MAKONGORO NYERERE AVUTWA UKUU WA MKOA


Makongoro Nyerere achafua hewa | Mtanzania

 MTOTO pekee wa kuzaliwa wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere anayejihusisha na siasa za majukwaani, Makongoro Nyerere, amevutwa na kupewa kazi ya Ukuu wa Mkoa, akipangiwa mkoani Manyara.

Hiyo ni kufuatia uteuzi wa leo uliofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan. Makongoro, ambaye aliwahi kujiondoa CCM na kujiunga na NCCR Mageuzi enzi za Augustine Mrema na kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Arusha mjini kabla ya kurejea, amewahi pia kuwa Mbunge wa Afrika Mashariki.

Makongoro pia alikuwa miongoni mwa makada zaidi ya 30 waliojitokeza kuwania nafasi ya kuteuliwa na CCM ili wagombee urais mwaka 2015, nafasi ambayo iliangukia kwa hayati Rais John Pombe Magufuli.

Licha ya familia yao kuwa maarufu, lakini watoto wa Baba wa Taifa wamekuwa adimu katika teuzi za serikali, ingawa imekuwa karibu muda wote katika matunzo ya mjane wake, Mama Maria Nyerere na imekuwa ikimtambua katika shughuli nyingi za kitaifa. Makongoro ndiye humsindikiza mama yake kwenye mialiko mingi anayopata.

No comments