DARAJA JIPYA LA WAMI KUKAMILIKA SEPTEMBA MWAKA HUU
Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Mkoa wa Pwani,
Mhandisi Yudas Msangi, amesema Daraja jipya la Wami lenye urefu wa mita 510 na barabara
unganishi zenye urefu wa kilometa 3.8 linalounganisha miji ya Chalinze– Pwani na
Segera– Tanga litakamilika mwezi Septemba mwaka huu.
Mhandisi Msangi amemueleza Naibu Waziri wa Ujenzi na
Uchukuzi, Mwita Waitara, mkoani Pwani wakati alipokagua maendeleo ya ujenzi huo
uliofikia asilimia 50.5 na kumuahidi kuwa kazi itakamilika kama ilivyopangwa.
Akizungumza mara baada ya ukaguzi huo, Naibu Waziri Waitara amesema ujenzi wa Daraja jipya la Wami
ni mkakati wa Serikali katika kuongeza ufanisi katika barabara ya Chalinze-
Segera na kupunguza adha kwa abiria na wasafirishaji wanaotumia daraja la
zamani lenye urefu wa mita 88.75.
“Kutokana na umuhimu wa daraja hili Serikali imeamua
kujenga daraja jipya ili kuondoa adha katika daraja la zamani lililojengwa mwaka
1959 kutokana na kutokidhi mahitaji ya magari yanayopita kwa sasa, kuwa jembamba
na lenye njia moja na barabara zake unganishi kupita katika miinuko mikali na kona
mbaya na hivyo kusababisha ajali za mara kwa mara”, amesema Naibu Waziri huyo.
Naibu Waziri Waitara, amemtaka Mkandarasi Power
Construction Corporation ya China, Msimamzi wa mradi Intercontinetal
Consultants and Tecnocrtrats Pvtya India
kwa kushirikiana na Apex Engineering Co. ya Tanzania na Meneja wa
TANROADS Mkoa kuongeza vifaa na wafanyakazi ili kazi ikamilike kama ilivyopangwa
na kusisitiza kwamba Serikali itaendelea kumlipa mkandarasi kwa wakati.
Aidha amewataka wafanyakazi wanaojenga daraja hilo kufanyakazi
kwa uzalendo, bidii na kujifunza ili kuwezesha Taifa kuwa na wataalam wake wa madaraja
makubwa siku zijazo.
“Zaidi ya wafanyakazi 280 kati ya 300 wanaojenga daraja
hilo ni watanzania, hivyo hakikisheni wingi wenu mnautumia kubaki na ujuzi na kufanya
kazi kwa uzalendo”, amesisitiza Naibu Waziri Waitara.
Zaidi ya shilingi bilioni 67 zinatarajiwa kutumika katika
ujenzi wa Daraja jipya la Wami lenye urefu wa mita 510 na upana wa mita 11.85 ambalo
limezingatia sehemu ya barabara za magari, watembea kwa miguu na vizuizi kwa ajili
ya usalama hivyo linatarajiwa kupunguza ajali katika eneo la Mto Wami na kuhuisha
huduma za usafiri na uchukuzi katika barabara kuu ya Chalinze – Segera.
Naibu Waziri Waitara yupo katika ziara ya siku nne katika mikoa ya Dodoma, Dar es Salaam, Tanga na Pwani kukagua miundombinu na kuzungumza na wafanyakazi wa taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo.
Imetolewa
na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.

Post a Comment