MBINGA MJI KINARA MBIO ZA MWENGE
Na Alex Nelson Malanga
Mbinga. Halmashauri ya Mji wa Mbinga imeibuka kinara katika mashindano ya mbio za Mwenge wa Uhuru 2023 katika mkoa wa Ruvuma baada ya kuwabwaga washindani wake saba.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Mhe. Kanali Abbas Ahmed Abbas alisema mapema wiki hii kuwa Mbinga Mji iliibuka kidedea katika mashindano hayo baada ya kupata alama 82.98.
Waliopoteza kwa Mbinga Mji ni Manispaa ya Songea iliyopata alama 80.06, Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru (77.96), Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo (77.82) na Halmashauri ya Wilaya ya Madaba (74.93).
Wengine ni Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga (73.57), Halmashauri ya Wilaya ya Songea (71.86) na Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa (71).
Katika ngazi ya Taifa, mkoa wa Ruvuma ulishika nafasi ya 10 baada ya kupata alama 76.27, kwa mujibu wa Mhe. Kanali Abbas aliyekuwa anazungumza wakati wa kikao cha maandalizi ya Mbio za Mwenge.
Mwaka huu mkoa wa Ruvuma unatarajia kupokea Mwenge wa Uhuru Juni 8 kutoka Mkoa wa Mtwara na kuukimbiza katika Halmashauri zake zote nane kabla ya kuukabidhi kwa Mkoa wa Njombe Juni 16.
“Tunapaswa kujiandaa kimkakati ili tufanye vizuri zaidi mwaka huu,” alisema wakati wa kikao kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Manispaa ya Songea.
Aliongeza: “Tunapaswa kufanya kila linalowezekana tuingie katika tatu bora mwaka huu.”
Ofisi ya Waziri mkuu imeandaa vigezo 10 vitakavyozingatiwa na vimeandaliwa kwa kuzingatia ujumbe wa mbio za Mwenge wa Uhuru na mahitaji ya serikali katika kipindi hiki.
Vigezo hivyo vyenye jumla ya maksi 100 ni pamoja na ufanisi wa usimamiaji wa miradi ya maendeleo (maksi 32), ufanisi katika mapokezi ya Mwenge (maksi 6), uzingatiaji wa itifaki za mwenge (maksi 8) na umahiri katika uandishi, usomaji na uwasilishaji wa risala ya utii kwa Mheshimiwa Rais (maksi 8).
Vigezo vingine ni uraghibishaji wa falsafa ya mwenge kwa mwananchi (maksi 4), uwezeshaji wa vijana (maksi 20), uwezeshaji wa makundi yenye mahitaji maalumu na ukatili wa kijinsia (maksi 4) na juhudi zinazochukuliwa katika mapambano dhidi ya VVU/Ukimwi, dawa za kulevya na Malaria (maksi 3).

Post a Comment