Mkurugenzi Kasulu awaongoza wadau kuwafariji wanafunzi wenye uhitaji maalum
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kasulu Mkoani Kigoma, Vumilia Simbeye, leo Jumamosi April 13, 2024,amewaongoza wadau kuwafariji wanafunzi wenye uhitaji maalum katika hafla iliyofanyika katika shule ya msingi Mwenge iliyopo Kata ya Kumsenga.
Katika hafla hiyo iliyoandaliwa na Wadau wa wanafunzi wenye uhitaji maalum Mkoa wa Kigoma, unaojumuisha Maafisa Elimu wa Shule za Msingi na Sekondari, maafisa elimu maalum wa kila halmashauri za mkoa huo na waalimu wenye mapenzi mema na wanafunzi hao, zawadi mbalimbali zilitolewa.
Wanafunzi hao wenye uhitaji maalum unawajumuisha wenye changamoto ya akili, viungo, usikivu na kuona.
Mkurugenzi Simbeye aliiambia Ojuku Blog kuwa alifurahishwa na utashi wa wadau hao waliomualika kuwa mgeni rasmi, kwani licha ya kushiriki pamoja nao katika tukio hilo aliloliita la kihistoria, lakini pia alifarijika kwa uwepo wa maafisa elimu maalum wa halmashauri zote, sambamba na Mwenyekiti wa Maafisa elimu Maalum wa Halmashauri zote nchini, Issa Kambi.
Wanafunzi hao walipewa zawadi mbalimbali ikiwemo mchele, mafuta ya kula, sabuni, biskuti, pipi, juisi na sare za shule.
Aidha, Mkurugenzi huyo alisema alifurahishwa pia na mwalimu mmoja mwenye ulemavu kutoka Halmashauri ya Kasulu DC, ambaye aliwawakilisha walimu wenznake wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu ambao kwa pamoja waliahidi kutoa mashati 20 kwa wanafunzi hao.
Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na wazazi, walezi, Kamati ya shule na wananchi wengine.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Simbeye alisema aliombwa, kama kiongozi wa Halmashauri, kusaidia kutatua changamoto ya njia za watoto wanaotumia viti maalum (Wheelchair) kwani njia hizo siyo rafiki.
Kujibu maombi yao, alisema amepokea na kwamba atawashirikisha wadau wengine walio ndani ya Halmashauri ili kuona namna ya kumaliza changamoto hiyo.

Post a Comment