KILICHONIPUNGUZIA USHABIKI KWA SIMBA

NCHINI Tanzania, angalau watu wamegawanyika kwa ushabiki wa timu mbili kongwe, Simba na Yanga. Hawa ni wote, akina baba na akina mama, wazee, vijana na hata watoto. Ingawa wapo, japo kwa kiwango kidogo sana, ambao si mashabiki ama wa Simba au wa Yanga.
Ndivyo hata mimi
nilivyokuwa. Niliipenda sana, na bado naishabikia timu hiyo, ingawa si kwa
mapenzi kama yale niliyokuwa nayo siku za nyuma, kabla sijaijua undani wa timu
hizi zinazotoka Kata moja ya Kariakoo, Ilala jijini Dar es Salaam.
Tokea utoto wangu,
nimekuwa ni shabiki wa Simba, yaani ile huniambii kitu. Ilipofungwa, nilikosa
raha sana na kila mmoja angefahamu na iliposhinda, furaha yangu haijawahi kuwa
na kifani. Tangu nilipopata akili, sijawahi kuacha kufuatilia mambo ya Simba.
Nilianza kuijua
timu hii kipindi kile cha mabeki Kihwelu Mussa na Mohamed Kajole hadi
nilipokuja kugundua kitu mwanzoni mwa miaka ile ya 2000.
Moja ya matukio
makubwa kabisa ninayokumbuka kuhusu Simba ni ahadi ya mmoja wa waliowahi kuwa
viongozi wa klabu hiyo miaka ya nyuma, Jabir Shikamkono, aliyeahidi endapo
Simba ingefungwa na Yanga angenyoa nywele zake na kuwa upara.
Ikumbukwe miaka ya
themanini kuelekea tisini, upara haikuwa fasheni kabisa kwa watu wazima.
Lilionekana ni jambo la ajabu kidogo. Ni kweli Simba alipigwa mechi hiyo na
Jabir alinyoa kweli kipara.
Mwaka ambao
nilikosa furaha kabisa kwa sababu ya Simba ni 1987, ambapo timu hii almanusra
ishuke daraja, kama siyo mipango kuinusuru baada ya kuishinda Yanga mechi ya
mwisho. Leo naweza kujua sababu za kwa nini Simba ilishinda mechi ile na kwa
nini Yanga iliuachia ubingwa ili kuinusuru Simba.
Ikumbukwe mwaka huo
Yanga ilikuwa ya moto kwelikweli na Simba mbovu. Kila shabiki wa soka aliamini
Mwananchi anakwenda kuchukua 'ndoo' lakini kilichotokea kinabaki kuwa historia.
Mwaka ambao
nilikuwa na furaha sana moyoni ni 1993, ambao Simba ilifika fainali za Kombe la
Shirikisho wakati huo likiitwa kombe la CAF. Aaah, ilikuwa ni timu ya kibabe sana
ile aisee.
Nakumbuka pia tukio
la mwaka mmoja kabla ya hapo, 1992, Simba ilishinda fainali za michuano ya
Afrika Mashariki na Kati iliyofanyika Zanzibar dhidi ya Yanga. Simba ilishinda
kwa penati. Mechi ile ilichezwa usiku na nakumbuka hadi saa sita usiku nilikuwa
barabarani na mashabiki wa Simba mjini Dodoma tukishangilia ushindi.
Mwaka 2000 mwanzoni
nikaingia katika tasnia ya uandishi wa habari. Kama ambavyo ilikuwa kawaida,
nilianza kwa kuripoti habari za mahakama za mwanzo, baadaye nikaingia kwenye kitengo
cha Michezo.
Huo ndiyo ukawa
mwanzo wa kufahamiana na kuwa na ukaribu na wachezaji, makocha, viongozi wa
klabu, viongozi wa mpira wa wilaya, mikoa hadi Taifa, wafadhili, makomandoo na
wadau hasa wa mpira.
Miaka hiyo ya 2000
kulikuwaga na michuano flani maarufu sana ikijulikana kama Hedex Cup, ambayo
ilikuwa inaratibiwa na kampuni hiyo ya dawa ya kichwa kutoka Kenya. Wakati wa
michuano hiyo, jamaa walikuaga wanamleta mwakilishi wao ambaye anaisimamia na
mara nyingi kama siyo zote, fainali ilizikutanisha Simba na Yanga.
Huyo jamaa wa Kenya
siku nafanya naye mahojiano, nilipomtajia jina langu, akashtuka na kuniuliza
kama mimi ni mtu wa Kenya.
Kwa kuwa alikuwa ni
mtu muhimu kwangu nyakati hizo za shindano, haraka nikamkubalia, nikimwambia
kuwa mimi ni mwenyeji wa Thika na huku nilikuja na wazazi wangu nikiwa mdogo.
Akafurahi sana na kuanzia siku hiyo akawa siyo tu mtu wangu wa karibu, bali
rafiki kabisa.
Nilipata mambo
mengi sana kutoka kwake. Kuna siku alinitaka nimsindikize kwa viongozi wa Simba
akakutane nao. Nilimsindikiza hadi Food World wakati huo, mgahawa uliomilikiwa
na Kassim Dewji ambaye amewahi kuwa kiongozi kwa nafasi mbalimbali, uliokuwa
maeneo ya Posta.
Kwa kawaida,
waandishi wengi walikuwa wakifika mgahawani hapo, kwani kwa vyovyote kama
hutakutana na viongozi wa klabu hiyo, ambao ni chanzo kikuu cha habari za
michezo, basi watakutana na wachezaji wa Simba au hata viongozi wa TFF (FAT)
wakati huo.
Mkenya huyo
alipofika waandishi wakamdaka, lakini akasema kwa wakati huo hakuwa na cha
kuwaambia, labda mpaka kwanza akutane na viongozi wa Simba waliokuwa
wakimsubiri. Akanishika mkono nikapanda naye ngazi hadi kwenye ofisi ya Kassim.
Niliwakuta Kassim
Dewji (ambaye nilifahamiana naye hata kabla sijawa mwandishi), Crecentius
Magori, Evans Aveva na mtu kama Mulamu au Salim 'Try Again', nimemsahau hasa
alikuwa nani.
Hao wote walikuwa
wananifahamu, baada ya kusalimiana na walipotaka kuanza kikao chao, walinitaka
nitoke nje,nilitii lakini yule Mkenya akawazuia, akawaambia anaomba nibaki kama
rafiki yake na siyo kama mwandishi.
Jamaa wakamkazia,
nikatoka nje nimsubiri. Basi baada ya kumaliza mazungumzo yao, akaja tukaondoka
zetu kuendelea na ratiba zingine.
Nikajaribu
kumdodosa ili nipate cha kuandika, akaniambia hana chochote kinachoweza kuwa
habari, lakini ataniambia mambo waliyojadili ambayo alitaka yasitoke kama
habari, nibaki nayo.
Aisee acha kabisa.
Sisi tunakaa tunashabikia, wakati mwingine hadi tunapinga (siku hizi wanasema
kubet), kumbe watu wanacheza mpira mezani. Ili timu hiyo iende hadi fainali,
kila hatua ina kiwango chake cha pesa. Na kama fainali itakutana na Yanga, basi
kiwango pia huongezeka. Ngoma inakuja nani afungwe mechi hiyo?....
Nikaanza kufanya
uchunguzi wangu kimyakimya ili nigundue kama hali huwa ipo hivyo pia upande wa
pili. Nilichogundua ni kwamba kama walivyo wachezaji wa Simba na Yanga,
viongozi hawa pia ni marafiki mno nje ya uwanja.
Wakati flani bwana
mdogo Athuman Idd Chuji aliondoka Simba na Katibu Mkuu wa Simba wakati huo,
Mwina Kaduguda akasema hatacheza tena mpira. Jioni moja nilikuwa na mdau mmoja
wa Simba, siyo kiongozi ila mtoa hela mzuri, akapigiwa simu na kiongozi
mwenzake wa Yanga (alinionyesha jina la mpigaji kabla hajapokea).
Kwa kuwa aliweka
sauti ya juu ili nisikie wanachozungumza nikasikia waziwazi. Yule wa Yanga
alimuuliza mwenzake wa Simba, umemsikia Katibu wenu anasema Chuji hatacheza
mpira? Yule wa Simba akacheka na kumwambia, achana naye, hatacheza mpira anajua
jinsi alivyokuja hapa Simba?
Na kila mtu anajua
Chuji alicheza soka la mafanikio sana Yanga. Nini kilitokea sijajua. Kuanzia
wakati huo, nikapunguza huo ushabiki wa kutupwa. Sijawahi kukosa raha kwa
matokeo yoyote ya Simba tangu wakati huo. Na kama siyo kutumwa kwenda uwanjani
kuripoti mechi, au kwenda kwa ajili ya kupata habari za kuziandika gazetini,
ningekuwa nimeshaacha zamani kufuatilia mpira.
Tangu nilipoacha
kuandika habari za michezo mwaka 2010, sijawahi tena kwenda uwanjani, ingawa
nina uhakika wa kuingia bure.
Kidogo sasa hivi
naanza kupata hamu mpya baada ya kuiona Simba inavyocheza. Kiwango chake
kinakufanya uamini katika uwezo na si mipango. Kama Yanga nayo itajenga kikosi
imara na kuanza kucheza mpira, nitaweza hata kwenda uwanjani siku za usoni.
Ushauri wangu kwa
mashabiki, muwe na ushabiki wa kiasi, wakati mwingine nyinyi mnapigana, wakubwa
wa Simba na Yanga wapo Serena wanakunywa bia!

Post a Comment