DOLA FEKI ZATUMIKA MIAKA 20 BILA KUJULIKANA

  

Hata zilishindwa kubaini noti hizo bandia

WAKATI Marekani ikijinasibu kama Taifa lenye intelijensia kali na bora kuliko wote duniani, habari mbaya kwao ni kwamba zimegundulika fedha bandia, dola za nchi hiyo, ambazo zimeingizwa katika mzunguko na kufanya kazi kwa zaidi ya miaka 20 bila kugundulika.

Noti hiyo ya dola bandia haikuwa na makosa yoyote na hata maafisa wa kitengo cha ujasusi hawakuweza kubaini iwapo ilikuwa dola bandia ama nakala halisi mbele yao.

Ni baada ya kipindi kirefu cha uchunguzi ndipo waliweza kuthibitisha kwamba zilikuwa hela bandia.

Lakini noti hizo za dola mia moja zilikuwa hazina dosari yoyote hadi zikapewa jina ''The Super fake Dollars''.

Zilikuwa na rangi kama ile ya noti halisi za dola za Marekani.

Pia zilichapishwa katika karatasi iliyokuwa sawa na ile ya pesa halisi ikiwa na robo tatu ya pamba na robo ya kitani (linen).

Picha ya noti hizo ilikuwa bora zaidi ya zile zilizochapishwa na shirika la kuchapisha fedha Marekani.

Mashine ya kuhesabu noti katika benki pia zilishindwa kubaini uhalisia wake. Zilikuwa na tofauti kidogo sana, wakati Gazeti la The New York Times liliporipoti kwamba fedha hizo hazikuwa halisi, Marekani lishangazwa kwamba fedha bandia ziliweza kupita benki zake bila kujulikana , kwa sababu hakuna aliyeweza kubaini tofauti.

Fedha hizo za Super Dollars zilisambaa kote duniani kati ya miaka 1990 na 2000.

Wakati wa miaka hii, Marekani iliamua kubadilisha noti ya dola 100 mara mbili lakini watengenezaji wa fedha hizo bandia walifanikiwa kubadilisha fedha hizo na kufanana kama zile zinazochapishwa na serikali.

Zilipatikana nchini Denmark, Ufaransa, Austria, Ujerumani, Latvia, Urusi, Czech Republic na Ireland.

Wahalifu nchini Urusi walizitumia bila aibu.

 

Kwa miaka kadhaa zilikuwa mwiba kwa shirika la ujasusi la Marekani FBI.

Hawakujua ni nani aliyekuwa akizichapisha, Ilichukua operesheni kali ya miaka minane ili kuanza kuwakamata wahusika.

Walifanikiwa kuwakamata washukiwa wa kwanza mjini California na New Jersey, baada ya wachunguzi kupata makasha ya fedha hizo kutoka katika meli kutoka kusini mashariki mwa bara Asia.

Wale waliokamatwa walikuwa na uhusiano na wahalifu wa kimataifa, lakini maafisa wa shirika la FBI walikuwa wakishuku kwamba mtandao huo ulikuwa mkubwa zaidi.

Fedha hizo hazikutengenezwa na wahalifu wa kawaida ama mtandao wa wahalifu, lakini zilitengenezwa na serikali ya Korea Kaskazini... Serikali ya Marekani ilisema.

Mara kwa mara fedha hizo zilipatikana katika mikono ya wanadiplomasia wa Korea Kaskazini, pengine kuongeza mapato ya taifa hilo ambalo lilikuwa likikumbwa na matatizo ya njaa na kuanguka kwa mshirika wake mkuu Muungano wa Usovieti.

 

Hata hivyo Korea Kaskazini inakana kuhusika katika kuchapisha fedha hizo.

''Korea Kaskazini imekana kuhusika katika usambazaji na uchapishaji wa sarafu bandia , lakini ushahidi unaonesha wazi kwamba ni wao'', alisema Daniel Glazer, Naibu Waziri wa Masuala ya Uhalifu wa kifedha akizungumza na New York Times.

''Hakuna maswali yoyote juu ya kuhusishwa kwa Korea Kaskazini'', alisema.

Mamlaka nyingine zilitaja kughushi huko kama shambulizi baya la mfumo wa fedha wa Marekani.

Hata hivyo , kipaumbele cha FBI kilikuwa kusitisha usambazaji wa fedha hizo katika taifa la Marekani.

 

 

No comments