JIDE ALIVYONIKAGUA KABLA YA KUKUBALI INTERVIEW
KAZI ya Uandishi wa habari ina mazonge mengi sana, hasa unapojikuta unagusa masilahi ya mtu bila wewe kujua au kwa kutokuwa na namna nyingine ya kufanya ili kuepuka kutomgusa mtu.
Katika hii kazi
nilitengeneza marafiki wengi sana, lakini pia sikukosa maadui. Hata hivyo
maadui walikuwa ni wachache ambao hata hivyo, nao niliwapata baada ya kuwa
marafiki kutokana na kazi hiyo hiyo ya uandishi.
Yaani unajikuta
umempata mtu mkaelewana kwa sababu ya uandishi, lakini baadaye mnatofautiana
tena kutokana na uandishi huo huo.
Msanii wa muziki wa
kizazi kipya, Judith Wambura Mbibo, wengi wakimfahamu kama Lady Jaydee au Jide,
ni mmoja kati ya watu niliofahamiana nao na kujenga ukaribu kutokana na
uandishi, lakini baadae tukatofautiana kabla ya kurejesha tena ukaribu huo.
Nilimfahamu Jide
kipindi kile cha mwanzoni mwa miaka ya 2000, akiwa bado hajachomoza na
kujitofautisha na wasanii wengine wa kike. Kipindi kile alikuwa katika vita
kali ya kumpata mbabe wa wadada, kwani Rehema Chalamila 'Ray C' alikuwa kwenye
chati, Stara Thomas alikuwa ana-shine, Unique Sisters walikuwa hot, hivyo
yaani.
Wakati huo nilikuwa
katika kampuni moja ya habari ambayo magazeti yake yalipendelea zaidi kudili na
watu maarufu na matukio. Kwa watu maarufu, wasanii wa muziki, filamu, komedi
walikuwa ndiyo walengwa wakubwa.
Hii ilinifanya watu
hawa niwafahamu, niwe nao karibu na ndiyo niliofanya nao kazi. Siku moja
nilikutana naye katika ukumbi wa Msasani Club, nyumbani kwa FM Academia akiwa
na Profesa Jay.
Enzi hizo ni
kawaida sana kukutana na wasanii wa muziki wa kizazi kipya katika kumbi za
muziki wa dansi, kwa vile kipindi hicho, FM Academia 'Wazee wa Ngwasuma' na
African Stars 'Twanga Pepeta' walikuwa katika kiwango chao cha juu kabisa cha
ubora.
Nikasalimiana nao
na kuanza kupiga stori. Jide aliniambia kuwa hakuwa akipendezwa na namna
magazeti ya kampuni yetu yanavyomuandika, kwani ni kama yanamuonyesha kwa sura
ambayo si nzuri kwa jamii.
Nilijaribu
kumwelewesha namna ambavyo yeye alipaswa kudili nayo, kwani mara nyingi hakuwa
akitoa ushirikiano kwa waandishi ambao walikuwa wakimtafuta ili kutoa majibu au
ufafanuzi wa mambo kadhaa, kitu ambacho kinapelekea yeye kuona kama hatendewi
haki.
Akaniambia kuanzia
siku hiyo, hatataka tena kuongea na mimi kuhusu mambo ya habari, labda
kusalimiana tu. Mimi na Profesa Jay tukacheka, lakini Komando alikuwa
anamaanisha, mkali kwelikweli. Nikamwambia asijali, lakini atambue kwamba yeye
ni staa na watu kama wao ndiyo walengwa wakubwa wa vyombo vya habari,
nikimtolea mfano wa jinsi Michael Jackson alivyokuwa akiishi kwa kujificha
ficha kwa kuwaogopa paparazi kutokana na ustaa wake.
Na kweli,
akanichunia. Maisha yakaendelea, mimi na yeye hazipandi. Tunakutana lakini
katika maeneo mengine, ikitokea tukawa uso kwa uso, tunasalimiana na ikitokea
vipi, kila mtu anachukua time yake.
Ilikwenda hivyo,
ingawa mimi kwa nyakati tofauti, nimeshawahi kuandika makala kadhaa za kusifia
kazi za Jide, maana kadiri muda ulivyokuwa unakwenda, yeye akachomoza na kuwa
kileleni miongoni mwa wasanii wa kike.
Katika kipindi cha
miaka kumi kuanzia 2000, unagundua kuwa Stara Thomas alififia, Ray C alijiondoa
katika ushindani na wale wadada wa Unique Sisters wakawa wameamua kuachana na
muziki, pale akabakia mkongwe Jide pekee.
Baadaye nikahama
pale kwenye ile kampuni, nikahamia nyingine. Hii ilikuwa ya magazeti pia lakini
haikuwa na mlengo kama ule wa kampuni ya awali. Hata hivyo sikurejea kwa Jide
ili tuendelee kufanya kazi. Tukaendelea hivyo hadi mwaka 2008 hivi nafikiri,
nilipohama tena kampuni nyingine.
Nikiwa hapo, bosi
wangu akaniambia alikuwa anafuatilia sana kazi zangu na kupendezwa na namna
ninavyoandika habari za wasanii. Akanipa orodha ya wasanii ambao alitaka
nifanye nao mahojiano ili niandike makala zao gazetini. Kati ya wasanii hao,
jina la Jaydee lilikuwamo!
Kwa kuwa sikuwa na
namba yake, nikaitafuta na kuipata, nikampigia. Nikamwambia nilihitaji kuonana
naye. Akaniambia hajabadili msimamo wake juu yangu, lakini mimi nikamwambia
ingekuwa ni vyema tukakutana kwanza, asikilize ninachotaka kumwambia halafu
aamue.
Akakubali. Akanipa
muda ambao angekuwepo katika hoteli ya Southern Sun, pale katikati ya jiji.
Ilikuwa jioni flani hivi, mida kama saa mbili usiku nikafika pale tukakutana.
Jide ni msichana
jasiri, mwelewa, mpambanaji na anajielewa. Akaniambia kabla ya chochote,
nimwambie kwanza ninachokitaka kutoka kwake maana hajui hasa nimefuata nini.
Nikamwambia nahitaji kufanya naye mahojiano (Interview), akacheka sana na
kuniuliza kama niko sawasawa.
"Nipo sawa, ni
kwamba mimi kule nimeshahama kitambo sana, hivi sasa nipo kampuni
nyingine," nikamwambia na kumtajia huko nilikohamia.
Akaniambia hana
taarifa za kuhama kwangu na akaniomba kitambulisho ili ajiridhishe. Nikampa,
akakipiga picha na kuniambia kwamba hana matatizo na mimi, isipokuwa yeye alikuwa
na tatizo na pale nilipokuwa nafanyia kazi.
Tukapanga siku ya
interview na hadi ninapokamilisha kukupa kisa hiki, Jide ni mmoja kati ya
wasanii wakongwe ambaye bado tuna mawasiliano mazuri ya kikazi.

Post a Comment