MICHUANO YA KOMBE LA MEI MOSI MAMBO YA NDANI, OCEAN ROAD ZANG'ARA



 

1.    Mchezaji Happy Kabelele (kulia) wa timu ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ameibuka mshindi wa tatu baada ya kumfunga Martha Mwasumbi katika mchezo wa bao wa michuano ya Kombe la Mei Mosi uliofanyika jana kwenye uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza. Semfukwe aliibuka mshindi

  

Na Mwandishi Wetu, Mwanza

WAKATI timu ya Wizara ya Mambo ya Ndani leo iking’ara kwa wanariadha wake kuibuka mabingwa, nayo timu ya Taasisi ya Saratani Ocean Road wametwaa ubingwa wa mchezo wa bao uliofanyika kwenye uwanja wa CCM Kirumba jijini hapa.

Mariam Salim na Fabian Nelson wote wamekuwa wa kwanza baada ya kumaliza mbio za kilometa nane wanawake na kilometa15 wanaume zilizoanzia eneo la Buhile kwa upande wa wanawake na Stendi ya Magu kwa wanaume na zote  ziliishia eneo la Sabasaba.

Ushindi wa pili ulikwenda kwa mchezaji Scolastica Halisi wa Uchukuzi na Winfrida Martin wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) ameshika nafasi ya tatu.

Kwa upande wa mshindi wa pili alikuwa Saing’ati Kisian wa Mamlaka ya Hifadhi ya  Ngorongoro (NCAA); huku Gift Kisaki wa Uchukuzi amemaliza wa tatu.

Wachezaji wengine wa upande wa wanaume walioshiriki kwenye mbio hizo ni Amos Tengu wa Nje, Kispan Nepapai wa NCAA, Kahamba Ngombe wa Kilimo, Magaisha Edward wa Ocean Road, Chogela Mussa wa MWAUWASA, Lusajo Ndaga wa TPDC na Polycarp John wa Tanesco.

Kwa upande wa wanawake ni Furaha Kaboneka wa Ukaguzi, Benedetha Petro wa TPDC, Zuwena Omari wa Taasisi ya Saratani Ocean Road, Bhoke Wambura wa Wizara ya Mambo yaNje, Laya Uledi wa Kilimo na Angela Lugamalila wa Wizara ya Habari.

Katika mchezo wa bao uliokuwa mkali na wa kuvutia mchezaji Ofarasia Muhola wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road alitoana jasho na Mwanahawa Rashid wa Wizara ya Kilimo, ambapo Ofarasia aliibuka bingwa; wakati kwa wanaume Imani  Mwaipaja wa Wizara ya Mambo ya Ndani alitwaa ubingwa kwa kumshinda Hashim Mwembe wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.

Naye Flugence Semfukwe wa Chuo Kikuu cha Tiba na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili (MUHAS), ameshika nafasi ya tatu baada ya kumfunga Yusuph Milanzi wa TPDC; wakati kwa wanawake Happy Kabelele wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kawa wa tatu baada ya kumfunga Martha Mwasumbi wa Wizara ya Mambo ya Ndani.

Michuano hiyo inashirikisha michezo ya netiboli, soka, kuvuta Kamba, bao, karata, draft na baiskeli ambapo inatarajiwa kufikia tamati tarehe 29 April, 2021.

 

 

 

No comments