SERIKALI KUKAGUA MADUKA YA DAWA YANAYOUZA VIDONGE KUZUIA MIMBA
SERIKALI imesema itaanza kufanya ukaguzi katika maduka ya dawa muhimu na yatakayobainika kuuza vidonge vya dharura vya kuzuia ujauzito (P2) na vya kutoa mimba (misoprostol) bila cheti cha daktari yatachukuliwa hatua
Pia, wananchi wametakiwa kutoa ushirikiano ili kuyabaini
maduka hayo na kupunguza madhara yanayoweza kutokea.
Msajili wa Baraza la Famasia nchini, Elizabeth Shekalaghe
alisema hayo katika mkutano mkuu wa chama cha wafamasia (PST) wenye kauli mbiu
“Wataalamu wa famasia ni muhimu kuboresha upatikanaji wa dawa bora Tanzania.”
Shekalaghe alisema P2 na misoprostol ni dawa za cheti
zinazoruhusiwa kuuzwa katika famasi lakini kwa cheti cha daktari.
“Pamoja na changamoto tunazokabiliana nazo katika udhibiti wa
uuzwaji holela wa dawa, imebainika dawa hatarishi nikimaanisha misoprostol na
P2 zimekuwa zikitumika kinyume na makusudio ya Serikali, tunatarajia lazima
zitolewe na cheti cha daktari,” alisema Shekalaghe.
Alitoa wito kwa wananchi kutoa taarifa pale watakapokuta dawa
zinazotolewa au kuuzwa kinyume bila cheti sababu ni kinyume cha sheria na
kanuni zinazosimamia utoaji wa dawa za cheti.
“Nawakumbusha wataalamu wote hata katika yale maduka
yanayoruhusiwa kuuza hizi dawa, ni vizuri kuweka kumbukumbu sahihi ili mamlaka
zinapopita zifahamu hizi dawa zilitolewa kwa misingi ipi,” alisema Shekalaghe.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Dorothy Gwajima aliagiza hatua zichukuliwe
kwa wafamasia na wauzaji wa maduka ya dawa wanaokiuka taratibu na kanuni hivyo
kuweka maisha ya Watanzania kwenye hatari.
“Iweje dawa zinazohitaji cheti cha daktari zitolewe kinyume
na kanuni, chukueni hatua kali kwa wote wanaokiuka, pia rekebisheni sheria na
kanuni zinazodhibiti suala la uandikaji na utoaji wa vyeti vya dawa,” alisema
Dk Gwajima.
Mfamasia Mkuu wa Serikali, Daudi Msasi alisema maduka ya dawa
muhimu ndiyo yanayouza dawa ambazo hazikubaliki na yanaongoza katika kuuza P2.
“Wananchi wanalalamika wafamasia tumeshindwa kuwalinda dhidi
ya dawa hizo, matokeo yake watoto wanazitumia ndivyo sivyo, kumbukeni maduka
haya vyeti vyenu vya taaluma vimetumika kuyafungua, lakini ndiyo yanayoongoza
kuuza dawa kinyume na sheria,” alisema Msasi.
Daktari bingwa wa magonjwa ya kinamama na uzazi kutoka
Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Living Colman alisema vidonge vya P2
hutumiwa na mtu ambaye amekutana na mwenzake bila kujua yupo katika kipindi cha
hatari cha kupata ujauzito.
“Au itokee kama amebakwa lakini kwa vyovyote na si yawe
matumizi ya mara kwa mara,” alieleza Dk Colman.
Alisema matumizi ya mara kwa mara ni kufanya mrundikano wa
uzazi wa mpango katika mfumo wa kizazi ambao husababisha madhara baadaye.
“Anayekusudia kutumia mara kwa mara ina maana anajiwekea
homoni nyingi mwilini ambazo zinaweza kuvuruga mfumo wa uzazi na pengine
akashindwa kupata mtoto,” alitahadharisha Dk Colman.

Post a Comment