NDUMBARO: VIONGOZI ZINGATIENI MATUMIZI BORA YA ARDHI

NA STEPHANO MANGO, TUNDURU
WAZIRI wa Maliasili na Utalii Dkt Damas Ndumbaro, amewataka viongozi wa Serikali
wilayani Tunduru mkoanin Ruvuma, kusimamia mpango wa matumizi bora ya ardhi ili
kukomesha vitendo vya uvamizi wa maeneo yaliyotengwa kwa kwa ajili ya uhifadhi
wa wanyama na shughuli za kitalii.
Waziri Ndumbaro ametoa kauli hiyo katika kikao kazi na viongozi wa
wilaya hiyo kuhusiana na mikakati ya kukabiliana na tatizo kubwa la uvamizi wa
wafugaji kwenye hifadhi na shughuli mbalimbali za kibinadamu katika
maeneo yasiyoruhusiwa.
Alisema, viongozi wa serikali ndiyo wenye jukumu la kusimamia matumizi ya ardhi
kwa kuweka utaratibu ambao utakomesha vitendo vya wafugaji
kupeleka na kuishi kwenye hifadhi za Taifa na mapori yaliyotengwa kwa ajili
ya utalii.
Ndumbaro alisema, kuanzia sasa serikali kupitia wizara yake haitakuwa na mzaha
kwa watu watakaovamia na kufanya shughuli za kibinadamu kwenye maeneo hayo, na
kuwataka wananchi katika wilaya hiyo kufuata sheria na kuheshimu mipaka
iliyowekwa ili kuepuka matatizo.
Ameiagiza Halmashauri ya wilaya kutoa kipaumbele kwa idara ya maliasili kwa
kuipatia vifaa na kuitengea fedha za kutosha ili iweze kutekeleza vyema
majukumu yake badala ya kuona kama haina mchango wowote.
Alisema, kila halmashauri hapa nchini ina idara ya maliasili lakini jambo la
kusikitisha idara hiyo imeachwa kama mtoto yatima hivyo kushindwa kutekeleza
wajibu wake kama sheria inavyotaka.
Aidha, amempongeza Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Julius Mtatiro kwa kazi nzuri
anayofanya kusimamia uhifadhi wa maliasili na kuwataka watendaji wengine
wa serikali kuiga utendaji kazi wa mkuu huyo wa wilaya badala ya kumuacha
akihangaika pekee yake.
Mbunge wa jimbo la Tunduru Kaskazini Hassan Zidadu Kungu alisema, kati ya mwaka
2019/2020 zaidi ya wananchi 24 wameuawa na wanyama wakali hususani Tembo
wanaotoka hifadhini na kwenda kwenye makazi ya watu.
Alisema, kutokana na tatizo hilo ipo haja kwa wizara ya maliasili kuwa na
mikakati mbadala ya kukomesha matukio ya wananchi kuuawa na wanyama wakali na
kuweka mipaka itakayoonesha sehemu za hifadhi na makazi ya wananchi ili
kuepusha muingiliano kati ya watendaji wa wizara na jamii.
Kungu, ameiomba wizara ya maliasili kuhamisha kikosi maalum cha kuzuia
ujangili kanda ya kusini (KDU) kutoka Songea ambako hakuna hifadhi
wala shughuli yoyote ya utalii na kuhamishia shughuli zake wilayani
Tunduru ambako ndiko sehemu sahihi.
Mkuu wa wilaya ya Tunduru Julius Mtatiro alisema, katika kipindi cha mwaka
2018/2020 jumla ya watu 78 wamekamatwa wakifanya shughuli za ujangili kwenye
hifadhi ya Taifa ya Nyerere.
Mtatiro ameipongeza wizara ya maliasili na utalii kwa mpango wake
wa kutoa kifuta machozi na kifuta jasho kwa waathirika wa wanyama wanaoharibu
mazao na wanaosababisha vifo kwa wananchi.
Hata hivyo alisema, changamoto kubwa katika kukabiliana na vitendo vya ujangili
na uvamizi kwenye hifadhi ni upungufu wa watumishi wa idara ya maliasili kwenye
halmashauri kwani waliopo ni tisa kati ya mahitaji ya watumishi 31.
Alitaja changamoto nyingine ni uvamizi wa mipaka kutokana na shughuli za
kibinadamu, vitendea kazi,wafugaji kuingiza makundi makubwa ya mifugo ambapo
ameiomba wizara hiyo kuisaidia katika operesheni za kuondoa mifugo kwenye
hifadhi ya Nyerere.

Post a Comment