UJENZI NA UBORESHAJI KIWANJA CHA NDEGE CHA TABORA KUKAMILIKA OKTOBA, 2024
Waziri wa Ujenzi,
Innocent Bashungwa ameihakikishia Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuwa
Serikali itahakikisha inasimamia ukarabati na uboreshaji wa Kiwanja cha Ndege
cha Tabora ili kukamilika ifikapo mwezi Oktoba, 2024.
Bashungwa ameyasema
hayo Machi 13, 2024 mkoani Tabora katika ziara ya Kamati hiyo ya kukagua
maendeleo ya mradi huo na kusisitiza Wizara kupitia Wakala ya Barabara
(TANROADS), itahakikisha inamsimamia Mkandarasi wa kampuni ya Beijing
Construction Engineering Group (BCEG), kufanya kazi usiku na mchana ili
kukamilisha kazi hiyo kwa ubora.
"Mheshimiwa
Mwenyekiti na Wajumbe wa Kamati, niwadhihirishie kuwa kutokana na baadhi ya
changamoto zilizojitokeza katika mradi, tutamsimamia Mkandarasi ili atukabidhi
mradi mwezi Oktoba mwaka huu", amesema Bashungwa.
Aidha, Bashungwa ameeleza kuwa moja ya sababu ya miradi kuchelewa ni kutokana na Taasisi za Serikali kutoshirikiana kwa karibu katika maandalizi na utekelezaji wa mradi na amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi kushiriana na Makatibu wakuu wengine katika uratibu wa utekelezaji wa miradi.
Kwa upande wake,
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Selemani Kakoso (Mb)
amemuagiza Waziri Bashungwa kuhakikisha anamsimamia Mkandarasi anayejenga na
kukarabati Kiwanja cha Ndege cha Tabora kufanya kazi kwa ufanisi na ndani ya
muda uliopangwa.
Kadhalika, Kakoso
amemtaka Bashungwa kufuatilia upatikanaji wa fedha za utekelezaji wa miradi kwa
wakati ili kuwawezesha Wakandarasi wanaotekeleza miradi nchini kupokea malipo
yao kwa wakati yatakayofanikisha ukamilishaji wa miradi kulingana na mikataba.
Naye, Kaimu Mtendaji
Mkuu wa TANROADS, Eng. Doroth Mtenga
ameeleza kuwa ujenzi na ukarabati wa Kiwanja hicho umefikia asilimia 38
na unahusisha ujenzi wa jengo la abiria lenye uwezo wa kuhudumia abiria 120 kwa
wakati mmoja, ofisi mbalimbali, sehemu za biashara, ujenzi wa mnara wa kuongoza
ndege na ujenzi wa barabara wa kuingia na kutoka kiwanjani.
Imetolewa na Kitengo cha
Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi.

Post a Comment