanda wa chini katika mikoa ya Rukwa na

 NA STEPHANO MANGO, NAMTUMBO

BAADA ya kutumika kwa shilingi milioni mbili kwa ajili ya kulima shamba darasa la kuwashawishi wakulima kujiingiza kwenye kilimo cha ufuta, Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma imeshindwa kuvuna kutokana na ukosefu wa fedha.

Ofisa Kilimo wa halmashauri hiyo Laurance Ndaka pamoja na mkuu wa idara ya kilimo ushirika na umwagiliaji, Joseph Mbilinyi waliiambia ojuku1 blog kuwa idara iliomba fedha kwa Mkurugenzi kiasi cha shilingi milioni moja ili kukamilisha zoezi la kuvuna na kujenga sehemu ya kuweka ufuta huo pamoja na kazi ya kuupiga lakini tangu April mwaka huu imekuwa kimya.

Walisema Idara ya kilimo wilaya ya Namtumbo iliomba fedha hizo kupitia vikao halali vya kisheria vya Halmashauri kulima shamba la maonyesho kwa wakulima wa zao la ufuta ili wananchi waweze kujifunza kupitia shamba hilo la ekari tano.

Na kwamba wazo  hilo liliungwa mkono na vikao halali vya kisheria ambapo  awali Halmashauri ilitoa shilingi milioni 2 kwa ajili ya kusafisha shamba, kulima pamoja na palizi hali iliyowafanya baadhi ya wakulima kuvutiwa kutembelea shamba hilo kujifunza.

Wakizungumza na blog hii, wakulima waliolima shamba hilo Saidi Kiokola na Sijawa Omari wameshangazwa na hali ya shamba hilo kutovunwa na kuuacha ufuta ukikaukia shambani na kuikosesha Halmashauri fedha nyingi ambazo zingepatikana kutokana na kuuza kwa ufuta huo kwa mfumo wa stakabadhi ghalani.

Kiokola alidai gharama iliyotumika kwa Halmashauri ya milioni 2 na ile ya kuvunia shamba hilo ingerudi na kupata faida kubwa licha ya yeye kutokuwa mtaalamu ila kutokana na kuona hali ya uzalishaji ulivyo na kiasi cha pesa ambacho kingeweza kupatikana kwa makadirio.

Akizungumza kwa njia ya simu, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo Evance Nachimbiya alikiri kuwepo kwa shamba darasa la ufuta lenye ukubwa wa heka 5 ambalo lilianzwa kulimwa mwezi disemba mwaka jana katika eneo la Nafco wilayani humo.

Nachimbiya alisema kuwa awali idara ya kilimo walileta dokezo la kuomba fedha shilingi milioni 3 kwa ajiri ya kulima na kuvuna ufuta katika  shamba hilo, ambapo kwa awamu ya kwanza walipewa shilingi milioni moja kwa ajiri ya maandalizi na kulima shamba hilo na baadae tena walipewa milioni moja kwa ajiri palizi na mbolea na kufanya jumla kuwa na milioni mbili.

"Nashangaa kukusikia kuwa ufuta huo umekauka na haiwezekani kuvunwa kwa sababu mie sikuwepo kwa zaidi ya wiki mbili, nilikuwa safarini kikazi mjini Dodoma, labda mpaka niwasiliane na Ofisa kilimo kwa ajiri ya maelezo zaidi," alieleza Nachimbiya.

 

 

No comments