SPIKA NDUGAI, NAPE WAIPAMBANIA KOROSHO BUNGENI

 

KILIMO BORA CHA KOROSHO |


MBUNGE wa Mtama mkoani Lindi (CCM), Nape Nnauye na Spika wa Bunge, Job Ndugai, wamelipambania zao la Korosho, wakiiomba Serikali irudishe Bodi ya Korosho pamoja na fedha za tozo ya mauzo ya nje ya nchi (Export Levy), kwa wakulima wa zao hilo, ili kulinusuru lisife.

Nape alitoa ombi hilo jana tarehe 24 Mei 2021, katika mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka wa fedha wa 2021/2022, bungeni jijini Dodoma
Mwaka 2018, Serikali ya Tanzania ilifanya mabadiliko katika sheria ya taasnia ya korosho, ambayo yalisababisha fedha zote za tozo ya mauzo ya zao hilo nje ya nchi, kupelekwa katika mfuko mkuu wa fedha za Serikali, badala ya mfuko wa kuendeleza korosho.

Kufuatia mabadiliko hayo, Mbunge huyo wa Mtama ameiomba Serikali irudishe utaratibu wa zamani, wa fedha hizo kupewa wakulima kwa ajili ya kugharamia shughuli za uzalishaji wa korosho.
“Kwa mahesabu ya kawaida, 2018 iliingizwa Sh. 37 bilioni wakati mfuko ukifanya kazi ya kugharamia pembejeo, Serikali ilipata mapato Sh. 1 trilioni na zaidi, kwa kuingiza kiasi hicho cha fedha tu. Mwaka huu makisio ya uzalishaji ni tani 280,000 hadi 350,000, tunahitaji Sh. 55 bilioni tu,” alisema Nape
Mwanasiasa huyo alisema “Maombi yangu kwa Serikali na bahati nzuri naibu waziri (Hussein Bashe), wakati ule tuna mgogoro wa tozo ya ushuru wa nje hapa bungeni. Alikuwa mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Bajeti na alituunga mkono,”

“Matumaini yangu kwenda kwake serikalini hakujambadilisha kuliona jambo hili kwa usahihi, tuchukue fedha ya export levy turudishe kugharamia korosho,” alisema Nape.

Baada ya Nape kutoa maombi hayo, Spika wa Bunge, Job Ndugai alimuagiza Waziri wa Kilimo, Prof. Adolph Mkenda, atoe majibu ya kina kuhusu suala hilo, leo tarehe 25 Mei 2021, wakati anahitimisha hoja yake kuhusu bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha ujao.

“Utakapohitimisha hoja yako, mambo haya na kwa msingi yalivyokuwa tungependa kusikia Serikali inasemaje,” alisema Spika Ndugai na kuongeza”

“Na kesho (leo), wakati wa mafungu nitakuwa nimekaa hapa. Wakikubana nitawaacha na nikiri kwamba, bahati mbaya na mimi ni mkulima wa korosho. Kwa hiyo kesho (leo) tunataka majibu, ili twende mbele kwenye zao la korosho.”"

No comments