SIKU NILIPOMUULIZA SWALI AMIRI JESHI MKUU!

 

Jakaya Mrisho Kikwete | president of Tanzania | Britannica


Napokea simu, kama saa nane hivi mchana, miaka ile ya katikati ya 2000. Ni mmoja kati ya kaka zangu kwenye tasnia ya habari ninaowaheshimu sana. Ananiambia ameandikisha jina langu Ikulu, ili niende jioni ya siku hiyo, kwenye chakula cha usiku, kilichoandaliwa kwa ajili ya mabinti wa shindano la Miss East Africa, kukutana na Rais Jakaya Kikwete.

Nikafurahi sana. Jioni yake, kama saa 12 hivi nilikuwa langoni pale Magogoni. Nikasalimisha simu na kuruhusiwa kuingia ndani. Ilikuwa mara yangu ya kwanza kuingia Ikulu aisee. Basi bwana, ndani kule nikakutana na waandishi wengine, pamoja na wale mabinti wa lile shindano.

 

Nilimkuta pia bosi wangu wa zamani, role model wangu, Salva Rweyamamu ambaye wakati huo alikuwa ndiye Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu. Nilipokumbatiana naye kwa salamu, nikajihisi furaha sana. Kama saa mbili na ushee hivi, Handsome Boy akajitokeza, shughuli ikaanza rasmi. Hakukuwa na hotuba, mzee wa Msoga akawa mara anachat na mabinti, mara na waandishi. Msosi time, tukajongea mezani, umewahi kula msosi wa Ikulu?

Mara vinywaji vikamwagika, watu wakawa wanajisevia. JK ni mtu wa tabasamu na anawajua waandishi, akaanza kuwatania anaowafahamu, wewe Nkoromo upo? Angela Michael vipi?

Angela Michael alikuwa ni mwandaaji wa shindano la Miss Kigamboni miaka hiyo na JK alikuwa mmoja wa wafadhili wake. Tangu aingie Ikulu nadhani hawakuwahi kuonana, so akatumia nafasi ile kumwambia "Mheshimiwa umenimwaga siku hizi".

JK akamwambia ni kweli, lakini mimi sasa hivi ni kama mfungwa, sina uhuru ule wa zamani, akaulizia anaendeleaje na shindano lake, binti akajibu poa ila linakumiss, watu tukacheka, maisha yakaendelea.

Sasa bwana, tukiwa naye, kila mwandishi na glasi ya kinywaji chake, watu wakawa wanatafuta cha kumuuliza, si unajua tena waandishi waliokuwepo pale ni wa michezo na burudani pekee?

Nikasema hapana, siwezi pata nafasi kama hii, halafu japo JK hanijui kivile, nikaondoka bila hata swali la kizushi. Sekunde chache baadae nikapata cha kumuuliza.

Unamkumbuka Marcio Maximo? Yule kocha wa Taifa Stars miaka hiyo? Yule Mbrazil alikuwa akilipwa mshahara na serikali. Huku mitaani akaonekana kama vile ni untouchable, maana wakati alifanya kazi yake kiweledi, watu wakajua anafanya vile kwa sababu ameajiriwa na JK.

"Mheshimiwa," nikaanza, akanigeukia kusikiliza na watu wote wakabaki kimya. "Kuna hlli suala la Maximo, huku mitaani wanasema wewe unampa jeuri, ndiyo maana anajifanyia tu anavyotaka katika timu yetu ya taifa, je ni kweli?"

Mkuu akaangua kicheko, akasema "Hata mimi nasikia hizo habari. Si kweli, mimi kama serikali, ninamlipa mshahara tu, waajiri wake ni TFF, kama anafanya ndivyo sivyo, waulizeni TFF, si mimi."

Keshokutwa yake, kumbuka ilikuwa usiku, magazeti ya kesho yake tayari yalikuwa kiwandani, magazeti yote yakaongozwa na habari kubwa ya michezo kuhusu hiyo stori.

Kila mtu ana cha kujisifu kuhusu career yake, kwangu mimi hii ni moja ya vitu ninavyovikumbuka sana, maana kumuuliza swali Amiri Jeshi Mkuu, tena ukiwa na glasi ya mvinyo, si jambo dogo.

 

 

No comments