MWANAANGA WA CHOMBO CHA KWANZA KUTUA KWENYE MWEZI AFARIKI

Na Danny Matiko ...
- Ni Michael
Collins Wa Marekani, Rubani Wa Apollo 11.
MWANAANGA Michael
Collins (90) ambaye ni miongoni mwa wanaanga watatu wa kwanza kusafiri kutoka
duniani kwenda kutua mwezi, ameaga dunia nchini kwao Marekani Aprili 28 mwaka
huu 2021.
Ukurasa huu ukiwa
ni miongoni mwa wadau wa habari za masuala ya anga za juu na sayansi zake,
unaangalia jinsi safari hiyo ilivyokuwa, na pia kunukuu maelezo ya mwanaanga
huyo katika safari hiyo.
Ikumbukwe kuwa
Collins wakati huo akiwa na umri wa miaka 39, ndiye alikuwa rubani wa chombo
cha Apollo 11 katika safari ya kurejea duniani.
SASA Endelea...
JULAI 20, 2019,
taaluma ya sayansi ya utafiti wa anga za juu duniani ilisherekea miaka 50 tangu
binadamu aliposafiri kutoka duniani kwenda kutua na kutembea kwenye ardhi ya
mwezi mwaka 1969.
Safari hiyo na
zingine 6 zilizofuatia hiyo kwenda kutua kwenye mwezi, mpaka wakati huu ni zile
zilizoandaliwa na shirika la anga za juu la Marekani (NASA).
Aidha, inafurahisha
na kutia moyo kwamba zimerejea upya jitihada za mataifa mbalimbali kutaka
kutuma watu wao kwenda kuishi kwenye mwezi, kwa ajili ya kuchimba madini ya
huko na kuyaleta duniani.
Madini hayo
yataweza kutumika katika uundaji bidhaa za viwandani kwa kutumia teknolojia ya
kisasa, na hivyo kuzidi kudumisha maendeleo ya sayansi na teknolojia duniani.
Katika safari hiyo
ya kwanza mwaka 1969, chombo cha anga za juu kilichotumiwa na binadamu katika
safari hiyo kilipewa jina la Apollo 11, na ambalo hapa tutaona maana yake.
Apollo ni jina la
"Mungu wa Anga" katika tamaduni za Kale wakati wa enzi ya dola za
Kigiriki na Kiruma, ambapo pia Mwezi ulikuwa na Mungu wake aliyefahamika kwa
jina Diana.
Apollo na Diana
walikuwa watoto pacha, na hivyo NASA waliamini kuwa Apollo kutoka duniani
alikuwa anakwenda kumsalimia ndugu yake Diana kule kwenye mwezi, na kwamba kule
angepokelewa salama salimini.
Aliyeshauri jina
hilo la Apollo ni mtaalamu wa masuala ya anga za juu, Dkt. Abe Silverstain,
ambaye pia ndiye alisaidia kubuni na kusimamia ujenzi wa mtambo wa kituo kikuu
cha kurushia Apollo kwenda anga za juu.
Kituo kikuu hicho
cha roketi za anga za juu cha 'Kennedy Space Center,' kipo Jimbo la Florida.
Dkt. Silverstain
mwenye asili ya Uyahudi alizaliwa nchini Marekani, alifariki mwaka 2001 akiwa
na umri wa miaka 92.
Katika safari hiyo
ya kwanza kwenda kwenye mwezi mwaka 1969, watu 3 waliokwenda huko ni kamanda
mkuu wa safari hiyo, Neil Armstrong (mwaka huo akiwa na umri wa miaka 39),
msaidizi wake, Edwin Buzz (39), na rubani Michael Collins (39).
Hata hivyo, wakati
Armstrong na Buzz walipotelemka na kutembea kwenye ardhi ya mwezi, rubani
Collins alisalia ndani ya Apollo akiwasubiri hao wenzake ili wakirejea kwenye
chombo hicho safari ya kurejea duniani ianze.
Safari hiyo ya
kwenda kwenye mwezi na nyinginezo zilizofuata kwa miaka 3 mfululizo (1970, 1971
na 1972), zilihusisha jumla ya binadamu 21 katika safari 7 za chombo hicho cha
Apollo.
Apollo hizo ni
namba 11 yenyewe, namba 12, 13, 14, 15, 16, na 17, ambapo namba 13 ilikumbwa na
hitilafu kubwa huko anga za juu na kushindwa kutua kwenye mwezi, na hivyo
kuvunja safari na kurejea duniani.
Miongoni mwa hao binadamu
21, 6 ambao kimsingi ndio walikuwa marubani wa vyombo hivyo, walikuwa wakisalia
ndani ya vyombo hivyo katika anga ya mwezi wakati wenzao 2 wakishuka kutua na
kutembea kwenye ardhi ya mwezi.
Pamoja na maelezo
mengi ambayo yalishatolewa na yanaendelea kutolewa kuhusiana na safari hizo
tangu mwaka huo 1969 hadi mwaka 2019 ambao ulikuwa ni wa 50, nimeona ni vyema
tumwangalie rubani Michael Collins ambaye sasa ni marehemu.
Baadhi ya sababu za
kumwangalia mwanaanga huyo ni hizi, kwamba:-
1. Alikuwa rubani
wa chombo cha anga za juu cha Apollo namba 11, katika safari ya uzinduzi wa
safari za binadamu kwenda kutua kwenye mwezi.
2. Alikuwa amepewa
amri nzito na wakuu wa NASA iliyomtaka kuondoka na chombo chake kurejea peke
yake duniani, endapo wenzake wale wawili wangekumbwa na ajali mbaya pale kwenye
mwezi na kushindwa kurejea chomboni.
3. Aliporejea
aliandika kitabu maarufu kiitwacho, "Carrying the Fire" (kubeba moto
kwenda kwenye mwezi), na ambacho pia tunapata baadhi ya maelezo yake ya
kusisimua kuhusiana na safari hiyo ya kwanza ya binadamu kwenda kukanyaga
mwezi.
4. Alikuwa
amehitimu urubani na kutunukiwa cheti maalumu cha urubani wa kuendesha ndege
katika mazingira magumu.
Jina lake lipo
kwenye orodha ya kihistoria ya mafanikio hayo ya binadamu katika nyanja ya
utafiti wa anga za juu, akiwa amekwisha tunukiwa medani 6, ikiwemo medani ya
kutukuka ambayo hutolewa na Rais wa Marekani.
Nishani hiyo ni
"Presidential Medan of Freedom," hutolewa kwa mtu aliyechangia
ujasiri wake katika kuhakikisha udumishwaji wa usalama wa taifa, amani, na
maendeleo yoyote ya binadamu kwa maslahi ya umma.
Collins anaeleza
hivi:
"Hakika,
naweza kusema kuwa siku hiyo ya kuondoka duniani kwenda kwenye mwezi ilikuwa ni
kubwa kuliko zote kwenye maisha yangu tangu kuzaliwa.
"Siku hiyo ya
Julai 16, 1969 tuliamshwa saa 10 usiku wa kuamkia safari hiyo, ili kujiandaa
kwenda ughaibuni.
"Tukiwa
watatu, yaani mimi Collins, Armstrong, na Buzz, tulipeana salamu za asubuhi na
kuanza harakati kubwa za kujiandaa.
"Baada ya
maandalizi ya kawaida ya kibinadamu, ikiwemo kufanya mazoezi ya viungo,
tulikwenda kwenye chumba cha kupima afya zetu ili kuwa tayari.
"Baada ya hapo
tulikwenda kupata mlo wa chakula cha kifungua kinywa.
"Baada ya
hapo, yaani majira ya saa 12 alfajiri, tuliingia kwenye ukumbi wa mikutano na
kukuta wamekusanyika wakuu kibao wa NASA kutoka ngazi zote.
"Akilini
mwangu nilijua hiyo ilikuwa siku yangu ya kwenda kufa huko anga za juu; na
zaidi sana nilimwangalia Armstrong na kuingiwa na majonzi kwa sababu ya kuhofia
usalama wake pale angekuwa wa kwanza kukanyaga ardhi ya mwezi.
"Licha ya NASA
kutuhakikishia usalama wetu pale kwenye mwezi, hata hivyo sote watatu
tulifahamu kuwa kulikuwa na uwezekano mkubwa binadamu kuzama katika ile ardhi
teketeke ya mwezi.
"Tuliketi
kwenye eneo letu humo ukumbini, ambamo zilitolewa hotuba mbalimbali za kututia
moyo, ikiwemo kuhakikishiwa na wakuu kuwa usalama wetu ulikuwa umezingatia
katika utafiti wa kina kuhusu mazingira ya mwezi.
"Niliweza
kuangalia kupitia dirishani na kuiona Apollo ikiwa kubwa na ya kutisha, huku
ikiunguruma mithili ya kiwanda kikubwa.
"Baada ya
kutolewa hotuba kadhaa, tulielekezwa kwenda chumba maalumu ambamo tulivaa
mavazi rasmi kwa ajili ya safari za anga za juu.
"Hotuba ya
Mkurugenzi Mkuu wa NASA ndiyo ilitupatia ujasiri zaidi, ambao nakumbuka hadi
leo hii.
"Katika hotuba
hiyo, mkuu alisema kwamba safari ambayo ilisubiriwa na Wamarekani wengi tayari
imewadia, na kwamba taifa lote lilikuwa nyuma yetu kushuhudia mtanange ambao
tunakwenda kuukabili katika safari hiyo muhimu.
"Alisema NASA
ilikuwa imefanya maandalizi yote muhimu, ikiwemo kuhakikisha usalama wetu
safarini.
"Mkuu
aliendelea kueleza kwa kirefu historia ya mtiririko wa mambo na matukio
kwelekea siku hiyo, ikiwemo uundaji wa Apollo, aina ya mavazi tutakayovaa
safarini, vyakula, malazi yenu ndani ya chombo hicho, na mengineyo mengi.
"Alitaja sifa
za kila mmoja wetu, ambazo zilipelekea kuchaguliwa kuwa wa kwanza kwenda
kuukabili mwezi.
"Akihitimisha
hotuba yake, mkuu huyo wa NASA alisema:
'Sisi NASA, kwa
upande wetu, tumekamilisha majukumu yetu katika safari hii; tunabaki tu duniani
kuwafuatilia huko anga za juu.
'Chombo cha Apollo
kina nguvu kubwa kupita kiasi, lakini hakikisha mnakidhibiti, na si chenyewe
kiwadhibiti ninyi binaadamu.
'Chunga muda na
kasi ya chombo ili msijikute mkipishana na mwezi.
'Mpaka hapo naweza
kusema sasa kazi inabaki kwenu wote 3. Kila la kheri safarini,' alihitimisha.
"Wageni
waalikwa walipiga makofi na kusimama wima kutoka kwenye viti vyao, ambapo
taratibu sisi tulisimama na kuanza kuondoka kwelekea mlangoni ili tutoke nje na
kwenda kupanda chombo tayari kwa safari.
"Tulipotoka
nje tulikuta umati wa watu wakitupungia mikono huku sisi tukijibu, ambapo pia
tuliingia kwenye gari ambayo ilitusogeza hadi kwenye mlango wa Apollo.
"Huku
tukifuatana na ofisa mmoja wa NASA, tuliingia ndani ya lifti ambayo ilitumia
sekunde 40 kutuyanyua hadi mlango wa kuingia ndani kabisa ya Apollo.
"Kumbuka
Apollo ilikuwa na urefu wa mita 110 kwenda juu, hivyo chumba chetu wanaanga
kilikuwa jirani kabisa na ncha ya chombo hicho.
"Tuliingia
ndani ya chombo hicho, ambapo tuliketi nyema na kusubiri saa ya chombo
kuondoka; yaani saa 3 asubuhi ya Julai 16, 1969.
"Ofisa
aliyetusindikiza hadi chomboni alituaga kwa kutwambia, 'guys take care,'
(jamani kuweni makini).
"Tulisubiri
tukiwa kimya, huku tukiangalia-angalia mitambo na vifaa kadhaa, ilimradi muda
uzidi kusogea tuanze safari.
"Muongozaji
mkuu wa Apollo akiwa kwenye chumba cha duniani kwa ajili ya kutuongoza,
alituuliza kila mmoja wetu tunajisikiaje kiafya na kisaikolojia, tukamjibu tupo
tayari kabisa.
"Ilipotimu saa
3:32 asubuhi tuliarifiwa kuwa Apollo inaondoka, na ghafla na kwa kasi kubwa
tuliondoka duniani kwenda kwenye mwezi.
"Mara moja
tulishika hatamu ya kukithibiti chombo hicho kikubwa, tukisoma alama zote
kwenye chumba cha mitambo kilichoitwa 'Command Module' (chumba cha kwendesha
Apollo).
"Apollo ikiwa
na uzito wa kilo milioni 3 pamoja na nishati ya mafuta mengi, iliondoka duniani
kwa kasi kubwa ya kilomita 40,000 kwa saa, sawa na kasi ya kilomita 11 kwa
sekunde.
"Uzito huo
mkubwa ulichangiwa na ukubwa wa roketi za kukiwezesha chombo kuwa na kasi ya
kuishida nguvuasili ya uvutano ya dunia, na kiasi kingi cha nishati ya mafuta
na hewa za gesi, kwa ajili ya matumizi ya safari.
"Wakati chombo
hicho kikipaa kwa kasi, tuliomo ndani tulitulia kimya na kuangalia kompyuta
zikielekeza.
"Binafsi
nilitarajia tukio baya la mlipuko kutokea na kututeketeza sawia, lakini kumbe
nilikuwa na mawazo potofu tu.
"Ndani ya muda
mfupi tuliweza kuchana ule ukanda hatari wa tabaka la 'ozone' na kutokea anga
ya juu kabisa.
"Majira ya
mchana wa saa 8 hivi chombo kilifika katika anga tulivu, ambapo kama ilivyokuwa
imepangwa kilikupunguza mwendo na kusimama angani, huku kikielea katika anga
hiyo.
"Hapo
lilifanyika zoezi gumu na la hatari, kwani kachombo kadogo ambako ndiko
kangetumiwa na akina Armstrong na Buzz kushuka hadi kutua mwezini kalikuwa
katikati ya Apollo, hivyo ilibidi kukachomoa kutoka hapo ili kukaleta mbele
kabisa ya Apollo.
"Zoezi hilo
lilifanyika kama ilivyopangwa, ambapo tulifaulu kukaleta kachombo hako upande
wa mbele ili tutakapofika kwenye anga ya mwezi iwe rahisi kukaachanisha na
chombo kikuu cha safari.
"Mipango
ilikuwa kuwa wakati Apollo itakapowasili katika anga ya mwezi, Armstrong na
Buzz wangeingia kwenye kachombo hako ili kaweze kuwashusha hadi kutua katika
mwezi.
"Mimi
ningebaki ndani ya Apollo wakati ikiendelea kuelea kwenye anga ya mwezi
nikiwasubiri wanaanga hao wapae wakiwa ndani ya kachombo hako, na kuja
kukaunganisha na Apollo ili tuanze safari ya kurejea duniani.
"Baada ya
kuunganisha kachombo hako na Apollo tungefaulisha (kutoka kwenye kachombo hako)
shehena ya mchanga na mawe walivyokusanya kule mwezini, ili tuvilete duniani
kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa kimaabara duniani.
"Baada ya
kufaulisha shehena hiyo, kachombo hako tunge kasukuma kaambae hadi kuanguka
kwenye ardhi ya mwezi na kulipuka.
"Zoezi hilo
lingewezesha Apollo kuzidi kupungua uzito na kuondoka kwa kasi kutoka anga ya
mwezi kurejea duniani, huku pia ikiwa ni nyepesi.
"Hivyo, hiyo
ndiyo ilikuwa sababu ya kukachomoa kachombo hako kutoka katikati ya Apollo na
kukatanguliza mbele.
"Pia, wakati
tukiwa tumesimama kwa muda kwenye eneo hilo la anga ya dunia majira hayo ya saa
8 mchana kwa saa za duniani, tulikula chakula na kisha kukagua mfumo wote wa
Apollo ili kuhakiki uimara wa chombo hicho.
"Chakula
kilikuwa kimewekwa kwenye paketi ndogondogo, sawa na paketi za 'take away',
huku kila mlo ukiwa imeandikwa siku na muda wa kutumiwa.
"Mfano kwamba,
mkate, chai na juisi vitumike asubuhi ya tarehe fulani; chapati, mchuzi na
nyama ni chakula cha mchana wa siku na saa fulani; wali, kuku, mchuzi na tunda
ni chakula cha siku ya tarehe tajwa na saa husika.
"Hivyo, kwa
vile vyakula vyote vilikuwa ni vikavu (vimekaushwa), tulitakiwa kupasha maji ya
moto na kuvitumbikiza humo na kisha kula kama mlo laini wa kawaida.
"Aidha, katika
kusafisha kinywa, tulitafuna kitu kama big-G maalumu ya kusafisha kinywa na
kutema kwenye mifuko maalumu ya plastiki.
"Katika
kujisaidia, kulikuwa tishu na kachumba kadogo hivi ambako tulijibanza humo na
kujisaidia ndani ya mifuko ya plastiki ikiwa na dawa ya kuua vimelea.
"Kama ni
mkojo, kulikuwa na kijisehemu ambamo tulijisaidia, na kisha mkojo huo
kupitishwa kwenye bomba na kutolewa nje ambapo ulisambaratishwa katika anga.
Pia, "mabaki
ya chakula, choo kubwa, nk, viliwekwa kwenye hiyo mifuko ya plastiki ili
turejee navyo duniani kuepuka kuchafua anga.
"Katika
kufanyia chumba usafi, tuliweza kuwasha vitufe maalumu ambavyo vilitoa upepo
mkali chumbani na kufyonza kila kitu kisichotakiwa chumbani na kuingizwa kwenye
mifuko maalumu ya plastiki na kuhifadhiwa chomboni.
"Chumba
kilikuwa kikubwa kiasi, ambapo kila mmoja wetu alikuwa na kitanda chake ambamo
tuliweza kupumzika wakati chombo kikiendelea na safari kama kawaida.
"Katika kulala
tulipeana zamu, ili mmoja abaki macho kuweza kufuatilia hesabu za kompyuta
ndani ya chombo hicho.
"Ndani ya
chumba hicho kulikuwa na kompyuta 2 zenye kusoma taarifa zinazofanana; hiyo
ikiwa na maana kwamba kasoro yoyote; mathalani, kutofautiana kompyuta hizo,
mara moja tungeweza kubaini kasoro na kutoa taarifa kwa waongozaji wetu.
"Kadhalika,
chumba cha kutuongoza kilikuwa na kompyuta kama hizo, katika kufuatilia safari
hiyo kupitia taarifa zinazofaa.
"Kuna wakati
tulisafiri bila kuuona mwezi, ingawa muda mwingi tulikuwa tumeulenga moja kwa
moja ili tukutane nao huko anga ya juu.
"Ndipo siku ya
3 safarini katika kuamkia siku ya 4 ya kutua mwezini, tulitokewa na kitu cha
kustaajabisha nje ya chombo chetu.
"Kitu hicho ni
mfano wa chombo cha anga ambacho kilikuwa na mwanga mkali mno, huku kikimudu
kwenda sambamba na kasi ya Apollo ambayo wakati huo ilikuwa ni kilomita 26,000
kwa saa.
"Mwendo wa
Apollo wakati huo ni ule unaoitwa "transonic speed" (kasi sawa na
kasi ya sauti), ambapo licha ya kutouona mwezi wakati huo, pia tulitarajia
kuanza kujiandaa kutua.
"Chombo hicho
cha kigeni kilikatiza mbele ya Apollo na kuizunguka na kukaa sambamba nayo,
kama vile gari moja ikitaka kuovateki nyingine.
"Mara moja
tulitoa taarifa duniani kwa chumba cha kuongoza Apollo, huku tukiwa na woga,
kwamba kuna chombo cha kigeni kimetutokea na kinakwenda sambamba na Apollo.
"Muongozaji
mkuu wa Apollo duniani alihoji maswali kadhaa na kisha kujibu kwamba hiyo ni
UFO, na kuongeza kuwa 'achana nacho, nyie zingatia safari tu, mpo jirani na
anga ya mwezi.'
"Muongoza
Apollo alisema kuwa tuwaachie wao NASA kazi ya kufuatilia chombo hicho cha
kigeni.
"Punde tu hivi
chombo hicho cha kigeni kilikula kona na kupotea kwenda kusikojulikana.
"Baadaye
tulijishangaa kwa nini hatukukumbuka tena kuulizia NASA kuhusiana na chombo
kile.
"Tuliingia
kulala, lakini asubuhi niliamka na kushangaa kuuona mwezi ukiwa mkubwa kupita
kawaida na ukiwa tayari upo chini ya anga badala ya kuwa juu kama
ilivyozoeleka.
"Tulielekezwa
na waongozaji wetu wa duniani kuwa tayari kwa vile tayari tupo kwenye anga ya
mwezi, na kutakiwa kuanza zoezi la kupunguza mwendo wa Apollo ili tuweze
kufanya maandalizi ya kutua.
"Hiyo ikiwa ni
siku ya 4 tangu tulipoondoka duniani, ndipo Armstrong na Buzz walihamia kwenye
kale kachombo kadogo tayari kushuka kwenda kutua kwenye mwezi.
"Niliwatakia
kheri kwa kuwaambia 'hey, guys take care!' (kuweni makini), waliitikia kwa
kusema 'goodbye!' (kwa heri).
"Punde tu
hivi, kwa mujibu wa ratiba tuliyopewa, nilibonyeza kitufe cha kufyatua kale
kachombo ili kaachane na Apollo na kushuka kwenda kuikabili ardhi ya mwezi na
kutua juu yake.
"Zoezi hilo
lilifaulu vyema, huku nikisalia ndani ya Apollo kwendelea kuzunguka-zunguka
kwenye anga ya mwezi nikiwasubiri hao marafiki zangu warejee ili tuanze safari
ya kurejea duniani.
"Hakika,
nilijawa na mawazo mengi, na kukumbuka ule usemi wa wakuu wa NASA kwamba 'kama
akina Armstrong watakwama mwezini, wewe utapewa amri ya kuondoka pekee yako
kurejea duniani na kuwaacha huko.'
"Hiyo
ingemaanisha kuwa Armstrong na Buzz wameangamia peke yao pale kwenye ardhi ya
mwezi.
"Hata hivyo,
baadaye sana nilipokea wito kutoka kwao akina Armstrong wakisema wanarejea kwa
Apollo (kutoka kwenye mwezi).
"Nilijawa na
furaha pale nilipoona kale kachombo kadogo kalikowabeba kakija kuungana na
Apollo.
"Baada ya
maandalizi yote kukamilika, ikiwemo kutumia mpira wenye upepo mkali ili
kupuliza vumbi la mwezini kutoka kwenye mavazi yao, safari ya kurejea nyumbani
ilianza mara moja.
"Nilifyatua
kitufe cha kuiondoa Apollo kutoka anga ya mwezi, ambapo punde tu hivi chombo
hicho kilishika kasi yake 'kupaa' kutoka kwenye anga ya mwezi kuelekea duniani.
"Nasema
tulipaa kutoka kwenye mwezi kuja duniani, kwa vile wakati tukiwa hapo kwenye
mwezi tuliiona dunia ikiwa juu kama vile tunavyouona mwezi tukiwa duniani.
"Tofauti ni
kuwa dunia ilionekana kubwa na ikiwa na rangi nzuri ya bluu, ambapo ilipita
taratibu juu ya anga ya mwezi kama hivi tunavyouona mwezi ukipita kwenye anga
ya dunia.
"Hatimaye siku
ya 8 tangu tulipoondoka duniani kwenda kwenye mwezi, tuliweza kuwasili duniani
na kupokewa kwa shangwe kubwa.
"Tuliingizwa
kwenye chumba maalumu kwa uchunguzi wa kiafya, ambapo kwa siku 21 tulikuwa
kwenye karantini mahsusi.
"Baada ya
kukamilika karantini hiyo tuliachiwa huru na kurejea uraia kuungana na familia
zetu, na kwendelea na maisha kama kawaida.
"Tukiwa
uraiani tulitoa mihadhara mingi, huku pia wanasayansi wakitumia maelezo yetu
katika kuandika vitabu na makala mbalimbali kuhusiana na uhalisia wa jiografia
na pia yalivyo mazingira ya mwezi."
Maelezo haya yamechukuliwa katika ukurasa wa facebook wa Salum Daudy

Post a Comment