BIFU KUBWA ZAIDI DUNIANI ILIKUWA HII

Unamkumbuka mwanamuziki anayeitwa Keith Sweat? Yule akitamba na wimbo wake mkali ulioitwa Twisted? Kama unamkumbuka, basi utakuwa unafahamu pia kwamba ni wakati huo, mkongwe LL Cool J alikuwa hakamatiki na kibao chake cha Loungin, kama ambavyo kundi la New Edition nalo likitamba na wimbo wao, Hit Me Off.
Kwa mashabiki wa muziki wa nchini Marekani, wanakumbuka pia wakati huo, jinsi R. Kelly alivyokuwa juu na wimbo wake wa I Can't Sleep Baby (If I), huku Toni Braxton naye akiwa kileleni mwa ubora wake na kibao chake cha You're Makin Me High.
Si hao tu, lakini kilikuwa ni kipindi cha wakali wengine wa muziki duniani walioacha alama kama Fugees, The Spice Girls, Aaliyah, OutKast na wengine wengi wa wakati huo.
Lakini wakati mashabiki wa muziki wa wakali hao wakiwa katika kilele cha furaha, saa 11:15, alfajiri ya Septemba 7, mwaka 1996, katika makutano ya barabara za East Flamingo na Kova Lane, jijini Las Vegas, Nevada, gari iliyokuwa ikiendeshwa na Marion 'Suge' Knight ilisimama katika kizuizi cha barabarani baada ya taa nyekundu kuwaka.
Walikuwa njiani kurejea nyumbani,
wakitokea katika ukumbi wa MGM Grand, Las Vegas, kuangalia pambano la ngumi
kati ya mwamba wa enzi hizo, Mike Iron Tyson dhidi ya Bruce Seldon.
Pembeni mwa Suge, alikuwa ameketi rapa mtata, Tupac Shakur.
Ghafla, gari lingine likaja na kusimama
pembeni yao. Mtu mmoja kwenye gari hilo aliyekuwa amekaa siti ya nyuma,
alitokeza dirishani na kurusha risasi nne, zote akimlenga 2Pac. Mbili zilimpata
kifuani, moja mkononi na moja pajani. Suge alipata majeraha madogo mkononi.
Suge alikuwa ndiye bosi wa lebo kubwa ya muziki wakati huo ya Death Row Records huku 2Pac akiwa miongoni mwa wasanii wake nyota. Baada ya siku saba za kuhangaika ili kuokoa maisha yake, hatimaye Septemba 13 mwaka huo, mkali huyo wa kibao cha Dear Mama, aliaga dunia.
Miezi sita baadaye, Christopher Wallace maarufu kama Natorious B.I.G au Biggie Small naye alipigwa risasi katika mazingira kama hayo huko jijini Los Angeles, California.
Machi 7, 1997, Biggie alikuwa amealikwa kumpa tuzo Toni Braxton za Soul Train Music Award na wakati akifanya hivyo, baadhi ya mashabiki walimzomea. Kesho yake kukawa na after party, ambayo ilifanyika katika ukumbi wa Petersen Automotive Museum, ikiandaliwa na jarida la Vibe likishirikiana na QWest Records.
Waalikwa wengine katika tukio hilo
walikuwa ni mkewe, Faith Evans, Aaliyah, P Diddy na wawakilishi wa magenge
pinzani ya Bloods na Southern Crips.
Shughuli ilikuwa kubwa na ilipofika saa sita na nusu usiku, B.I.G aliamua kuondoka ukumbini kurejea hotelini alikofikia baada ya Polisi kuifunga pati hiyo kutokana na watu kujaa kupita kiasi.
Mkali huyo wa East Coast akiwa na wapambe wake, alisimama kwenye kizuizi baada ya taa nyekundu kuwaka katika makutano ya barabara za Wilshire Boulevad na South Fairfax Avenue, umbali wa mita 50 kutoka ukumbini. Mitaa ikiwa imejaa watu waliokuwa wakitoka katika pati hiyo, ghafla gari jeusi likaja na kusimama pembeni ya gari la B.I.G.
Dereva wa gari hilo akashusha vioo, akatoa bastola na kumlenga Natorious, akampiga risasi nne na kukimbia.
Pamoja na ubora wa Polisi wa Marekani,
hadi leo wameshindwa kuwapata wauaji, ingawa inadhaniwa mauaji hayo yalitokana
na uhasama wa makundi ya hip hop ya East Coast na West Coast.
Lebo ya Bad Boy Records chini ya Sean Combs 'Puff Daddy' ndiyo iliyokuwa mhimili wa East Coast wakati wale wa West Coast, waliongozwa na Marion 'Suge' Knights na lebo yake ya Death Row Records. Wawili hawa wote wapo hai.
Baada ya mauaji ya 2Pac, watu
walimhusisha B.I.G, lakini nyota huyo pamoja na familia yake walikataa katakata
kuhusika na sakata hilo, wakidai siku ya mauaji, yeye alikkuwa New York
akirekodi wimbo wake.
Na ili kukabiliana na vitisho, aliajiri
walinzi ambao alikiri wazi kuwa aliwapa kazi kutokana na hofu aliyokuwa nayo
juu ya maisha yake.
Aliyedaiwa
kumpiga risasi Tupac, Orlando Anderson, naye aliuawa kama alivyomuua mwenzake
akiwa kwenye taa za barabarani mwaka 1998.

Post a Comment