AFISA WA TAKUKURU AKAMATWA KWA RUSHWA YA MILIONI 50
Kwa niaba ya
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa – TAKUKURU Brigedia
Jenerali John Mbungo, napenda kuufahamisha umma kwamba, Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa imekuwa ikiendelea na utekelezaji wa majukumu yake ya
kuzuia na kupambana na rushwa nchini, kama yalivyotamkwa na Sheria ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa Na. 11 ya Mwaka 2007.
Kupitia majukumu
haya, tumekuwa tukiuhabarisha umma juu ya mafanikio mbalimbali yanayotokana na
utekelezaji wa majukumu haya ikiwa ni pamoja na kuwahabarisha juu ya watumishi
wa umma wanaokamatwa kwa tuhuma za kuomba na kupokea rushwa.
Kama mtakavyokumbuka,
wiki iliyopita kupitia ofisi yetu ya TAKUKURU mkoa wa Arusha tumewakamata
Askari Polisi 7 waliodaiwa kudai rushwa ya Shilingi Milioni 200 kutoka kwa
Mfanyabiashara mmoja wa jijini Arusha na kupokea shilingi milioni 100, lakini
pia kupitia ofisi yetu ya TAKUKURU mkoa wa Manyara, tulimkamata Mwendesha
Mashitaka wa Mkoa wa Manyara kwa kosa la kuomba na kupokea Rushwa ya Shilingi
Milioni 5 kutoka kwa watuhumiwa wa makosa ya Jinai.
Ndugu waandishi wa
Habari,
Kupitia taarifa hii
ya leo, tunaujulisha umma kuwa tumemkamata Mtumishi wa Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa - TAKUKURU aitwaye ZAINAB MOHAMED JABIR, kwa kosa la kuomba
na kupokea Rushwa – Kinyume na Kifungu cha 15 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana
na Rushwa Na. 11 ya Mwaka 2007.
Mtumishi huyu aliomba
rushwa kiasi cha shilingi Milioni 50 kutoka kwa mtu mmoja (Jina limehifadhiwa)
kwa madai ya kumsaidia mtu huyo katika tuhuma dhidi yake ambazo zinachunguzwa
na TAKUKURU. Uchunguzi dhidi ya tuhuma hii unaendelea na utakapokamilika hatua
stahiki zitachukuliwa.
Ndugu Waandishi wa
Habari,
Vilevile, kwa niaba
ya Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, napenda kuzungumzia kuhusu uwepo wa tabia ya
baadhi ya watu wanaofanya UTAPELI kwa kujitambulisha kwa vyeo tofauti tofauti
ikiwemo Afisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa - TAKUKURU.
Matapeli hawa
wamekuwa wakipiga simu na kujitambulisha kuwa wao ni Maafisa wa TAKUKURU
wakiwaeleza watu hao kwamba tuhuma zao zipo TAKUKURU na kwamba wanawaita
TAKUKURU kwa ajili ya mahojiano.
TAKUKURU
inawapongeza wale wote walioweza kubaini kuwa watu hawa ni MATAPELI na kutoa
taarifa TAKUKURU mara moja. Hata hivyo, tunaendelea kusisitiza wananchi
kutokubali kutapeliwa na mtu yeyote. Unapopokea simu ya aina hii tafadhali fika
katika ofisi ya TAKUKURU iliyoko karibu nawe kwani TAKUKURU ina ofisi katika
mikoa yote na Wilaya zote Tanzania Bara.
Ndugu Waandishi wa
Habari,
Kwa niaba ya
Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, tunaendelea kuwashukuru wananchi na wadau wengine
wote ambao wamekuwa wakishirikiana nasi katika kufanikisha jukumu hili la
kuzuia na kupambana na rushwa nchini kwa kutuletea taarifa za wale wote
wanaojihusisha na vitendo vya rushwa.
IMETOLEWA NA:
DOREEN J. KAPWANI
AFISA UHUSIANO
KWA NIABA YA
MKURUGENZI MKUU WA TAKUKURU

Post a Comment