RUBANI ALIYETOROSHA NDEGE YA TANZANIA AFARIKI

RUBANI Mstaafu wa Tanzania, kampteni Narzis Mapunda amefariki dunia jana jijini Dar es Salaam.
Mwaka 2019 Kapteni Mapunda ambae ni rubani mstaafu
alitunukiwa tuzo na Rais John Magufuli kwa uzalendo wa kutorosha ndege ya
Tanzania baada ya kuvunjika iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka
1977.
Kwa mujibu wa maelezo ya Mapunda, siku ilipotangazwa kuwa Jumuiya
ya Afrika Mashariki imevunjika, alikuwa zamu na rating yake ya kazi siku hiyo
ilikuwa kurusha ndege kutoka Nairobi kwenda Mombasa, halafu Tanga na mwisho Dar
es salaam. Alipofika Mombasa, taarifa zilimfikia kwamba jumuiya imevunjika
hivyo ameagizwa awashushe abiria wote Mombasa, kisha airudishe ndege hiyo
Nairobi.
Ndege hiyo ilikuwa aina ya Fokker Friendship F27 anaeleza
alikataa kushusha abiria kwa sababu abiria wengi kwenye ndege hiyo walikuwa
wanakwenda Dar es salaam, akawaomba wamuongezee mafuta ya kumfikisha Dar na
kuahidi kwamba akishawafikisha atairejesha ndege Nairobi hata hivyo wahusika
walikataa kumpa mafuta kwa kigezo kuwa mafuta ya ndege yameisha.
Ndipo alipopiga hesabu yake na kuona kwamba mafuta
aliyokuwa nayo yalimtosha kufika Tanga. Akaendelea na safari yake hadi Tanga na
alipofika Tanga aliongeza mafuta na kwenda Dar na mara baada ya kufika
alishusha abiria wote aliyokuwa nao na kuikabidhi ndege kwa wahusika pale
uwanja wa ndege wa Dar es salaam - terminal 1.

Post a Comment