'STRESS' ZINAKUTOAJE KWENYE RELI?


Stressed Black Man HD Stock Images | Shutterstock

HAPA duniani bwana mambo ni mengi kweli kweli, kiasi kwamba kuna vitu vinaendelea hadi ukiwa peke yako unajiuliza, hivi hili limetokeaje, maana hata huamini.

Sisi waswahili wakati mwingine mtu akiishi miaka 80 na kuendelea huko, inabidi umpongeze sana, maana hapa katikati amepitia misukosuko mingi sana, kuanzia nyumbani, kazini, barabarani, vijiweni na hata katika mitikasi mingine nje ya kazi tunazozifanya.

Unaweza ukawa umetoka zako home fresh kabisa, unaenda zako kazini, uwe kwenye usafiri wako binafsi, upande bajaj, bodaboda au hata daladala. Chukulia umepanda daladala kwa mfano, unasubiri abiria wajae.

Mara mpiga debe anakuja upande uliokaa, halafu analipiga gari kwa nguvu eti anaitia abiria. Kwanza anakushtua, halafu anakupigia kelele, unaweza kupandisha hasira ghafla na kujikuta anaanza kutupiana naye maneno. Ni bora awe mstaarabu akuelewe kwamba kitendo alichofanya siyo cha kiungwana, tatizo linakuja pale anapoamua naye kuja juu halafu anakupa maneno ya kuudhi.

Hapo ikishakuwa hivyo, inakubidi tena ujitafakari na uamue unyamaze tu, maana vinginevyo unaweza kuamua kushuka ukabiliane naye. Sasa hapo kwenye kukabiliana naye ndipo panapotisha, maana hujui nini kitatokea. Unaweza kumpiga ukashinda, lakini umemuumizaje? Anaweza kukupiga ukashindwa, umeumiaje?

Kwa vyovyote, uamuzi wa kukabiliana naye ni hatari zaidi kwako kuliko kwake kwa sababu wewe ndiye utaharibikiwa na mambo yako mengi muhimu kuliko yeye. Kama utakuwa umemuumiza au kinyume chake, suala hilo linaenda polisi na si unajua, wale ndugu zetu hawana jambo dogo maana kwanza wote mnakuwa mmevunja sheria ya kupigana hadharani.

Halafu mmeumizana. Ni lazima fedha itahusika. Asikudanganye mtu, huwezi timiza jambo lako polisi bila hela, labda uwe na mkubwa anakusimamia, vinginevyo hata ukiwa na ndugu yako, atakushawishi 'umtoe' afande maana ndiye kawezesha hilo jambo liishe!

Huo ni mfano mmoja tu kati ya changamoto nyingi tunazokutana nazo barabarani. Wengine wanazinguliwa na bodaboda, wengine bajaj, wengine madereva teksi na wengine madereva wa daladala. Si unakumbukaga kisa cha mkuu mmoja wa mkoa aliyewahi kumpiga risasi na kumuua dereva wa daladala baada ya 'kulipiga pasi' Prado lake?

Hizi changamoto za barabarani ni cha mtoto, kuna watu wana changamoto majumbani mwao, kunawaka moto. Baba na Mama hawapikiki chungu kimoja, familia imesambaratika na umasikini unawanyemelea.

Usimuone mtu anatembea anaongea peke yake barabarani, ukute hapo anamfokea mtu, anamtukana bosi wake kazini au hata anamkaba mtu shingo.

Kuna watu huko makazini kwao wanaandamwa sana na mabosi, ana anapigwa vita sana na wenzake, kiasi kwamba kibarua chake wakati wowote kitaota nyasi. Hana raha. Au wengine ndiyo hivyo, wamepewa barua za kuachishwa kazi.

Yaani hata kosa lako hulijui, unaambiwa kazi basi. Hapo jana tu ndiyo umetoka kusambaza pesa za mkopo uliokopa ili ufanyie mambo yako urejeshe taratibu kwa taasisi hizi za mikopo. Lazima tumbo likuume!

Kwa kifupi, namaanisha zipo changamoto nyingi na za aina tofauti. Usije ukamuona mtu ana jumba kubwa, gari la thamani na watoto wote English Medium Schools ukadhani jamaa yupo comfortable!

Huwezi jua kilicho nyuma yake, wengine wamesuswa na familia zao. Yaani pamoja na pesa zake, lakini hana uhusiano kabisa na wazazi wake, ndugu zake wa kuzaliwa pamoja na hata ukoo. Anaishi kama mnyama ambaye ana mashaka ya kulogwa wakati wowote. Huyo, akiona ndege katua kwenye paa lake, akili yote anaipeleka kwa uchawi, anakimbilia kwa mganga.

Lakini, pamoja na yote, hizi changamoto ambazo tunapenda kuita wakati mwingine msongo wa mawazo au stress, tunazikaribisha sisi wenyewe. Laiti kama ungejua, hicho kitu kiuhalisia hakipo!

Believe me, adui yako namba moja ni wewe mwenyewe. Kwa nini, kwa sababu ni wewe ndiye unayeanza kuutengeneza wasiwasi akilini mwako, ukiamini kuwa jambo lililokukuta ni baya na litakusumbua. Niliwahi kukoma kitabu kimoja na ningekushauri ikikufaa kitafute, kinaitwa How To Start Living Again.

Hiki ni kitabu kinachokurudisha katika maisha baada ya kupatwa na kile kinachokutesa. Listen, hakuna jambo geni hapa duniani ambalo wewe utakuwa mtu wa kwanza kulifanya au kufanyiwa, hakuna. Kama lipo hebu jikumbushe mwenyewe kwamba hili hukupata kulisikia.

Kuna watu wanajiua baada ya kufukuzwa kazi..Came on, wewe vipi? Mbona unafanya ujinga namna hii? Halafu anaacha ujumbe kuwa nimejiua kwa sababu nina madeni na kazi nimefukuzwa, shit!

Kuna watu wanadaiwa billions of money na wamefilisika, lakini bado wanadunda tu. Kama Mungu alikujaalia ukafanikiwa kujenga kibanda, ukachukulia mkopo ukashindwa kulipa afu wanaokudai wakaja kukichukua, usijali. Hiyo ndiyo mipango ya Mungu, ana kusudi lake!

Uliwezaje kupata hela ya kukijenga mara ya kwanza ushindwe mara ya pili? Eti umefumaniwa na mtoto wa ndugu yako ukiwa umelala naye, sasa unaamua kujiua eti unakwepa aibu. Ha ha haaaa, hebu acha kutuchekesha, unaona aibu?

Kama ulikuwa na aibu ungetafakari mapema kabla ya kuamua kumuingia na hivyo ungejiepusha nayo, lakini kwa vile uliamua liwalo na liwe, means ulikuwa umejiandaa kisaikolojia. Komaa, pambana na aibu hiyo mbele yako kwa sababu wewe siyo mtu wa kwanza kufumaniwa ukiwa umelala na mtoto wa ndugu yako.

Kuna watu walifumaniwa na watoto wao wa kuwazaa na bado maisha yanaendelea. Hapa simaanishi kwa mifano hii miwili nakushauri ukopee fedha kibanda chako au umtongoze au kulala na mtoto wa ndugu yako. Nimetoa mifano hii kwa sababu ndiyo inayoeleweka mapema.

Maana yangu ni kuwa ili kukabiliana na matatizo makubwa, unapaswa kujiuliza kama wewe ni wa kwanza kuyapata au kama unadhani utakuwa wa mwisho. Kwa vyovyote jibu litakuwa HAPANA. So, kabiliana nalo kwa namna yoyote.

Kuna mtu yupo sehemu anaweza kukusaidia, hata kama siyo kwa asilimia kubwa. Kitu cha kwanza unachopaswa kufanya ni kumshirikisha mtu unayemuamini katika tatizo lako. Ni mtu gani unayemuamini?

Hii pia inaweza kuwa changamoto, lakini kifupi ni yeyote ambaye unaamini ataguswa na utakachomweleza, siyo lazima awe rafiki yako wa miaka mingi. Mtu mwingine anaweza kuwa ni mkubwa au mdogo kwako na hamjawahi kuwa na ukaribu wa kutisha, lakini anaonekana ni mtu mwenye uelewa, MFUATE.

Huyu kwa vyovyote atakushauri uvute kwanza subira. Na hiki ndicho kitu kikubwa unachokihitaji, SUBIRA. Unakaaje na mawazo ya kukosa ajira hadi unachanganyikiwa wakati kuna kazi kedekede mjini hapa? Mbona kuna watu kama wewe wanabeba mchanga, wanaponda kokoto na wanaishi na familia zao. Mbona kuna wengine ni mama ntilie na wanasomesha watoto wao?

Stress ni ugonjwa wa kujitakia, ukatae...

 

 

No comments