MICHEZO YA MEI MOSI 2021, UCHUKUZI, TPDC HAKUNA MBABE
Timu ya kuvuta Kamba ya wanaume ya Uchukuzi ikiwavuta wenzao
wa Ukaguzi kwa mivuto 2-0 katika mchezo wa michuano ya Kombe la Mei Mosi uliofanyika
jana kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza
Na Mwandishi Wetu,
Mwanza
TIMU za soka za Uchukuzi
na Shirika la Maendeleo ya Petrol nchini (TPDC), leo zimetoka sare ya bao 1-1
katika mchezo wa soka wa michuano ya Kombe la Mei Mosi uliofanyika kwenye Uwanja
wa CCM Kirumba jijini hapa.
TPDC walikuwa wa
kwanza kupata bao lililofungwa kwa njia ya penati na Barnabas Mwashambwa baada ya
nahodha Dalush Shija kufanyiwa madhambi na Ramadhani Madebe wa Uchukuzi katika eneo
la hatari.
Pamoja na mchezo huo kuwa
mkali, na Uchukuzi kucheza pungufu baada ya Madebe kutolewa kwa kadi nyekundu katika
kipindi cha pili, waliweza kusawazisha kupitia kwa Rahim Ayeshi aliyeunganisha krosi
safi ya Idrisa Bahatisha.
Hata hivyo, bado Uchukuzi
inaongoza kundi B ikiwa na alama nne na magoli nane ya kufunga, huku TPDC wakishika
nafasi ya pili nao wakiwa na alama nne na magoli saba ya kufunga. Timu ya Wizara
ya Kilimo inashika nafasi ya tatu kwa kuwa na alama tatu huku Jiji Mwanza na Wizara
ya Mambo ya Nje zikiwa hazina pointi.
Katika michezo ya
Kamba timu ya wanaume TPDC iliwavuta Kilimo kwa mivuto 2-0; wakati Tanesco wakishindwa
kufurukuta mbele ya Wizara ya Mambo ya Nje kwa mivuto 2-0 na Uchukuzi wakiwavuta
Ukaguzi kwa mivuto 2-0.
Katika michezo ya wanawake
timu ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) waliwaadhibu Mamlaka ya Majisafi
na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) kwa mivuto 2-0; na Taasisi ya Saratani
Ocean Road ilichapwa na Uchukuzi kwa mivuto 2-0.
Michuano hiyo itaendelea
leo katika michezo ya kuvuta Kamba wanaume Uchukuzi watakutana na MWAUWASA;
huku Tanesco watacheza na Kilimo; na NCAA watapepetana na Jiji Mwanza; wakati kwa
wanawake Tanesco itawakaribisha Wizara ya Mambo ya Nje; nayo Kilimo itakutana na
MWAUWASA.
Katika michezo ya soka
timu ya MWAUWASA watawakaribisha Tanesco; huku Wizara ya Mambo ya Nje itacheza na
Jiji Mwanza; wakati katika netiboli timu ya Ikulu itacheza na Kilimo; Jiji
Mwanza watakutana na TPDC na Wizara ya Mambo ya Ndani watacheza
na MWAUWASA.

Post a Comment