TWANGA PEPETA YAJA NA UZINDUZI, TUZO KWA MAGWIJI

MIAKA nane sasa, bendi kongwe ya muziki wa dansi ya African Stars Twanga Pepeta haijatengeneza albamu, lakini mwishoni mwa mwezi huui, jambo hilo linakwenda kutokea pale Break Point, Makumbusho jijini Dar es Salaam.
Mara ya mwisho Twanga Pepeta ilitambulisha albam mpya "Usiyaogope Maisha" mwaka 2016 jijini Mwanza, wakati kwa upande wa Dar es Salaam tukio la aina hiyo lilifanyika 2013 kupitia albam ya "Nyumbani ni Nyumbani".
Katika uzinduzi wa albamu yake ya 14, Twanga itasindikizwa na Msondo Ngoma na Tukuyu Sound;
Albam ina jumla ya nyimbo sita:
"Povu" utunzi wake Haji Ramadhani, "Twanga Mbele"
uliotungwa na Kalala Jr ambaye kwasasa anaitumikia Tukuyu Sound, "Penzi
Sigara Kali" ya Chaz Baba, "Ningekuwa" kutoka kwa chipukizi
Joshua Pianno, "Rekebisha" na "Push to Start" zote za Said
(Diouf) Msafiri.
Boss wa Twanga Pepeta, Asha Baraka "Iron Lady" ameiambia Saluti5 kuwa jina la albam litatajwa ukumbini lakini akaongeza kuwa siku hiyo pia zitatolewa tuzo kwa wanamuziki wagwiji walioacha alama kwenye muziki wa dansi.
Twanga inajivunia muunganiko mzuri wa wapiga vyombo wanaofahamiana kwa muda mrefu na walioshikana ipasavyo wakiwemo Jojoo Jumanne (bass gitaa) Miraji Shakashia (solo na rythim gitaa), God Kanuti (solo na rythim gitaa), Victor Nkambi (Kinanda) na Kirukuu (drums).
Safu yao ya uimbaji inatisha
kama njaa na imesheni mastaa tishio kwenye dansi kama vile Luizer Mbutu, Chaz
Baba, Saleh Kupaza, Khalid Chokoraa, Msafiri Diouf na Haji Ramadhan bila
kusahau vijana wawili wanaochipukia Joshua Piano na Tariq Zuberi ambao hakuna
ubishi kuwa wameongeza ladha mpya kwenye bendi hiyo.
Ally Chocky 'Mzee Mbishi' amethibitisha atakuwepo katika onyesho hilo, uwepo ambao huenda ukajibu maswali mengi juu ya 'ndoa' tarajiwa kati yake na Twanga.
Credit: Salute5

Post a Comment