KUELEKEA DERBY YA KARIAKOO, SIMBA NA YANGA
KABLA hawajaja wale
wachambuzi wetu wa baada ya mechi na vibwagizo vyao vya WHAT A MATCH!!, WHAT A
GOAL!!! kwa uzoefu wangu wa kutazama mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu,
nina machache nataka kuzungumza nikiutazama mchezo huu kabla haujachezwa siku
sita zijazo.
Kwanza tukubaliane
kwamba mwenye presha kubwa zaidi katika mechi hii ni Yanga. Kuna sababu kadhaa
za kwa nini awe na presha, lakini chache ni hizi..
1. Matumaini ya ubingwa
yamebakia bahati nasibu..
Kulikuwa na
matumaini makubwa ya mabingwa hawa wa kihistoria kuibuka na ubingwa msimu huu,
hasa baada ya wafadhili wao wakubwa, GSM kuamua kuingia kwa miguu miwili na
kusimamia mchakato mzima wa usajili wa wachezaji na benchi la ufundi. Walifanya
kazi kubwa na kila mmoja ameona.
Usajili wa
wachezaji wa viwango kama Calinyo, Fiston, Yocouba, Tonombe, Saido na Dickson
Job. Hawa ni wachezaji walioongeza thamani ndani ya timu na haikushangaza,
ilipoongoza Ligi na hivyo kuweka hai matumaini ya mashabiki. Baada ya kuongoza
kwa muda mrefu, taratibu ikaanza kupoteza makali na hatimaye hadi unaposoma
makala haya, kimahesabu, Yanga iko nyuma kwa pointi kumi kwa Simba.
Kwa hiyo, hii ni
moja kati ya sababu za msingi sana za kuipa Yanga presha. Wote ndani ya Yanga
wanajua, wachezaji, viongozi na mashabiki, kwamba ubingwa kwao msimu huu ni
miujiza na njia pekee ya kujiliwaza ni ushindi dhidi ya Simba.
Ili Yanga wapumue
na wawe na cha kusema, ni LAZIMA waifunge Simba Jumamosi ijayo. Watashindaje
mchezo huo, ni KITENDAWILI.
2. Kutocheza soka la kuvutia...
Presha nyingine
inayokumbana nayo Yanga kuelekea mchezo huo, ni ukweli kwamba wamekuwa hawana
soka la kuvutia kama ilivyo kwa wapinzani wao. Yes mpira ni magoli, lakini
katika wakati ambao soka pia ni biashara, burudani inahusika sana kwa
mashabiki.
Wachezaji, viongozi
na mashabiki wa Yanga wataingia katika mchezo huo wakijua wapinzani wao
wanacheza soka la kuvutia kuliko wao, hivyo njia pekee ya kuwatuliza, ni
KUWAFUNGA. Hata ucheze mchezo wa kuvutia vipi, ni lazima utoke na matokeo
chanya, vinginevyo, unakuwa kama Arsenal ya enzi za mwishoni mwa zama za Arsene
Wenger!
3. Imani ya mashabiki kwa kocha
mpya
Baada ya kumuondoa
kibaruani kocha Cedric Kaze, Yanga waliutangazia umma kuwa Juma Mwambusi,
ambaye ametumika sana msimu huu kama Kocha Msaidizi, atapewa timu awe Kaimu
Kocha Mkuu hadi mwisho wa msimu...na Of course mashabiki walielewa.
Kwamba klabu
itafute kocha bora taratibu ili aje aichukue timu aanze nayo msimu ujao.
Mwambusi amefanya kazi yake vizuri akipata matokea ya kawaida. Sijui nini
kimetokea, ghafla viongozi wamemleta kocha mpya na kumpa timu.
Yes, CV yake
inaonyesha ni kocha mzuri, pengine kuliko Gomez, kwani ana vikombe kama sita
hivi katika ufundishaji wake wa soka la Afrika, ingawa naye kama alivyo
mwenzake wa Simba, wana leseni ya Uefa.
Ameiongoza Yanga
katika mechi mbili. Yanga imeshinda mechi zote mbili chini yake, lakini zote ikionekana kupambana kwelikweli. Ni matumaini
ya wana Yanga kwamba timu yao iwe inawatisha wapinzani ndani na nje ya uwanja.
Presha hii ya
kocha, ipo zaidi kwa viongozi, kwa sababu, kwa vyovyote vile, kufungwa na Simba
ni kutokufaa kwa kocha huyo. Kama kuna eneo viongozi walicheza karata zao 'kwa
kubahatisha', ni kumruhusu huyu jamaa akae pale benchi kabla ya mechi hii. Ili
wabebwe tena na mashabiki, ni LAZIMA MNYAMA AFE KWA MKAPA.
Siku zote, hakunaga
mechi ndogo au isiyo na umuhimu zinapokutana timu hizi, bila kujali nani yupo
katika nafasi gani kwenye msimamo wa Ligi. Ukitazama, unaiona Simba kama timu
inayoingia ikiwa haina mashaka yoyote, kwani hata ikifungwa, bado itaendelea
kubakia pale juu, hata kama ni kwa muda.
Inaingia uwanjani
ikiwa mabega juu kila idara. Licha ya kuwa imecheza mechi mbili chini ya
wapinzani wao, lakini ndiyo wanaongoza Ligi Kuu, tena wakiwa juu kwa pointi
nne.
Katika michuano ya
kimataifa, imeingia robo fainali ya Kombe la Ligi ya Mabingwa Afrika, tena ikiwa imeweka historia
ya kuongoza kundi lao, ambalo lilikuwa na bingwa mtetezi Al Ahly. Unaweza
kubeza mafanikio haya kwa sababu tu ni shabiki wa Yanga, lakini kiukweli, hii
ni hatua kubwa sana katika soka letu la Bongo.
Simba pia inaingia
uwanjani ikijivunia uwezo wake wa kuumiliki mpira. Kwa mujibu wa takwimu za
kila baada ya mchezo, Simba ndiyo timu pekee iliyokuwa na wastani mzuri wa
kumiliki mpira katika mechi zake zote ilizocheza katika Ligi Kuu Tanzania Bara
msimu huu.
NINI KITATOKEA?
Yanga itaingia
uwanjani ikiwa na lengo moja tu, kuibuka na ushindi katika mechi ambayo
ikishinda, itakuwa na faida mbili.
Kwanza itapunguza
wigo wa tofauti ya pointi na kufikisha saba na pili itakuwa imewapa matumaini
upya mashabiki wao. Lakini ni wachezaji gani wataisaidia Yanga? Sina uhakika,
lakini nadhani mfumo wa 4-4-2 utawasaidia kusukuma mashambulizi langoni mwa
Simba.
Mfumo huu
unatengeneza mizani katika safu ya ulinzi na kiungo, kwani viungo hao
wanagawika, wawili wakisaidia ulinzi na wawili ushambuliaji. Washambuliaji wa
Simba ni wazuri, lakini ni wazito ukimuondoa Konde Boy.
Safu ya Ulinzi ya
Yanga inapaswa kuwa na walinzi wenye nguvu, hasa katikati na mmoja anayetumia zaidi
akili. Kwangu, Lamine Moro, japo ni mzuri, lakini ana hasira. Huyu asubiri
kwanza, aanze yule dogo mrithi wa Cannavaro, Ninja. Kama Dickson Job atakuwa
amepona majeraha, huyu anastahili kuwepo uwanjani, kwani licha ya ufupi wake,
lakini ana timing za aina ya akina George Masatu.
Kushoto na kulia
kwa Yanga sionagi kama wana tofauti sana, kwa hiyo hata wanaocheza sasa,
Kibwana na Adeyum wanaweza kuendelea na majukumu yao.
Kiungo cha chini
Yanga itahitaji huduma za Mwalimu Mukoko Tonombe na Feisal Salum. Hawa wana
nguvu, ari na uwezo mzuri wa kumiliki mpira. Hili ni eneo ambalo Yanga
inahitaji watu watulivu mno kiakili, kwa sababu wanakutana na wapinzani wenye
uwezo kama wao katika umiliki wa mpira. Hata hivyo, itabidi Feisal apunguze pia
presha, maana kuna wakati ni kama anapanik hivi!
Pale katikati, yule
dogo mtanashati wa Kireno akisimama na Saido, wanaweza kufanya jambo, hasa kwa
kuwa hawa hawana mambo mengi. Wanaweza kukontroo mpira na wana macho ya tai,
yenye uwezo wa kuona mnyama aliye umbali wa maelfu ya kilometa.
Wana kile watu wa
mpira wanaita penetration passes, yaani kwa kiswahili pasi mpenyezo, ambazo mtu
anakutana nazo kwenye nafasi. Itazame ile aliyopewa Yacouba siku Prisons
anaanguka pale Sumbawanga kwenye FA Cup.
Yacouba naona kama
anajimilikisha ile namba ya Sarpong. Huyu anastahili kuanza na kwa mawazo
yangu, aanze sambamba na Deus Kaseke. Kwa nini? Hawa wawili watataka ku-prove
kuwa wanaweza kucheza pacha kwa sababu kuna vitu wanafanana, navyo ni ari ya
upambanaji.
Kaseke amekuwa na
maana kubwa sana anapoingia dakika za mwishoni anazopewa, kiasi cha kujiuliza
kwa nini anabakia nje kwa muda mrefu. Khalid Mussa, Haruna Niyonzima, Ditram
Nchimbi na Bakari Mwamnyeto ni watu ninaotegemea pia kuwemo ndani ya 18.
Simshauri kocha kumpanga mlinda mlango
Metacha...
Kwa Simba, wataingia
tayari wakiwa washindi. Ushindi wa Simba Jumamosi si ushindi wa mabao, bali
matokeo. Shida kubwa ya Gomez itakuwa ni kujilinda ili asipoteze mchezo,
period!
Ushindi wa mabao kwake
ni bonasi tu, kwa nini? Wekundu hawana cha kupoteza kwa kupata sare, kwa sababu
wataendeleza wigo wao wa pointi kumi dhidi ya Yanga, huku michezo ikizidi
kupungua kabla ya ligi kumalizika.
Kwa kuzitazama timu
zilizobaki kucheza na Simba kabla ya msimu kumalizika, ni Yanga pekee ndiyo
unaweza kuiwekea fedha ya kuishinda Simba na bado bia baridi ikapita bila
wasiwasi. Na hii ndiyo mechi ngumu zaidi kwa Simba kuliko zote zilizopita na
kubaki.
Kwa maana hiyo,
Simba wataingia kwa kujilinda zaidi na bahati nzuri inao wachezaji wa
kuliwezesha hilo, kama ilivyotokea katika michuano ya Ligi ya Mabingwa
walipofanya hivyo ugenini.
Ili kulifanikisha
hilo, Gomez atakuja na mfumo wake wa siku zote akitafuta kujilinda, wa 4-2-3-1.
Ikimaanisha walinzi wake wataendelea kuwa ni wale wale kama hakutakuwa
majeruhi, Kapombe, Tshabalala, Wawa na Onyango. Pale juu ana machaguo mengi,
lakini Mkude, Lwanga na Nyoni wanaweza kuwa chaguo la kuanza na wawili kati
yao.
Kiungo cha
ushambuliaji pia machaguo ni mengi, lakini uzoefu unatuonyesha Bwalya, Chama na
Konde Boy wataingia na kuanza usumbufu kwa Yanga huku mshambuliaji mmoja wa
kumalizia, hauhitaji kumtaja jina, kwani yeyote kati ya Kagere, Mugalu na Bocco
anafaa.
Bwalya, Chama na
Konde Boy pia wanaweza kutumika kurudi nyuma na kujilinda kutoa msaada kama
presha itakuwa kubwa kutoka kwa wapinzani wao.
Golini kwa Simba
ataendelea kuwepo Manula, ingawa kwangu, siku zote nimekuwa nikimuona Benno
Kakolanya kuwa ni bora kuliko Air Manula. Benchini sura ambazo hazitakosekana
ni pamoja na Muzamiru, HD, Ndemla, Morrison na Kennedy.
Naitazama kama
mechi inayoenda kuwa miongoni mwa mechi bora zaidi msimu huu, kwani timu hizi
ndizo zenye wachezaji wengi zaidi wa kigeni kuiko timu zingine, hivyo uzoefu
wao kuleta ladha inayotarajiwa na mashabiki.
Hofu yangu pekee, ni waamuzi!!!!

Post a Comment