DARAJA LA KIYEGEYA MBIONI KUKAMILIKA
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi, Dkt.
Leonard Chamuriho (mwenye tai), akiangalia mihimili mikuu itakayowekwa kwenye daraja
la Kiyegeya, mkoani Morogoro, wakati Waziri huyo alipofika darajani hapo kujionea
maendeleo yake.
Serikali imesema inatarajia kukamilisha ujenzi wa daraja la Kiyegeya, mkoani Morogoro, hivi karibuni, ambalo lilibomoka mwezi Machi, mwaka jana kutokana na mvua kubwa zilizokuwa zikinyesha.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukagua
maendeleo ya ujenzi wa daraja hilo katika mkoa huo, Waziri huyo amesema kuwa ujenzi
huo unatekelezwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), kwa kushirikiana na
Wakandarasi wengine kwa mtindo wa ‘Force Account’.
“Ningependa kuwapongeza TANROADS kwa kazi nzuri walioifanya
tena kwa ufanisi mkubwa, hivyo, tunatarajia baada ya miezi michache daraja hili
litakamilika ili wananchi waweze kulitumia tena, mapema iwezekanavyo”, amesema Chamuriho.
Aidha, Chamuriho amesema kuwa ametembelea sehemu wanayotengeneza
mihimili mikuu ya daraja hilo na kufafanua
kuwa katika miezi michache ijayo kazi ya kuinyanyua na kuiweka juu mihimili
hiyo itafanyika, na baada ya hapo utafuata ujenzi wa barabara za maungio mbili ambapo
moja itakuwa na mita 1000 na nyingine mita 800, upande wa Dodoma na upande wa Morogoro.
Ameongeza kuwa ujenzi wa daraja hilo lililopokatika
barabara ya Morogoro- Dodoma ni muhimu, kwani ndio njia pekee inayounganisha mkoa
wa Dar es Salaam, Morogoro na mikoa ya Kaskazini ya kati na hata kuelekea nchi za
jirani za Rwanda, Burundi na Uganda.
Ametoa rai kwa Mameneja wa TANROADS katika mikoa yote
nchini kuhakikisha wanaendelea kukagua madaraja yote ikiwemo kingo zake, pamoja
na kukagua mito yote inayoelekea kwenye madaraja hayo na kuisafisha ili kudhibiti
matatizo ya kukatika kwa madaraja.
Kwa upande wake, Meneja wa TANROADS, mkoa wa Morogoro,
Mhandisi, Kolante Ntije, amesema kuwa ujenzi unaendelea vizuri na mpaka sasa umefika
asilimia 58.
“Kama alivyosema Mheshimiwa Waziri, wakati wowote tunatarajia
kuweka mihimili hapa juu, na niwahahakishie watumiaji wa barabara hii kuwa hatutachukua
muda mrefu kuikamilisha kazi hii”, amesema Mhandisi Ntije.
Daraja hilo ambalo lilibomoka mwezi Machi, mwaka jana
na kuleta msukosuko mkubwa na hivyo kupelekea Serikali kujenga
daraja la muda pembeni yake, linajengwa upya na Serikali, ambapo ujenzi wake
unagharimu shilingi Bilioni 6.9.
Imetolewa
na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Post a Comment