Gadner Gabriel Habash ameonyesha utu unavyolipa

 

Hapa ni ndani ya hema lililotengenezwa rasmi kwa ajili ya wadau kuuaga mwili wa aliyekuwa mtangazaji nyota wa kituo cha redio cha Clouds, Gadner G Habash, Leaders Club Dar es Salaam.

Na Ojuku Abraham

Saa tano na dakika chache hivi, Jumatatu ya tarehe 22 April 2024 naingia katika viwanja vya Leaders Club, Kinondoni jijini Dar es Salaam, nikiwa na rafiki yangu wa miaka mingi, Henry Mdimu, maarufu kama Zee la Nyeti. Huyu ni mmoja kati ya waandishi nguli, bobevu na mwenye maono makubwa.

Wote tumekwenda kwa ajili ya kumuaga rafiki yetu, Gadner G Habash, mtangazaji wa muda mrefu wa kituo cha Clouds Media Group. Kati yetu, kila mmoja alifahamiana naye kwa namna yake na wakajenga urafiki kivyao, lakini kikubwa ni kwamba wote tumetoka tasnia moja, tukikutana katika matukio mbalimbali ya kihabari.

Leaders ya leo siyo ya jana. Miundombinu siyo rafiki na ukichanganya na mvua hizi, kuna madimbwi mengi ya maji na nyasi ndefu. Inaonyesha haiko bize kama enzi zile za shangwe kila wikiendi, mechi za maveterani asubuhi, inafuata supu na bia hadi jioni Twanga Pepeta walipokuwa wakija kuimaliza siku kwa shoo kali.

Mvua inanyesha kidogo kidogo, kwa hiyo watu siyo wengi. Ndani ya mahema mawili, watu wachache wanaonekana, huku kwenye vibanda viwili vitatu vilivyojengwa kwa ajili ya watu kusaini vitabu vya maombolezo, nako kuna watu wachache pia. Mvua hazionyeshi kupungua, kadiri muda unavyokwenda, nayo inaongezeka.

Picha ya Gadner G Habash, siku chache kabla ya kufikwa na mauti akiwa studio

Ilipofika saa sita mchana, kiasi cha dakika kama thelathini baada ya kuwasili, idadi ya watu inaongezeka sambamba na mvua. Askari wa usalama barabarani ambao waliwekwa katika viwanja hivyo, wako bize kuelekeza magari wapi sehemu ya kuegesha na wapi panapaswa kuwa njia.

Ni wakati pia ambako juu ya jukwaa, watangazaji wenza wa Gadner, wanaendelea kutoa jumbe mbalimbali kuhusu taratibu za jinsi ratiba ya kuaga itakavyokwenda. Ninawaona nyota wa muziki wa Bongo Fleva, waigizaji wa Bongo Muvi, muziki wa dansi, waandishi wa habari, wanasiasa na wengine wa kada mbalimbali.

Gadner aliishi na hawa watu wote vizuri. Kila mmoja ameenda kwa kumbukumbu zake. Ni siku nyingi sijamuona Ferooz, yule mwamba kutoka kundi la Daz Nundaz, aliyetamba na kibao cha Kamanda. Ninawaona pia wale 'pacha' Mandojo na Domokaya, Joh Makini, Madee, Mheshimiwa Temba, Chegge, Soggy Doggy, H. Baba, Banana Zorro, Nikki wa Pili na wengine kadhaa.

Wapo wanasiasa Henri James Mkuu wa Wilaya ya Iringa, aliyekuwa kabla yake, Richard Kasesera, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda,  Mwenyekiti wa CCM Wilaya Kinondoni, Mbunge viti maalum Keisha, Naibu Waziri wa Sanaa, Utamaduni na Michezo, Mwana FA, Katibu Mkuu Wizara ya Habari na Teknolojia ya Habari, Gerson Msigwa, Kaimu Mkurugenzi wa Michezo, Ally Mayai na wengine kadhaa.

Wanamuziki wa muziki wa dansi pia walikuwa wengi, ukiachana na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari, wakiongozwa na mkongwe Tido Mhando, CEO wa Azam Media.

Hao ni pamoja na wadau wa kila aina waliokuwepo. Yes, Gadner alistahili umati huo ambao kila wakati ulivyokuwa unaongezeka kiasi kwamba wakati mwili wake ulipowasili kiasi cha saa saba na nusu hivi mchana, tayari mahema mawili yalikuwa yameshajaa na viunga vya nje navyo watu walikuwa pomoni.

Gadner, licha ya umaarufu wake, hakuna mtu wa nyodo. Ninamfahamu vyema. Tuliwahi kuwa karibu sana, tukionana karibu kila siku, wakati akiwa Meneja wa aliyekuwa mkewe, Lady Jaydee. Nilihitaji kupata habari za msanii huyo mkubwa mara kwa mara na mtoa taarifa alikuwa ni Gadner. 

Nimeshiriki matukio kadhaa yanayowahusu kama wanandoa, nikifika hadi nyumbani kwao, Temboni Kimara Dar es Salaam. Mimi ni miongoni mwa watu walioumia sana wawili hao walipoachana. Nikakosa upande, nikabakia kuwa mwaminifu, nisiyepeleka habari za huku kuzipeleka kule.

Ni yeye, ndiye aliyenithibitishia kuachana kwao, baada ya kuibuka kwa habari za wawili hao kuachana, wakati huo Jide akiwa Marekani. Mwanzoni alinificha akidai haelewi lolote kuhusu yanayosemwa na watu, lakini baadaye aliamua kuniambia ukweli na nadhani mimi nilikuwa mtu wa kwanza kuripoti ukweli wa kuvunjika kwa ndoa yao.

Urafiki wetu uliendelea, tukikutana kwenye matukio yaliyohusiana na habari. Tulikuwa wote kwenye 'academy' ya Tuzo za Kili Music Award mara kadhaa. Gadner ni mcheshi, muungwana na asiye na kinyongo.

Wakati fulani yeye akiwa Meneja, Jide alipishana na bosi wake Gadner, Ruge Mutahaba (RIP). Niliwahi kumuuliza anafanyaje kazi na mtu ambaye hana uhusiano mzuri na mkewe. Jibu lake lilikuwa rahisi kuliko nilivyofikiria. 'Ojuku, mimi nipo kazini, Clouds na kwa Jide'.

Gari lililobeba mwili wa mtangazaji huyo mahiri likiwasili katika eneo la Leaders Club

Alifafanua. Hawezi kuchanganya mambo. Akiwa kazini kwake Clouds hawezi kushindana na bosi wake na wakati huohuo, akiwa meneja wa mkewe, hawezi kuchanganya mambo ya mapenzi na kazi.

Katika nyakati zote ambazo nimekuwa naye karibu, sikuwahi kumuona akikasirika. Muda wote alibakia akicheka na utani mwingi. Na ucheshi na utani huu, hakufanya kwa mimi peke yangu, hakufanya kwa wasanii peke yake, alifanya hivyo kwa kila mtu aliyekutana naye. Hakuweza kuufanya ustaa wake kuweka ukuta kati yake na wenzake. 

Kama ulikuwa haumfahamu, ukimkuta sehemu kwenye watu zaidi ya wawili, isingekuwa rahisi kumtambua kwa sababu hakuishi kistaa. Alikua anaweza kuzungumza mazungumzo ya aina zote, siasa, michezo, burudani, uchumi, ujasiriamali. 

Na usifikiri alikuwa bishoo. Alizijua stori za kihuni na kisela na aliweza kuzungumza lugha zao. Mkianza kuzungumza kimtaani, naye anaingiza stori, simulizi zinaendelea. Na hii ndiyo siri kubwa ya kwa nini Gadner alikuwa rafiki wa kila mtu.  

   

No comments