WAITARA AAHIDI KUDILI NA WAKANDARASI NA WAFANYAKAZI WABABAISHAJI
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara,
(mbele wa kwanza kulia), akiwa katika picha ya pamoja na menejimenti na wafanyakazi
wa Bodi ya Mfuko wa Barabara (RFB), mara baada ya kumaliza kikao kazi kilichofanyika
Jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, amewaonya wakandarasi na wafanyakazi wababaishaji na wanaoidanganya Serikali kuwa wana sifa na vigezo lakini wanajenga barabara na madaraja chini ya viwango kuacha tabia hiyo mara moja.
Amesema ujenzi wa
miundombinu ya barabara na madaraja chini ya viwango husababisha gharama
kubwa kwa Serikali kutokana na kufanya matengenezo ya barabara mara kwa mara.
Naibu Waziri Mwita
ametoa kauli hiyo jijini Dodoma, katika kikao kazi na menejimenti na
wafanyakazi wa Bodi ya Mfuko wa Barabara na kupokea taarifa ya Bodi hiyo ambapo
pamoja na mambo mengine ameupongeza mfuko huo kwa namna unavyoweza kusimamia
matengenezo ya barabara nchi nzima kwa uharaka unaoendelea kufanywa na Wakala
wa Barabara (TANROADS) pamoja na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini
(TARURA).
Amezungumzia
umuhimu wa wafanyakazi kutoa elimu sahihi kwa Jamii ili kuilinda
miundombinu yote ya Barabara, Madaraja, Reli, Bandari, Vivuko na Viwanja vya
Ndege ili idumu kwa muda mrefu.
"Tutahakikisha
tunachujana humu humu ndani na ukigundua kuwa wewe sio
mwenzetu ujitafakari mapema kabla sijakufikia, tunahitaji watumishi
wazalendo na wakandarasi wenye sifa na weledi sio wababaishaji",
amesisitiza Naibu Waziri huyo.
Waitara amewataka
watendaji kuongeza kasi katika maamuzi hasa pale inapotokea dharura ya madaraja
na barabara kukatika na kusababisha wananchi kukosa huduma mbalimbali za
kijamii.
Aidha, amesisitiza
umuhimu wa watumishi kutumia muda wao wa Serikali vizuri kwa kuleta michango
chanya yenye ubunifu pamoja na kuweka mkazo katika kutatua changamoto za
wananchi kwa haraka na kasi.
Akiwasilisha
taarifa ya utekelezaji wa Bodi hiyo kwa Naibu Waziri huyo, Meneja wa Mfuko wa
Barabara Bw. Eliud Nyauhenga, amesema kuwa mfuko umeweza kufadhili tafiti mbalimbali
zinazofanywa kwenye ujenzi wa gharama nafuu ili kujenga barabara nyingi zaidi
na imara.
Nyauhenga,
ameongeza kuwa Bodi imeendelea kutoa elimu kwenye ngazi zote kuhusu matumizi
bora ya barabara ili kuilinda miundombinu hiyo na kupunguza gharama kubwa za
matengenezo.
Naibu Waziri
Waitara yupo katika ziara ya kikazi katika mikoa ya Dodoma, Dar es Salaam na
Tanga yenye lengo la kujitambulisha, kuzifahamu taasisi zinazosimamiwa na
Wizara yake, kukagua miradi pamoja na kuzungumza na wafanyakazi kuhusu mwelekeo
wa Serikali.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.

Post a Comment