DIAMOND PLATNUM TUNAMKUZA WENYEWE

KWAMBA Diamond Platnum ni msanii mkubwa wa muziki wa kizazi kipya, siyo jambo la kutia mashaka tena. Amethibitisha hivyo mara nyingi na kwa namna zote, ndani na nje ya uwanja.
Ndani ya uwanja,
Diamond ndiye msanii mwenye mafanikio zaidi kimuziki, kwani aina ya muziki wake
na video zake, zimemfanya kuwa msanii ghali zaidi kuliko wote hadi sasa katika
tasnia hiyo.
Ndiye msanii ambaye
ili kumchukua aweze kufanya onyesho, kwampasa anayemhitaji kutoboka sana
mfukoni, tofauti na wasanii wengine. Hii ndiyo sababu inayomfanya kutoonekana
katika matamasha yaliyozoeleka, yanayowakutanisha wasanii karibu wote maarufu.
Diamond alishaacha
kuonekana kwenye tamasha maarufu la Fiesta, ambalo wajuzi wa mambo wanasema
ndiyo sababu ya kumfanya msanii huyo kuanza kupigwa zengwe na nyimbo zake
kutopigwa katika kituo kimoja kikubwa cha redio na televisheni kinachohusishwa
na uendeshaji wa tamasha hilo.
Sababu kubwa ni
malipo. Inasemekana msanii huyo alidai fedha nyingi kuliko wengine ambazo
ziliwashinda na hivyo kuondolewa. Diamond ndiye pia msanii mwenye mialiko mingi
nje ya nchi kimuziki na jambo lingine, ndiye msanii ambaye siyo tu
amewashirikisha wasanii wengi wakubwa wa nje, lakini pia ndiye msanii
aliyeshirikishwa zaidi na wasanii wakubwa wa nje kuliko wote Tanzania.
Jambo ambalo
linapelekea kumfanya msanii huyo kuwa ghali, maarufu na mkubwa kuliko wote kwa
sasa, ni kutokana pia na namna video zake zinavyofanya. Video zake zinadaiwa
kuwa zina gharama kubwa zaidi kuliko za wasanii wengine.
Siyo tu zina
gharama kubwa, lakini pia zinatajwa kuwa na ubora wa hali ya juu, kwa namna
ambavyo wanenguaji wake wanavyovaa, nguo nzuri, za bei mbaya na kwenye maeneo
mazuri, lakini pia watengenezaji wa video zake ni wenye uzoefu, wenye vifaa
bora na bei kubwa.
Nje ya uwanja,
Diamond Pllatnum ni msanii mkubwa kwa maana halisi, kwani ana mafanikio mengi
ya kifedha. Ndiye msanii anayetumiwa kutangaza kampuni nyingi na kubwa kwa
malipo mazuri kuliko msanii mwingine ye yote. Au kwa lugha ya kisanii, ndiye
msanii mwenye ubalozi wa brand nyingi.
Ndiye msanii pekee
nchini anayemiliki chombo cha habari, akiwa ni mmiliki mwenza wa Wasafi Media,
yenye redio na televisheni ambayo ndiyo inayosikilizwa na kufuatiliwa zaidi na
vijana kwa sasa. Pia ana mtandao anaouza nyimbo za wasani wote nchini.
Ndiye msanii mwenye
lebo yenye mafanikio makubwa kuliko lebo zote nchini, akiwa ni bosi wa wasanii
zaidi ya wanne, wote wakiwa ni wakubwa. Katika lebo yake ya Wasafi, anawamiliki
wasanii RanVany, Mbosso, Lavalava, Zuchu.
Ndiye msanii mwenye
tamasha lake binafsi, linalojulikana kama Wasafi Festival, ambalo lilipaswa
kuwa linafanyika kila mwaka, lakini kutokana na matukio kadhaa, limeshindwa
ku-mantain.
Mafanikio haya ya
Diamond, ndiyo yanayowafanya mashabiki wengi kumkuza zaidi, kwani hivi sasa
kila wanapotajwa wasanii bora kwa kila jambo Afrika, macho yao kuangalia namba
ambayo Diamond Platnum atakuwa ameshika.
Wakitajwa wasanii
wenye fedha nyingi zaidi Afrika, mashabiki wa Tanzania huangalia kama Diamond
yupo na inapotokea hayumo, wanaomshabikia hutilia mashaka orodha hiyo, wakati
mahasimu wake hushangilia.
Kwa nini mahasimu
wake wanashangilia? Wanashangilia kwa sababu kwa ndani ameshashinda kila kitu,
hana tena wa kumlinganisha naye. Hofu ya mahasimu ni kumuona akichomoza Afrika
na baadaye duniani.
Wakitajwa wasanii
wanaofuatiliwa zaidi mitandaoni, macho ya mashabiki wa Tanzania huangaza kuona
kama jina la Diamond litakuwepo na inapotokea halipo katika nafasi ya Kumi
Bora, huanza kutilia mashaka ukweli wa habari hizo.
Kama kawaida,
mahasimu wake hushangilia na kumuona kuwa si lolote si chochote kwa Afrika.
Kitu ambacho
mashabiki hawakitambui ni kwamba kile kitendo tu cha kumtazamia msanii huyo
kuwa anaweza kushika nafasi katika chati za Afrika au hawezi, maana yake ni
kwamba hizo ndiyo levo ambazo anatarajiwa awe. Manaa yake pia ni kuwa kwa levo
za Bongo, ameshatoboa kila tobo.

Post a Comment