RASMI: JONAS MKUDE ASIMAMISHWA SIMBA
BAADA ya kutoonekana dimbani katika mechi mbili ambazo klabu ya Simba imecheza tangu irejee kutoka Afrika Kusini, hatimaye kilicho nyuma ya pazia juu ya kiungo fundi Jonas Mkude kimeonekana.
Inadaiwa kuwa kiungo huyo amesimamishwa baada ya kutoingia kambini baada ya timu kurejea kutoka Afrika Kusini katika mchezo wa kwanza wa robo fainali dhidi ya Kaizer Chiefs.
Taarifa kutoka Simba zinadai siku ya pili baada ya kurejea kutoka kwa Madiba Jumanne Mei 18, wachezaji wote wa kikosi hicho walirejea kambini ila Mkude hakuwepo tena bila ya sababu maalumu.
Siku aliyokwenda kambini Mkude alitoa sababu zake, jambo ambalo si kocha, Didier Gomes wala Meneja, Patrick Rweyemamu aliyeikubali. Baada ya sababu yake kugonga mwamba, alitakiwa kuwa nje hadi baada ya mechi ya marudiano na Amakhosi.
Taarifa zilieleza zaidi kuwa hata baada ya mechi na Kaizer Chiefs, alikataliwa kurejea kambini.
Suala hilo la
kinidhamu ambalo bado hawajaliweka wazi Simba kuwa Mkude amefanya nini tayari
limepelekwa hadi kamati ya nidhamu ambayo itatoa adhabu yake baada ya
kumsikiliza kiungo huyo.

Post a Comment