Wenye akili wanatushangaa sana
Na Ojuku Abraham
Yes, Taifa linaadhimisha miaka mitatu ya uongozi
wa Madame President, Samia Suluhu Hassan ambaye alichukua nafasi kikatiba,
kufuatia kifo cha hayati John Pombe Magufuli. Rais wa kwanza mwanamke Tanzania,
wa kwanza Afrika Mashariki na miongoni mwa wanawake tisa tu kuwahi kuongoza
serikali barani Afrika.
Kwa nafasi yake, anastahili pongezi nyingi kwa
namna ambavyo amefanya tofauti na mawazo ya wengi hapo awali ambao kwa miaka mingi,
mfume dume umetufanya tuamini kuwa wanawake si watu wa kuwapa kazi nzito
wakazifanya ipasavyo. Amethibitisha, kwa kiwango kikubwa, kwamba anaweza
kuliongoza taifa letu kuelekea kwenye matarajio.
Yapo mambo ambayo ameshindwa kuyapatia uvumbuzi
wa moja kwa moja, ama kwa sababu ya muda, au kwa sababu zilizo nje ya uwezo
wake kama kiongozi wa kitaifa. Kushindwa kwake, hakuwezi, kwa namna yoyote
kuchukuliwa kuwa ni kwa jinsia yake, bali ameshindwa kama ambavyo Mwalimu
Julius Nyerere, Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa, Jakaya Kikwete na JPM
walishindwa.
Yes, Mwalimu alishindwa kuikomesha rushwa, akajitahidi
kwa kiwango cha kuridhisha kudhibiti ubadhilifu, alimudu, angalau kukazia
uwajibikaji miongoni mwa watumishi wa umma na hakuna shaka kabisa kuwa aliishi
falsafa yake ya Ujamaa na Kujitegemea kwani aliwezesha ujenzi wa viwanda vingi
vilivyotumia malighafi za ndani.
Kila kiongozi aliyeingia, kuna mambo aliweza na
yapo yaliyomshinda, kwa hiyo, leo akitokea mtu akisema Madame President
ameshindwa kufanya hili, asionekane msaliti au hana adabu. Bali iwe ni
changamoto tu ambayo tukiibeba kwa mlengo chanya, itatusaidia kufika
tunakoenda.
Katika maadhimisho haya ya miaka mitatu ya mama
madarakani, kuna mengi yanasemwa juu yake. Bahati mbaya sana, mengi
yanayozungumzwa kufanywa naye, ni yale mazuri tu. Kila kiongozi, wa kila kada,
akipata nafasi ya kuzungumza kuhusu miaka hii mitatu, ni kutaja yale mema tu,
kana kwamba hakuna mambo ambayo hayakwenda vizuri, kitu ambacho siyo kweli.
Tumejenga utamaduni wa kuwaona wasema kweli kuwa
ni maadui. Utamaduni huu unaligharimu sana Taifa na kuwanufaisha watu wachache
wanaojificha katika kusifu. Pamoja na mazuri yote yaliyofanywa na Rais Samia
Suluhu Hassan, lakini bado kuna changamoto nyingi zinazowakabili wananchi wa
hali ya chini.
Bado kuna baadhi ya wateule wa Rais Samia
wanawadhulumu wananchi wa chini kwa kutumia ofisi za umma. Kuna malalamiko
mengi ya wananchi juu ya kunyimwa haki zao na watu wenye fedha ambao
wanasaidiwa na wateule hawa wa kiongozi mkuu wa nchi, kwa vile tu wanafaidika
na dhuluma hizi.
Bado kuna upigaji mkubwa wa fedha za umma katika
nyanja mbalimbali. Maofisa wakubwa wana wakandarasi wao, wanawapa tenda,
wanafanya kazi ndogo kwa malipo makubwa. Kuna dhuluma kubwa inafanywa na wenye
viwanda kwa wafanyakazi kwa kulipwa kiwango kidogo cha mishahara na wanakaa
muda mrefu wakitumika kama vibarua.
Bado viongozi wengi, wakiwemo mawaziri, manaibu
wao, makatibu wakuu, wakurugenzi wa idara mbalimbali za serikali, wanaishi kama
malaika ili hali wananchi wanahangaika kupata huduma bora za afya, elimu na
fursa za kiuchumi zilizo sawa.
Ni kweli, majengo mengi ya shule na zahanati
yanajengwa kila kukicha. Lakini je, nguvu kazi ipo? Watumishi wa sekta za elimu
na afya, wanalipwa vizuri kiasi cha kuwapa motisha?
Viongozi wanapiga kelele kutaka vijana
wajiajiri. Oke, sawa pengine vyuo vya ufundi vimeboreshwa kwa maana ya vifaa
vya ufundishaji, lakini je, nchi imeandaa mazingira rafiki ya vijana kujiajiri?
Kijana kujiajiri siyo tu kwa sababu ameshapata maarifa chuoni, je kuna mikakati
ya makusudi ya kumkopesha, kumuendeleza na kumlinda ili asimame?
Serikali inasema elimu inatolewa bure. Bure hii
ni nini? Kule kijijini kwetu wazazi wanatakiwa kupeleka chakula shuleni na hili
ni jambo la lazima. Wanachangia majengo ya shule, wanatumia nguvu kazi
kuyajenga (wanafyatua matofali, wanashiriki ujenzi, wanachangishwa fedha,
lakini ukija Mwenge wa Uhuru, wanatoa takwimu zinazoonyesha majengo hayo
yamejengwa kwa mabilioni ya shilingi bila michango na nguvu kazi za wananchi
kuainishwa). Kuna michango isiyo na idadi inayobuniwa na walimu. Mbele ya
kamera tunasema tunapata elimu bore, lakini ukweli halisi ni kuwa hakuna cha
bure.
Haya ni machache, lakini kuna mengi ambayo
hayaendi sawa huku mitaani, ambayo hatutaki kumwambia mama ili ayafahamu.
Tumebaki kutafuta namna ya kumfurahisha hadi tunamkera, kiasi cha yeye kukataa.
Alianza kuwakataa watu wanaojiita chawa. Wakaanzisha vikundi, ambavyo juzi pia
kavikataa. Yeye hana vikundi, ni mama wa wote.
Kuna mtindo mbaya ambao unaanza kuwa utamaduni
wetu, unakera sana. Ni jambo la ajabu kwamba hata wale tunaoamini ni wasomi,
nao wanaingia kwenye mtego huu. KUMTAJA RAIS SAMIA HATA ASIPOSTAHILI!
Unashangaa msiba umetokea mtaani. Ni kawaida kwa
watanzania kupeana pole na kushiriki shughuli bila kujali hadhi wala jina.
Lakini mathalan, kwa kuwa kuna diwani, mbunge au waziri ameungana nanyi, kwa
heshima anapewa nafasi ya kuongea chochote.
Pamoja na kutoa pole kwa wafiwa kama ilivyo
utaratibu, atatafuta kila ‘engo’ ili mradi tu amtaje Rais Samia Suluhu Hassan.
Jamani, kitu gani hiki? Haya, tupo kwenye sherehe au tafrija za kibinafsi, kwa
mfano za kidini au kielimu (mahafali). Mtu katumia gharama zake, amewakaribisha
ndugu, jamaa na marafiki!!
Anatokea mtu anatafuta nafasi ya kumtaja Rais
bila sababu zozote. Hili jambo, pengine hatufahamu, lakini linatuondolea sana
heshima mbele ya jamii kwa sababu watu wanazungumza.
Ni kawaida sasa, hawezi kusimama kiongozi ye
yote wa kisiasa, kuanzia mjumbe wa shina, mwenyekiti wa kitongoji/kijiji,
diwani, mbunge au Waziri, atasimama na kuzungumza bila kumtaja Rais Samia. Sawa
ni kiongozi wetu, lakini mbona kuna wakati tunamtaja bila sababu?
Huko nyuma, ukiachana na yale Mabilioni ya
Kikwete yaliyoliwa na wajanja, ulikuwa huwezi kusikia eti Rais Mwinyi, Mkapa au
Kikwete ametoa mabilioni ya shilingi kujenga zahanati, shule, barabara,
maabara, soko au ofisi za umma.
Ilifahamika kwamba fedha hizi ni za serikali.
Lakini leo hii, waziri kabisa ambaye huku tunaambiwa ni msomi, anasimama mbele
ya hadhara na kusema anamshukuru rais kwa kutoa mabilioni ya fedha kwa ajili ya
ujenzi wa hiki au kile. Kwa nini shukurani hizi zisiende kwa serikali ambayo
kiuhalisia ndiyo yenye fedha?
Tunamtaka rais wetu ajue, hawa wanampamba ili
kuficha ubadhilifu wao, kuficha matumizi yao mabaya ya ofisi za umma, kuficha
ushiriki wao katika kuwadhulumu wananchi haki zao ikiwemo mashamba/nyumba, kusaka
teuzi na vyeo. Vyema akajua kuwa katikati ya kupambwa kwake, watu wanaugulia
sana maumivu kutoka kwa baadhi ya wateule wake!

Post a Comment