_PETER TOSH ALIUAWA NA ALIYEKUWA AKIMSAIDIA

 

 

Bunny Wailer amnyooshea kidole mjane wa Bob Marley, Rita Marley.

Ulikuwa ni usiku wa joto jingi katika mji wa Kingston nchini Jamaica. Usiku ambao haukukomaa saana tangu jua lizame. Usiku wa ijumaa ya tarehe 11 Septemba, 1987. Ambapo gwiji wa muziki reggae duniani, Peter Tosh, damu yake ilipomwagwa kinyama nyumbani kwake. Na kwa hakika walifanikiwa kuufumba "mdomo mkubwa! Hatimaye wakapumua, walimaliza kazi. Ndiyo, Peter Tosh aliuawa usiku huo, akimfuata mwenzake, Bob Marley.

Ni siku ambayo, punde tu, alikuwa nyumbani kwake akipumzika baada ya safari ya kutoka Marekani katika ziara yake ya kimuziki. Na wakati huo ndani ya nyumba yake alikuwa na mkewe Marlene Brown - mke mwingine mdogo aliyekuwa anaishi naye kwa kipindi hicho. Pia walikuwemo watu wengine watano, 'memba' wa bendi yake na wengine waliokuja kumsalimu mara baada ya ziara. Na watano hao, ni Wilton 'Doc' Brown, Michael Robison, Jeff 'Free I' Dixon ambaye alikuwa Dj wa mtaani pamoja na mkewe Joy Dixon, pia alikuwepo Carlton 'Santa' Davis; mpiga "drum" matata katika bendi ya Peter Tosh. Wote walikuwemo nyumbani kwake usiku huo.

Haikupita kitambo sana, Peter Tosh alisikia kama kuna jambo nje. Kama vile mtu anagonga mlango. "Mikey, nenda kaangalie getini", Tosh alimwambia mmoja kati ya watu waliokuwemo ndani humo. Hakujua ulikuwa ni usiku wa mwisho kwake. Usiku ambao muziki wa reggae uliuawa.

Punde tu, mara Michael alipofungua geti, watu watatu wenye bunduki waliingia ndani. "Tulieni! Na hili linatokea kwa sababu yako wewe", alisema mmoja kati ya wauaji hao watatu akimuoneshea mke wa Tosh, Marlene Brown. Anaikumbuka sana siku hiyo Carlton 'Santa' Daivis, mmoja kati ya manusura aliyekuwa anatoa ushuhuda huu hivi karibuni. Na wakati huo wa tukio yeye alikuwa bado hajaonwa na wauaji hawa, kwa kuwa likuwa ameketi katikati ya mapazia yaliyokuwa yamemziba asionekane vizuri.

Na nyuma yake, 'Santa', kulikuwa na mlango wa kioo, hakudhani kama wamemuona. Alimgundua mmoja kati ya wauaji hao, Leppo Lobban, mtu aliyekuwa ameachiwa kutoka jela mwaka mmoja tu upite, na ambaye alikuwa akipewa msaada na Peter Tosh sanjari na kutafutiwa kazi mara baada ya kutoka jela. Walikuwa hawajavaa vinyago, na hawakujali hata kama wangejulikana. Lakini haikuchukua muda, walimuona 'Santa' aliyekuwa amezibwa na mapazia. "we rasta, lala chini!", alisema mmoja kati ya wauaji akimwambia 'Santa'. Wakati huo, wote walikuwa wamelala chini. Wamelalia matumbo na sura zikitazama kiupandae - yaani zimelalia sikio.

Hapo ndipo Leppo alipoanza kumuuliza Peter Tosh kwamba ameweka wapi pesa. Tosh alisistiza kwamba hakuwa na pesa yoyote ndani kwa wakati huo, labda angekwenda Benki siku ya jumatatu. "Nitakwenda Benki jumatatu". Walimpiga na kitako cha bunduki tena na tena. 'Santa' aliyekuwa amelala pembezoni mwa Tosh, alimsikia Tosh kwa namna alivyokuwa akigugumia kwa maumivu makali. "kwa kweli inaumiza, sikuwa na uwezo wa kufanya lolote kumuokoa kaka yangu", alisema 'Santa'.

Baada ya kipigo kizito kwa Tosh, na wakati huo hana pesa, mmoja wao alisikika akisema, "unakufa usiku huu". Kulikuwa kimya kidogo. Na kwa mara ya kwanza mtu mgumu na jasiri, Tosh alionekana kuogopa, alijua kifo kimefika, ila hakuwa na namna. Baada ya sekunde kadhaa risasi zilipigwa. Ni Peter Tosh, alikiwa amelala sakafuni kimya na rasta zake ndefu, risasi zimefumua nyuma ya kichwa chake. Walifuatia wengine na wao wakamiminiwa risasi.

'Santa' alikuwa wa mwisho, alijua ni zamu yake imefika. Alipgwa risasi sehemu ya bega upande wa kushoto. Baada ya muda kukawa kimya. Akasikia kwa nje mlio wa gari iliyowashwa na kutokomea.

'Santa' alikuwa anapumua kwa shida wakati huo, alimwambia Marlene aliyekuwa pia hajiwezi, kuwa pumzi ina mbana. Alikimbilia haraka haraka na kwenda kwenye gari lake aina ya "Jeep". Aliiwasha ambapo upande mmoja tu, wa kulia wa mwili wake ndio uliokuwa na uzima, na mwingine ukifa ganzi. Aliendesha hadi hospitali ya chuo cha West Indies. Baada ya dakika kumi alikuwa akipiga honi kwa nguvu nje ya geti. Alipokuja kuchukuliwa na kukimbizwa chumba cha dharura, alipoteza fahamu kwa muda.

Baada ya kuzinduka, upande mmoja alikuwa Jeff 'Free I' Dixon akiunguruma kwa taabu, na upande mwingine alikuwa Peter Tosh ambaye madaktari walimzigira wakihaha huku na kule. Hapa ndipo 'Santa' aliposikia daktari mmoja akisema, "Nina mashaka kuwa bwana Tosh ametutoka". Licha ya kuwa hajiwezi, kauli hiyo ilimuumiza sana 'Santa'.

Peter Tosh alikuwa amefariki, katika umri wa miaka 42. Jeff 'Free I', Dj wa mtaa, alifariki kwa majeraha mabaya. Wilton 'Doc' Brown pia alifariki. Wengine wakasalimika roho zao, ila wakiwa na majeraha makubwa.

Baada ya polisi kuwahoji waliosalimika, walimtaja Leppo Lobban. Baadaye alikamatwa na kufunguliwa mashitaka. Naada ya hukumu iliyochukua dakika 11 tu, alihukumiwa kunyongwa hadi kufa, lakini baadaye adhabu ikatenguliwa na kuwa ya kifungo cha maisha. Leppo ambaye amekuwa akikanusha hadi sasa kuwa hausiki na mauaji hayo. Na kwamba usiku wa tukio alikuwa katika kioski akipata kinywaji na ndipo aliposikia tukio hilo la kuuawa kwa Tosh kupitia kwa watu.

Dennis 'Leppo' Loban, mtukutu aliyetumia maisha yake kwa kiasi kikubwa akiwa jela. Hata baada ya kutoka tu, Octoba 1986, mwaka uliofuata, Septemba 1987, akaondoa uhai wa Peter Tosh, mtu ambaye alijitolea kumsaidia kwa kila hali kwa sababu alimfahamu, na wamekuwa wote mitaa ya Trench Town. Na sasa ndio huyu aliyerudi kuuondoa uhai wa Tosh. Kweli Tosh aliwahi kuimba katika wimbo wake mmoja unaoitwa "Maga dog" akisema "Sorry fi maga dog. Him turn around bite you". Akiwa na maana ambayo si ya moja kwa moja, kwamba unaweza kuumpa chakula mbwa mwenye njaa na aliyekonda ili anawili, lakini baadaye akageuka na kuuma mkono uleule unaompea chakula. Na ndivyo alivyofanya Leppo Lobban kwa Peter Tosh.

'Santa', anamnyooshea kidole mke wa Peter Tosh, Marlene Brown kwamba ndio chanzo cha Tosh kuuawa. Kwamba siku chache kabla ya tukio. Marlene alikwaruzana na Leppo, alimtukana na kumwita Leppo jina ambalo ni matusi kwa Jamaica, "batty man", kwa maana ya mtu anayeshiriki mapenzi ya jinsia moja. Leppo alilaani na kusema Tosh ameshindwa kumchunga mkewe aliyemtawala, hiyo yeye atamfundisha.

Kuna baadhi ya vyanzo vinadai kuwa, aliyekuwa mwanakundi wa "The Wailers", Bunny Wailer, amemshutumu mke wa Bob Marley, Rita Marley kuhusika na mauaji ya Peter Tosh akimtumia Leppo Lobban. Pia Bunny Wailer akinukuliwa na vyanzo hivyo, anaenda mbali na kudai pia Rita ndiye aliyepanga mauaji ya mumewe, Bob Marley kwa kumpa vumbi la mlipuko wa nyuklia(Radioactive Ash) alilopewa na aliyekuwa mmiliki na 'prodyuza' wa lebo ya "Island Record", Christopher Blackwell ambaye Bob Marley alikuwa chini yake. Au kwa kuwa Bunny Wailer na Rita Marley wanaugomvi wa muda mrefu? Hatujui. Lakini ukweli unabaki kuwa Peter Tosh alitakiwa afe tu. Kwanini?

'Mdomo mkubwa' na msimamo ulimuua Tosh. Leppo alikuwa ni kama 'kisu' tu. Lakini kuna mkono ulioshika 'kisu' hiki, ndio ulioangamiza maisha ya gwiji huyu wa reggae duniani. Kujua kwanini Peter Tosh aliuawa, ni lazima kujua falsafa ya maisha yake kwa ujumla.

_*Naam,*_ Peter Tosh alizaliwa mnamo tarehe 19 Octoba, 1944 mji wa Westmoreland Jamaica. Alizaliwa kwa jina la Winston Hubert McIntosh. Alizaliwa kutoka kwa wazazi wawili waliokuwa watu wa kanisa. Baba yake, James McIntosh aliyekuwa mchungaji wa kanisa katika mtaa wa Savanna-la-Mar, ambako alikutana na mama yake Peter Tosh, Alvera ambaye alikuwa muumini wa kanisa hilo.

Kwa nyakati hizo za makuzi ya udogoni akitumia jina la ubatizo la Winston Hubert McIntosh, hakupata bahati ya kulelewa na wazazi wake. Hasa kwa baba yake ambaye alikuwa na watoto wengi, hivyo na kuwasahau wengine. Maisha yake kwa kiasi kikubwa amelelewa na Shangazi yake. Lakini, tunaweza kisema, amejilea mwenyewe.

Amekuwa ni mtu wa kujitegemea sana tangu akiwa mdogo. Aliwahi kuulizwa kama shangazi yake ndiye aliyemkuza na kama alikuwa na mchango wa kufanya maisha yake yawe kama yalivyokuwa. "Hapana. Hapana. Unajua, nilikuwa na miaka mitatu kwa umri, lakini ni kama nilikuwa na miaka hamsini kifikra"

Akiwa katika umri wa mdogo kabisa, alianza kujifunza kupiga gitaa. Hasa ni baada ya kupita mtaani na kumuona mtu aliyekuwa analicharaza. Tosh alivutiwa sana. Alisogea na kumtazama kwa karibu mtu huyo, ambaye aliamua kumfundisha kwa muda mfupi. Baadaye alipopata la kwake, alifanya mazoezi na kuwa mpigaji hodari wa gitaa. Kutokana na ubishi, udadisi na ung'ang'anizi wa kutaka kujua jambo, ndivyo vilivyomsaidia baadaye ukubwani kujua kupiga karibia ala nyingi za muziki na kuwa mwalimu mzuri wa Bob Marley katika gitaa mara walipokutana.

Baada ya kuishi katika mji wa Savanna-la-mar kwa zaidi ya muongo mmoja, Tosh na shangazi yake mwaka 1956 walihamia mtaa wa Denham, Kingston. Ambapo miaka mitatu mbele, Tosh akiwa na miaka 15, shangazi yake alifariki na kumuacha na mjomba wake. Ambapo ni kama alikuwa anajilea mwenyewe.

Ni katika mji huo mkuu wa Jamaica, Kingston, katika mitaa ya Trench Town, ndipo Peter Tosh alipokutana na rafiki zake wawili ambao walikuja kuweka alama katika duniani katika uwanda wa muziki. Alikutana na Robert Nesta Marley au Bob Marley, na Neville O'Reilly Livingstone maarufu kwa Bunny Wailer. Na ni wakati huo Peter Tosh alikwisha badili jina kutoka Winston Hubert McIntosh, na kuitwa Peter Tosh rasmi. Winston alipewa baada ya waziri mkuu wa Uingereza. Hivyo akalichukua Peter jina ambalo aliwahi kuitwa wakati wa utoto na Tosh kutoka kwenye McIntosh. Yote hii ni kukana fikra za kitumwa.

Hiyo vijana hawa watatu, mwaka 1962 wakajiunda kwa ajili ya muziki chini ya mshauri au wao aliyeitwa Joe Higgs. Na kati ya mwaka 1964 wakaanzisha kundi lao la muziki na kuliita "The Wailing" au "The Wailers". Kwa mujibu wa Peter Tosh, yeye ndiye alikuwa "figure" wa kuanzisha kundi hilo, kwa kuwa ni yeye tu ndiye aliyekuwa anaweza kupiga ala za muziki, na ndiye aliyemfundisha Bob Marley mupiga gitaa.

Baada ya kujisuka, Joe Higgs aliwapeleka kwa kwa mzalishaji(prodicer) wa muziki na mmiliki wa lebo ya "Studio One", bwana Clement 'Coxsone' Dodd. Aliwapeleka kufanya majaribio ili Dodd awatazamie. Walifanya vizuri. Siku nyingine walirudi studio hapo kurekodi kibao chao cha kwanza kabisa kilichoenda kwa jina la "Simmer Down" kibao ambacho kilishika nafasi za juu katika chati za muziki nchini Jamaica. Kutoka hapo sasa "The wailers" wakaanza kuonesha makali na kusimama.

Katika kila jambo hakukosekani changamoto, Tosh anakumbuka namna walivyokuwa wanapewa paundi tatu kwa wiki na Dodd licha ya kibao chao kitikisa vilivyo katika chati za muziki Jamaica.

Mwaka 1970 wakahamia kwa 'prodyuza' maarufu kuliko wote Jamaica, mwenye mkono wa kazi kweli kweli, Lee 'Scratch' Perry. Wakiwa chini ya Perry, walitoa albamu tatu chini ya lebo ya Trojan, lakini yasemekana hawakulipwa kitu. Na zaidi katika wakati wa kujifua(rehearsal) vipande vya Tosh vilirekodiwa kwa siri na kuachiwa baadaye nchini Uingereza kwa jina la "Peter Touch"

Baada ya tanga tanga nyingi na tapeliwa, hatimaye mwaka 1972 walitua mikononi mwa 'prodyuza' ambaye sasa aliwaweka katika ramani ya muziki wa reggae kimataifa na kubadili maisha yao. Christopher Blackwell, 'prodyuza' ambaye hakuwa na jina sana kwa wakati huo na lebo yake ya "Island Records". Hivyo kuwasaini "The Wailers" ilikuwa ni faida kwa pande zote(win wini situation) - "The Wailers" waliinuka; na Chris Blackwell akawa "mogul" katika uwanda wa muziki.

Chini ya "Island Records" walianza na albamu yao ya kwanza ilikwenda kwa jina la "Catch A Fire" ambayo ilibeba nyimbo 9 ndani yake na kuachiwa tarehe 13 Aprili, 1973. Na miongoni mwa nyimbo hizo, nyimbo mbili ndizo ambazo Tosh alikuwa kama muimbaji mkuu - nyimbo kama vile "400 Years" na "Stop That Train". Pia katika albamu hii, kuna wimbo pendwa sana wa "Stir It Up".

Haikuchukua muda sana baada ya kuona mafanikio ya albamu ya "Catch A Fire" chini ya Chris Blackwell, miezi sita tu, walifutia na albamu waliyoiita "Burnin", iliyoachiwa tarehe 19 Octoba, 1973 ikiwa ni mwendelezo wa albamu ya "Catch A Fire". "Burnin" ilikuwa na nyimbo 10, pamoja na nyimbo za ziada(bonus tracks) 3, hivyo kuwa na nyimbo 13. Na ndani ya "Burnin" kulikuwa na wimbo uliotamba sana ulimwenguni, "Get Up, Stand Up", ukiwa kama wimbo wa kimataifa juu ya masuala ya haki, ukiwa wimbo maalumu kwa kwa shirika la haki "Amnesty International", na Peter Tosh akiwa kama muimbaji mkuu wa wimbo huu.

Kosa la kusambaratika kwa kundi hili, lilianzia taratibu katika albamu ya "Burnin". Chris Blackwell alianza kumtengeneza taratibu Bob Marley na kumfanya kuwa kichwa cha kundi. Katika albamu hii, muimbaji mkuu kama si kwa asilimia kubwa ni Bob Marley, huku Peter Tosh na Bunny Waler wakiwa kama waitikiaji(back vocals) jambo ambalo Tosh na Bunny hawakulifurahia sana.

Mwaka 1974, kundi la "The Wailers" likavunjika rasmi. Ni kwamba Chris Blackwell alikuwa anambania Tosh na Bunny kutoa kazi zao binafsi chini ya lebo hiyo kama "solo artist". Haikuwa rahisi kwa mtu mwenye msimamo kama Peter Tosh kushikiwa uwezo wake na mtu. Aliona Blackwell amewasaliti mkubwa na mtu mbaya. Tosh kuanzia hapo akaamua kubadili jina la Blackwell na kumuita 'Whiteworst'. Kwa mfano, WCB watoe album kwa pamoja na jina la kundi ni WCB, lakini album ikitoka, jina linaonekana "Diamond na Wasafi Classic Band". Ndivyo ilivyokuwa kwa "The Wailers", katika album ya "Catch A Fire", jina linaonekana "Bob Marley and The Wailers", badala ya "The Wailers".

Zaidi, Tosh alimuona rafiki yake Bob Marley ni msaliti mkubwa baada ya kuendelea kutumia jina la "The Wailers" wakati kundi walilo anzisha pamoja limevunjika. "Tulipoondoka kama 'The Wailers', Bob Marley akajichukulia watu wengine na kujiita 'The Wailers', alisema Tosh.

Ndiyo, kundi likavunjika na kila mtu akaendelea kivyake. Lakini baadhi ya watu wanadai kuwa, Chris Blackwell aliona ni bora abakie na Bob Marley si kwamba alikuwa na uwezo kuliko Tosh, kwa kuwa, kwanza; ni mchanganyiko wa rangi mbili - mweusi na mzungu(chotara) - kwamba akitoa kazi zitakubalika pande zote. Pili; Peter Tosh na Bunny Wailer walikuwa na misimamo ya kiharakati zaidi kuliko Bob na kwamba nyimbo zao zisingepokelewa vyema na upande wa tabaka tawa au watu weupe kipindi hicho, na zingeharibu soko. Hii ni mitazamo ya baadhi ya watu tu.

Naam, sasa safari ya Peter Tosh kama mwanamuziki wa kujitegemea(solo musician) ikaanza. Akijiamini katika uwezo wake, ambapo baadaye alijipa jina la "Stepping Razor", kwamba yeye ni hatari kama wembe mkali - kwa uwezo wake. Baadaye alipoulizwa kuhusu kutengana na rafiki yake Bob Marley na matarajio ya kazi zake, ".....Ninaendelea na kazi zangu, wala sitafuata mtindo wa mtu. Bob anatumia aina yake ya uimbaji kufikisha ujumbe, pia nitaendelea na yangu".

Tosh aliibuka na albamu yake ya kwanza Juni 1976 chini ya "Columbia Records" akiwa sasa kama mwanamuziki binafsi. Album hii inayoitwa "Legalize It", imebeba nyimbo kumi ukiwemo wimbo pendwa wa "Brand New Second Hand". "Legalize It", Tosh alihamasisha serikali ya Jamaica kuhalalisha matumizi ya mmea wa bangi kama dawa, na kukomesha ukatili wa polisi juu watumiaji wa mmea huu. Tosh aliamini bangi ni zaidi ya dawa, mmea ambao madaktari, wabunge, wahandisi, wanajeshi na wengine wengi waliutumia Jamaica, lakini serikali ilipambana na watu wa hali za chini. Serikali ya Jamaica ilianza kumuona Tosh kama tishio, na hivyo kuufungia wimbo wake wa "Legalize It" alioutoa mwaka 1975. Tosh aliamini uvutaji wa bangi ndio uliompa mawazo mapana na kufanya mambo makubwa. Na katika kila, onesho lake, jukwaani mara kadhaa alivuta bangi. Mawazo ya Tosh juu kuhalalisha bangi sasa yanatimia katika nchi zilezile zilizotumia propaganda kupinga mmea huu, ndizo hizihizi zinazohalalisha wananchi wake watumie.

"Kila mmoja analilia amani, ndiyo. Hakuna anaye lia juu ya haki". Ni kweli, huwezi kupata amani pasipo kuwa na haki. Marehemu Mchungaji Mtikila aliwahi kusema: "Amani ni tunda la haki". Basi Tosh aliyaimba haya katika wimbo ulioitwa "Equal Rights" na ambao ulibeba jina la albamu yake ya pili ya "Equal Rights" iliyotoka mwaka 1977 chini ya Rolling Stones Records.

Peter Tosh, huenda safari yake ya kifo ilianzia hapa. Tarehe 22 Aprili, 1978 kulikuwa na tamasha kubwa lambalo lilikiwa na watu zaidi ya 40,000 kwa ajili ya amani ya Jamaica. Tamasha ambalo lilikuwa na lengo la kuwapatanisha viongozi wa kisiasa waliokuwa wanahasimiana na kusababisha uhalifu, maisha magumu na hali ya uslama kuzorota - Waziri mkuu wakati huo, Michael Manley wa chama cha "People's National Party", na Edward Seaga kutoka chama cha upinzani cha "Labour Party" na aliyekuwa anaungwa mkono na Marekani. Basi katika tamasha hilo, walikuwepo wanamuziki wakubwa wa Jamaica. Peter Tosh na Bob Marley waliongea siku hiyo. Bob Marley aliwashikanisha mikono viongozi hao na vyombo vya habari vikimulika tukio hilo kwa mbwembwe. Lakini ilipofika zamu ya Tosh, hewa ilichafuka, alitoa hotuba kali iliyowanyooshea kidole moja kwa moja viongozi hao.

*_"Nina furaha kwamba waziri mkuu upo hapa na kiongozi wa upinzani. Hatuwezi kuwafanya wezi wadogo waje hapa na kuiba rasilimali zetu. Kwa kuwa wamekuwa wakifanya hivi kwa muda mrefu katika hali ya machafuko. Mimi siyo mwanasiasa, lakini madhara yake ninayapata". Hakika lilikuwa ni dongo kwa viongozi hao. Tosh akaonya, "Watu walio na hasira, ni wale wenye njaa"._*

Ni kuanzia hapo, nyimbo zake zikaanza kufinywa Jamaica na usalama wake ukawa hatarini, japo iliishi katika misimamo yake ile ile ya kusema kweli na kutetea wasio na sauti. Meizi michache mbele, alipigwa vibaya sana na polisi karibia ya kifo kwa sababu walimkuta na bangi. Alipasuliwa fuvu na kuvunjwa mkono aliokuwa anajikinga usoni. Kwa mujibu wake, hakuna kiungo kilichokuwa kinafanya kazi, zaidi ya macho tu, na akili. Alikiona kifo usoni. Alikotwa na mlevi tu, akakibizwa hospitali.

Ni mwaka huu aliopata kipigo, alitoa albamu yake ya tatu iliyoitwa "Bush Doctor" akimshirikisha Mick Jagger katika wimbo wa "Don't Look Back". Tosh alikuwa mtu kweli. Aliwashutumu Rolling Stones Record kwa kuto mtangaza vema kama inavyotakiwa kulingana na uwezo wake. Tosh alijiamini kwa uwezo wake, na ndio maana akajiita "Stepping Razor".

Mwaka 1979, alikataa ofa ya kufanya onesho Israel kwa kupinga ukandamizaji wake kwa wapalestina. Na mwaka huohuo, kwa kuwa alikuwa ni mtu aliyepinga sana masula ya nyuklia hivyo alipata nafasi ya kutangazwa zaidi kwa kutokea ndani ya kipande cha filamu kilichopinga masuala ya nyuklia akiwa na Bruce Springsteen katika uwanja wa Madison Square Garden, New York. Na siku hiyo Tosh alipanda jukwaani akiwa amevaa mavazi ya kipalestina huku akivuta bangi yake.

Si hivyo tu, Tosh alikataa tena ofa ya kufanya onesho nchini Afrika Kusini mwaka 1983, na badala yake akaenda kufanya onesho nchi ya jirani ya Swaziland(Eswatini), Disemba 1983 ambako alibebwa juu juu kwa kwa furaha na mashabiki. Hii yote Tosh alifanya kupinga waziwazi sera za kibaguzi(apertheid policy) za Afrika kusini wakati huo chini ya serikali ya kikaburu. Tosh hakuwa mbinafsi, angeweza kwenda kuzichukua pesa hizo na kuacha ndungu zake wakiangamia.

Zaidi, alitoa katika albamu ya "Equal Rights" ya mwaka 1977, ndani yake kuna wimbo unaitwa "Apartheid", ameimba kukemea mfumo huo. Na wakati huo Afrika Kusini iliungwa mkono na nchi za magharibi pamoja na Marekani, lakini Tosh aliweza kupaza sauti yake juu ya mfumo huo wa kibaguzi. Jaribu kufikiria, alikataa onesho Israel, alikataa onesho Afrika Kusini, na akaenda mbali kukemea mfumo wa kibaguzi, je, mtu huyu anayepambana na mfumo anakuwaje salama. Hakika Tosh alikuwa na mshipa.

"Wanted Dread and Alive", ikiwa ni album yake ya mwisho chini ya lebo ya "Rolling Stones Records" mwaka 1981, ilibebaba nyimbo 9. Miongoni mwa nyimbo zilizofanya sana vema sana katika albamu hii, ni "Rastafari Is", "Reggae Mylitis", na "Oh Bumbo klaat".

Alijivunia kuwa mtu mweusi, na alipenda watu weusi watambue asili yao kwamba ni Afrika, hata azaliwe sehemu nyingine. Katika wimbo wake wa "African" anasisitiza kuwa haijalishi utaifa, lakini akiwa mweusi tu, basi asili yake ni Afrika. Pia alikuwa mstari wa mbele kupigiania uhuru wa nchi za Afrika. Katika albamu yake ya "Mama Africa" iliyotoka mwaka 1983 ikiwa na nyimbo 9 chini ya lebo ya EMI, kuna wimbo unaoitwa "Not Gonna Give Up", akiwa na maana ya hakuna kukata tamaa hadi nchi zote za Afrika ziwe huru. Mtu huyu alikuwa mmajumui(Pan Africanist) halisi. Hakiaka alikuwa.

Kutokana na ubishi wake katika kuamini uwezo wake, aliweza kupiga karibia ala zote za muziki. Mpiga gitaa aliyemfunza Bob Marley kupiga gitaa. Mara nyingine alipenda kutumia gitaa lenye umbo la bundiki aina ya M16 alilopewa zawadi jijini Los Angeles na msanii wa mtaani, Bruno Canoon mwaka 1983. Yeye mwenyewe alidai kwa anatumia gitaa hilo pamoja na muziki wake wa reggae kama silaha ya kupambana na udhalimu.

Tosh alikuwa mtundu wa lugha. Alitengeneza lugha zake mwenyewe kwa kuzibadili na zikaleta maana. Kwa mfano siku moja akiwa Grenada, alikaribishwa na Bishop, Maurice aliyesema "Salaam, komredi. Karibu Granada Granada('Greetings, comred. Welcome to Granada')". Tosh alijibu, "sijageuka kuwa mwekundu, bado ni mweusi('I don't come red[comred]. I man come black". Pia Tosh amedalili baadhi ya maneno, kama vile alivyokuwa anamwita 'produzya'wao wa zamani baada ya kuvurugana, badala ya Chris Blackwell, alimwita Chris 'Whiteworst'.

Kwa lugha yake, alimwita Malkia Elizabeth(Queen Elizabeth) kwa jina la "Queen 'Ere Lies a Bitch'". Pia kuna vyeo alivipa majina yake. Kama meneja(Manager), alimwita "Dameger", na Jaji(Judge) alimwita "grudge", na wanasiasa(poticians) aliwaita "crime minister who 'shits'in the 'House of Represent-a-t'iefs'"

Mwaka anaouawa, 1987, alitoa albamu yake ya mwisho kwa jina la "No Nuclear War". Ambapo mwaka 1988, baada ya kufariki, ilichukua tuzo ya "Grammy" kama albamu bora ya reggae ya mwaka. Ni katika albamu hii, Tosh amepinga matumizi ya silaha za nyuklia, na kupinga ubaguzi wa makaburu Afrika Kusini, katika nyimbo za "No Nuclear War" na "Fight Apartheid".

Na hii ndiyo ilikuwa falsafa yake, ambayo watu waliifananisha na ile ya Malcolm X katika kidai haki. Hakupenda kuimba nyimbo za kuhamasisha upendo kama Bob Marley wakati wengine wanakandamizwa. Falsafa yake ilitofautiana na ya Bob Marley aliyefananishwa na Martin Luther King Jr, ya kudai haki kwa kuhimiza upendo na mshikamano.

Tosh hakuwahi kuwa mnafiki, aliongea kile kilichopo katika fikra zake. Aliwahi kuulizwa kama kifo cha cha Bob Marley atakuwa amepoteza kitu. "Hapana, hakuna nilichopoteza. Kama mke wangu akifa, hakuna nitakachopoteza. Hivyo, hata kaka yangu alivyofariki, hakuna nilichopoteza. Sijali kuhusu hilo". Kuna wakati pia aliwahi kuulizwa kama atamkuta Bob Marley peponi badala yake alijibu kuwa amekwisha kuwepo huko mara kadhaa.

Peter Tosh, mwembamba na mrefu wa futi 6 na inci 4. Alikuwa hajibu kwanza kabla hajafikiria. Kwa matendo yake, alikuwa kama mtume aliyetumwa kupitia muziki wa reggae kufikisha ujumbe. Alikuwa mtu wa watu ambaye hakuwahi kuwa mbinafsi. Mtu aliyewafanya Lucky Dube na Senzo kuanza kuimba muziki wa reggae.

Lakini huyu Peter Tosh, alikuwa mtu wa kuuawa(a man who must be killed) kwa aliyoyasimamia na kuyafanya. Ndiyo mawazo ya wakubwa yalivyokuwa yanawaza. Hakika mawazo yake hayakupendwa na mfumo ouvu aliouita "Babylon System". Alikuwa zaidi ya mwanajeshi aliyepigana vita kwa kutumia silaha za moto. Alitumia kalamu na maiki kupandikiza fikra za kimageuzi kwa watu waliokandamizwa hususani watu weusi na Afrika kwa ujumla. Alipigana kipindi kigumu, kipindi ambacho wanaharakati wengi waliuawa. Tosh aliipigania Afrika kuliko mwanamiziki yeyote wa ulimwengu huu kupata kutokea. Hadi aliamua kutoa albamu na kuiita jina la "Mama Afrika", hakujali kama wazungu walioshikilia mfumo kwamba wataitangaza ama kuinunua, alijali utu. Alikuwa mmajumui(Pan Africanst) kweli kweli kuliko hata waafrika wenyewe. Kabla ya kuuawa, alikuwa na ndoto ya kujenga shule kwao Jamaica ili watoto wasome. Kifo kilichokuwa kinamnyemelea, hatimaye kikamchukua akiwa na umri wa miaka 42 tu kabla ya ndoto yake kutimia.

Hadi sasa, wakubwa wa Jamaica wanaonekana kutompenda Peter Tosh zaidi ya Bob Marley, wala nyimbo zake hawazipendi. Ni msumari wa moto unaochoma kidondani.

Dennis Leppo Lobban, mtu aliyetumika kama kama kisu, alimuua. Je, ni nani aliyekuwa nyuma yake? Basi kwa kazi za Tosh na maisha yake kwa ujumla, muuaji umekwisha mtambua fikrani mwako.

Peter Tosh ameacha mke na watoto sita wengine wakiwa wanamuziki wa reggae kama baba yao. Wanajitahidi kulitangaza jina la baba yao, na wananuia kufungua jumba la makumbusho kwa ajili ya baba yao.

#Sky_videos_production_tz

#Mr_camera_man

Jah bless!


No comments