MBUNGE MSTAAFU AKUJUZA KILIMO CHA NGORO MBINGA

NA STEPHANO MANGO, MBINGA
Ngoro ni aina ya kilimo
kinachohifadhi mazingira kwa njia ya asili ambacho kinaaminika kilianza
kutumika na wakulima wa kabila la wamatengo Wilaya ya Mbinga Mkoa wa Ruvuma
zaidi ya miaka 300 iliyopita.
Kilimo cha ngoro
kilianzishwa na wazee maarufu wa kabila la wamatengo waliotokea nchini Malawi
katika karne ya 17 ambapo tayari vizazi zaidi ya 10 vimepita hivi sasa tangu
kilimo cha ngoro kilipoanzishwa katika wilaya ya Mbinga.
Elineus Ngwatura Ndunguru
Mbunge Mstaafu wa Mbinga anataja moja ya madhumuni ya kuanzisha kilimo hiki ni
kuudhibiti udongo wa juu wa ardhi ambao kwa kawaida huondolewa na maji au
upepo kutokana na mmomonyoko wa ardhi ya juu ambayo ina rutuba
nyingi ya kuifanya mimea iweze kustawi vizuri na hatimaye kutoa mavuno mengi na
bora.
‘‘Tunajua kuwa udongo
ulio chini ya tabaka la juu hauna rutuba ya kutosha ya kuwezesha mazao kustawi
vizuri, Kutoweka kwa udongo wa juu toka shambani au bustani kwa njia ya
mmomonyoko ni hasara kubwa kwa vile kunasababisha upungufu wa
mavuno’’,anasisitiza Ndunguru ambaye ni Mkurugenzi Mstaafu wa idara
ya wanyama pori iliyo chini ya wizara ya Maliasili na Utalii.
Anazitaja njia za
kuhifadhi ardhi zinaweza kutumiwa kwa kutegemea hali ya hewa, mazingira ya eneo
kama ni maeneo ya mwinuko au tambarare.
Hata hivyo, zinaweza
kutumika njia mbili au tatu katika shamba moja. Ziko njia kuu mbili za
kuhifadhi ardhi ambazo ni njia za asili au za kienyeji na njia ya kisasa ambazo
zimefanyiwa utafiti wa kina na wataalam.
Wataalam wakongwe kama
akina Bike mwaka 1938, Stenhouse mwaka 1994, Temu na
Bisanda mwaka 1966 wanaeleza kuwa Wamatengo walilazimika kutumia
kilimo cha ngoro ili kuhifadhi udongo mzuri uliopo katika miteremko
hiyo.
Katika mashimo ya ngoro
hupandwa mazao kama maharage, mahindi na ngano kwenye kingo za mashimo hayo.
Mkulima hufyeka shamba lake na kuzipanga nyasi
zilizokatwa kwenye mashimo ya ngoro.
Mkulima akipindua udongo
wa chini kuwa juu hukata nyasi na kwamba udongo wenye rutuba hugeuka kuwa mboji
na rutuba huongezeka. Maji ya mvua yakisimama katika mashimo ya
ngoro hulinda unyevu wa ardhi na kukinga mmomonyoko wa ardhi.
Inaaminika kuwa kilimo
cha ngoro ambacho tunaweza kukiita draft agriculture kinahusishwa na shughuli
za kuwepo kwa mapango ya kuishi. Historia ya Wilaya ya Mbinga inaonesha kuwa, hapo
zamani wananchi wa Wilaya ya Mbinga walikuwa na tabia ya kufanya kilimo cha
kuhamahama.
Wakulima wakati huo
walilima sehemu moja na wanapogundua sehemu hiyo rutuba imemalizika walikuwa
wanahamia sehemu nyingine yenye rutuba na kuendesha kilimo bila kujali athari
za kimazingira ambazo zilikuwa zinajitokeza kutokana na aina hiyo ya kilimo.
Kutokana na kuwepo kwa
mapango, wazee hao wa kabila la wamatengo waliamua kuanzisha kilimo cha kulima
na kufukia majani ili kupata mbolea ya asili hivyo kuendesha kilimo
walichokiita ngoro katika sehemu moja bila kuhama huku wakirutubisha ardhi na
kuzuia mmomonyoko wa udongo kutokana na ardhi ya Mbinga kuwa na
milima yenye miteremko mikali.
Mbunge mstaafu wa
Mbinga Ngwatura Ndunguru anasisitiza kuwa wamatengo tangu wameanza
kutumia kilimo cha ngoro miaka 300 iliyopita hadi sasa wamekuwa wanazalisha
vyakula kwa wingi na kuhifadhi mazingira kwa njia ya asili kwa kuzuia
mmomonyoko wa udongo kutokea kwenye miteremko ya milima ya umatengo wilayani
humo.
Anabainisha zaidi kuwa
katika kilimo cha ngoro mvua zinaponyesha maji huingia kwenye mmea
na majani yaliyowekwa chini yanaoza ambapo katika msimu mwingine
majani yaliota kwenye shimo yatafyekwa, mazao yaliosalia yanavunwa
na kutandazwa kwenye shimo na kufukuliwa majani ya mwaka jana ambayo tayari
yanakuwa mboji.
John Mbunda (80) mkazi wa
kijiji cha Kilanga Juu wilayani Mbinga anasema wamatengo walianzisha
mfumo maalum wa kilimo cha ngoro uliyowasaidia uliyojulikana kwa
kabila la wamatengo kwa jina la Ingoro.
Anasema mfumo huo
uliwawezesha kuendelea kulima kwenye maporomoko ya milima bila ya kusababisha
mmomonyoko wa udongo au kuathiri vibaya rutuba kwenye mashamba yao.
Alex Ndunguru mkazi wa
Kijiji cha Ilela anasema wenyeji wa Mbinga walilazimika kubuni
kilimo cha ‘ngoro ili kuhifadhi udongo mzuri ulio katika miteremko ya Umatengo
na kwamba ngoro ndiyo mkombozi katika kilimo kwa kuwa kilimo kimekuwa endelevu
badala ya mfumo wa zamani ambao wamatengo walifanya kilimo cha kuhamahama.
Utafiti umeonesha wazi
kwamba teknolojia ya ngoro ni bora zaidi katika kilimo, ambapo
wakulima kutoka maeneo mbalimbali nchini wamekuwa wakifika katika
Wilaya ya Mbinga kujionea wenyewe na kujifunza teknolojia hiyo inayohifadhi
ardhi na kutunza mazingira kwa muda mrefu.
Moja ya faida ya kilimo
cha ngoro ni kwamba hata kama mvua hazitanyesha, bado shamba litaendelea kuwa
na unyevunyevu kutokana na maji yaliyomo ndani ya mashimo hayo.
Kulingana na Mbunge Mstaafu
Ngwatula Ndunguru tayari wameanza kukitangaza kilimo hicho na kukiingiza kuwa
ni miongoni mwa vivutio vya utalii ambavyo vinapatikana katika wilaya ya Mbinga
pekee.
Baadhi ya
wageni ambao wamekuwa wakitembea kwenye magari kupitia barabara ya
Mbinga hadi Mbambabay Wilaya ya Nyasa pamoja na maeneo mengine ya milima ya
umatengo wamekuwa wakisimama mara kwa mara kwenye milima hiyo na kuchukua picha
za kawaida na video.
Ndunguru anasisitiza kuwa
kilimo cha ngoro kimeonekana kuwavutia watu wengi
wa ndani na nje ya nchi hasa mimea inayochomoza na
kuonekana mfano wa mapambo yaliopambwa juu ya milima ya Umatengo.
Wizara ya Kilimo
imeanzisha Mradi wa kufufua Mifumo muhimu ya asili ya kilimo duniani (Global
Importance Agricultural Heritage System- GIAHS) ili kuendeleza Kilimo cha asili
na kumpunguzia mkulima gharama za uzalishaji.
Taarifa kutoka Idara ya
Matumizi Bora ya Ardhi Katika Wizara hiyo inaeleza kuwa mradi huo unatekelezwa
na Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) ambao unalenga kutambua mifumo ya
asili na endelevu ya kilimo na ufugaji ili kumsaidia mkulima.
Kwa mujibu wa taarifa
hiyo katika Afrika Mashariki nchi ya Tanzania na Kenya ilichaguliwa kufufua
mifumo hiyo kwa kuwa na sehemu muhimu za kilimo na kwamba baada ya kuchaguliwa
nchi ya Tanzania ilipendekeza mifumo mitatu ya kilimo asili ukiwemo mfumo wa
Ngoro ambao unatumiwa na kabila la wamatengo.
Mifumo ya asili ya kilimo
ilianza kupendekezwa duniani tangu mwaka 2002. Baadhi ya nchi ambazo zimeanza
kutumia mifumo hii ya asili katika kilimo ni Japan, Uphilipino, China
na Ujerumani.

Post a Comment