SHIRIKA LA MASOKO KARIAKOO LAKALIA KUTI KAVU

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Ummy Mwalimu ameunda tume huru ya kuchunguza kero na malalamiko ya wafanyabiashara wa Soko la Kariakoo na kutoa siku 14 kukamilika kwa uchunguzi huo, huku pia akitaka watu hao kuishauri serikali kama bado ipo haja ya kuendelea kuwa na shirika hilo la masoko.
Ameunda tume hiyo leo mara baada ya kuongea na wafanyabishara
wa soko hilo katika ziara yake ya kukagua utendaji kazi na kusikiliza changamoto
za wafanyabishara wa soko hilo, Jijini Dar-es-salaam.
Waziri Ummy amesema kuwa baada ya kuwasikiliza
wafanyabiashara hao amegundua kuwa lipo tatizo katika soko hilo ambapo amesema
tatizo kubwa ni ukosefu wa mahusiano mazuri kati ya wafanyabishara na
menejimenti ya Shirika la Masoko la Kariakoo, uwepo wa tuhuma za rushwa kwa
baadhi ya viongozi, tozo kubwa la kodi na uwepo wa madalali wa vigoli pamoja na
uwepo wa ubadhilifu wa fedha za mali za Shirika la Masoko ya Kariakoo.
Ameiagiza Tume hiyo kuhakikisha inapitia kwa kina malalamiko
yaliyowasilishwa na wafanyabiashara hao ili yaeze kupatiwa ufumbuzi na Serikali
kwa wakati na kufanyiwa uamuzi utakaosaidia kulipeleka taifa mbele katika
kuhakikisha wafanyabishara wanafanya biashara zao katika mazingira mazuri kwa
gharama zinazokubalika na Serikali.
Akizungumzia uwepo wa madalali, Waziri Ummy amesema kuwa wapo
madalali waliojimilikisha vizimba na vigoli katika soko hilo ambapo
wanawapingisha wafanyabiashara wadogo kwa gharama kubwa hali hii inarudisha
nyuma juhudi za Serikali za kuhakikisha watu wake wanapata maeneo ya kufanyia
biashara ili kujikwamua kimaisha na kujiongezea kipato.
Aidha, ameiagiza Timu huru ya uchunguzi kuishauri Serikali
kama upo umuhimu wa kuendelea kuwepo kwa Shirika la Masoko ya Kariakoo kwa
kipindi cha wakati wa sasa kulingana na mabadiliko ya kisanyansi na Teknolojia.

Post a Comment