CHAMURIHO AAGIZA UWANJA WA NDEGE SONGWE KUKAMILIKA SEPTEMBA

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi, Dkt. Leonard Chamuriho, amemuagiza Mkandarasi GECI Espanola S.A wa Spain anayesimika taa katika uwanja wa ndege wa Songwe, kuhakikisha anakamilisha zoezi hilo ifikapo mwezi wa Tisa mwaka huu, ili kuruhusu ndege kuweza kutua usiku.
Aidha, Waziri Chamuriho ameagiza pia, ujenzi wa njia
ya kuruka na kutua ndege unaotekelezwa na Mkandarasi M/s China Geo Engineering
Corporation katika uwanja huo, nao kukamilika ifikapo mwezi wa Saba mwaka huu.
Akizungumza mara baada ya kukagua maendeleo ya mradi
huo, Waziri Chamuriho amebaini kuwa Makandarasi hao wana uwezo wa kukamilisha kazi
zilizobaki katika miezi hiyo ili sasa wananchi wa mkoa huo na mikoa jirani kuweza
kufurahia huduma za usafiri wa anga mchana na usiku kama wengine.
“Mara baada ya kukagua uwanja huu, nimebaini kuwa Makandarasi
hawa wana uwezo wa kukamilisha kazi hizi mapema, maana vifaa vyote muhimu vinavyotakiwa
kwa ajili ya kazi vimesha wasili isipokuwa mashine ya kukwangua lami ambayo inatarajiwa
kuwasili mwezi Mei”, amesema Chamuriho.
Chamuriho, amefafanua kuwa adhabu za kimkataba zitatolewa
kwa Makandarasi hawa endapo wakishindwa kukamilisha kaz ihizo kwa muda walioahidi.
Katika hatua nyingine, Waziri Chamuriho amekagua mradi
wa ujenzi wa Barabara ya Chunya- Makongolosi kwa kiwango cha lami (Km 39), ambapo
amesema kuwa mradi huo umefika asilimia 87 na kumtaka Mkandarasi China Railway
15th Group kukamilisha ujenzi huo mwezi wa Saba mwaka huu kama alivyoahidi.
Amempongeza Mkandarasi huyo kwa kujenga zahanati yenye
jengo la mama na mwana pamoja na jengo la upasuaji ambayo aliahidi kwa aliyekuwa
Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt. John
Pombe Magufuli, wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi la barabara hiyo mwezi Mei
2019, ili kurudisha huduma kwa jamii.
Kwa upande wake, Msimamizi wa mradi wa ujenzi wa Uwanja
wa ndege wa Songwe, Mhandisi, Abdallah Mziray, amesema kuwa mradi huo ambao unagharimu
shiling iBilioni 14.7 unaendelea vizuri kwani tayari Mkandarasi amekamilisha kazi
ya ujenzi wa maeneo ya usalama mwanzo na mwisho wa uwanja (RESA), na kwa sasa anaendelea na matayarisho ya uwekaji
wa tabaka la lami.
“Kazi zinaendelea vizuri, ujenzi wa RESA
umekamilika, na kwa sasa Mkandarasi ameanza matayarisho kwa ajili ya kusimika taa
za kumuongoza rubani wakati wa kutua”, amefafanua Mziray.
Naye, Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania
(TANROADS), Mkoa wa Mbeya, Mhandisi Peter Mkolwa, amesema kuwa mradi wa ujenzi wa
barabara ya Chunya – Makongolosi (Km 39), unaenda sambamba na ujenzi wa zahanati
ambapo amebainisha kuwa ujenzi wa barabara hiyo umefika asilimia 87 na Zahanati
umefika asilimia 60.
Waziri Chamuriho, amekamilisha ziara ya kikazi ya siku
mbili mkoani Mbeya ambapo alikagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na Wizara yake
ili kujionea maendeleo yake ikiwemo mradi wa ujenzi wa Uwanja wa ndege wa Songwe
na barabara ya Chunya – Makongolosi (Km 39) kwa kiwango cha lami.
Imetolewa
naKitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Post a Comment