CHUO KIPYA CHA UFUNDI KUANZA KUJENGWA DODOMA

Na Mwandishi Wetu, Dodoma
SERIKALI kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
inajenga Chuo cha Ufundi katika Mkoa wa Dodoma chenye uwezo wa kuchukua
wanafunzi 5000 ili kuongeza wigo na fursa za upatikanaji wa ujuzi na maarifa.
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini Mkataba wa ujenzi wa
chuo hicho uliofanyika Jijini Dodoma, Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na
Teknolojia, Dkt. Leonard Akwilapo amesema ujenzi wa chuo hicho utagharimu zaidi
ya Shilingi bilioni 17 kupitia mradi wa Kukuza Ujuzi na Stadi za Kazi (ESPJ)
unaosimamiwa na Wizara.
Katibu Mkuu huyo ameitaka kampuni iliyoshinda zabuni ya
ujenzi wa chuo hicho, CRJE East Africa Ltd. kuhakikisha inakamilisha ujenzi huo
ndani ya miezi 18 kama Mkataba unavyoonyesha.
“Leo tumesaini mkataba wa ujenzi wa Chuo cha Ufundi Dodoma,
ni matarajio yangu kitakamilika kwa wakati naubora unaotakiwa ili malengo ya
kuanzishwa kwa chuo hiki yaweze kutimia,” amesema Dkt. Akwilapo.
Naye Meneja wa kampuni ya CRJE East Africa Ltd. tawi la
Tanzania, Xu Cheng ameahidi kutekeleza mradi huo kwa ubora unaokubalika na
kuhakikisha unakamilika kwa wakati uliopangwa.
Mradi huo utahusisha ujenzi wa miundombinu ya Jengo la
Utawala, Ofisi za Idara, nyumba za watumishi, mabweni, Zahanati, Vyoo vya
wanafunzi na watumishi, karakana tatu na kituo cha kupoza umeme.

Post a Comment