Familia yabomolewa nyumba kibabe, kesi ilikuwa mahakamani, OCD amlinda, Mwenyekiti wa Mtaa amkana, Tibaijuka atajwa

 


Charles Forodha (kulia) akiwa na mwanawe Joyce Forodha (katikati) na mkewe Rose Forodha

MKAZI mmoja wa mtaa wa Kihonzile, Bunju B wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam, Charles Forodha amevunjiwa nyumba yake mchana kweupe na mtu ambaye inadaiwa ni tajiri yake, aliyemzawadia kiwanja miaka kumi iliyopita.

Forodha aliiambia Ojuku Blog kuwa kwa zaidi ya miaka 20, alifanya kazi kama mlinzi wa eneo (shamba) la tajiri yake aliyemtaja kwa jina la Diana Alex Tibaijuka na mwaka 2014, alimkatia eneo pembeni la shamba lake, akimwambia kuwa ni zawadi kwa mtoto wake (Forodha) aitwaye Joyce, aliyekuwa na umri wa miaka nane wakati huo.

“Alisema ananikatia kiwanja hicho ili nijenge nyumba, niipangishe ili kodi yake iweze kumsomesha mwanangu. Alisema kiwanja hicho ni cha mtoto wangu lakini kwa kuwa alikuwa na umri mdogo wakati huo, hakuweza kuwandiwa hati. Kwa hiyo mimi na mke wangu tukaanza ujenzi kidogo kidogo hadi nyumba ikakamilika baada ya miaka mingi,” alisema Forodha ambaye kutokana na hali yake kuwa katika hali ya kuchanganyikiwa, aliomba maelezo zaidi yatolewe na mke wake.

Mkewe, Rose Forodha alisema kwa kipindi chote hicho walikuwa na uhusiano mzuri, lakini hali ilikuja kubadilika baada ya yeye (Rose) kumtaka tajiri wao (Diana) alipe deni ambalo yeye alimkopea kwa mtu.

“Kuna mtu nafahamiana naye vizuri, ana duka la Hardware (vifaa vya ujenzi), sasa akawa ananiambia nimkopee na mimi kwa kuwa namfahamu ni mtu mwenye uwezo, nikawa nakopa lakini deni likawa kubwa, mwenyewe akawa anataka hela yake, nilipomwambia ndipo hali ilipoanza kubadilika.

“Kwanza alitutaka tuondoe paa ambalo alisema linamwaga maji upande wake, tukalazimika kupandisha paa letu juu ili kuzuia maji ya mvua kuangukia upande wake. Baadaye akaja akajenga ukuta kutuziba kabisa upande tulioweka madirisha kwa ajili ya kupata hewa. Tukaenda serikali ya mtaa wakamwambia avunje ule ukuta lakini akakataa.

“Badala yake akaanzisha kesi, lakini sisi hatukuwahi kuitwa huko mahakamani. Yaani kesi ya upande mmoja hadi akaja tu kutuambia ameshinda kesi. Ikabidi tumtafute mwanasheria wa kutusaidia, alipofuatilia ndiyo ikaonekana alitushtaki sisi kama wakimbizi wakati kiwanja alitupatia mwenyewe, tena mbele ya mashahidi wengi tu.

“Sasa wakili wetu akakata rufaa Mahakama Kuu na hivi hapa tunasubiri siku ya kesi tuitwe, lakini tunashangaa leo ghafla amekuja hapa na mabaunsa na polisi wa Mabwapande wamesimamia. Tumewaomba karatasi za kuonyesha kwamba wameruhusiwa na mahakama hawatuonyeshi. Wanasema tu huyu anayesimamia zoezi ni dalali wa mahakama. (Analia).

Akizungumza kwa shida huku akilia, mama huyo alisema alijaribu kuwaomba wabomoaji hao wampe nafasi japo ya kutoa vitu vyake nje lakini wakakataa hali iliyosababisha upotevu wa vitu vyake vingi, ikiwamo fedha zaidi ya shilingi milioni nne zilizokuwa ndani kwake.

“Mimi nachezesha michezo ya wanawake na ninakaa na hela za watu maana nina vikundi vingi, pesa zangu zimepotea, vitu vyangu vimevunjwa hovyo na vitu vingine vimepotea kusikojulikana. Sijui hata nitafanya nini mimi,” alisema mwanamke huyo.

Alisema mwanamke huyo anajivunia dada yake aliyemtaja kuwa ni Anna Tibaijuka, aliyewahi kuwa Waziri siku za nyuma.

“Anajivunia huyo dada yake, anasema yeye ana hela na hatuwezi kumfanya kitu maana serikali ipo mikononi mwake. Hapa hata akiitwa ofisi za serikali ya mtaa haendi, anasema hadhi yake si ya kuitwa na ofisi kama hiyo. Hapa mtaani anagombana na kila mtu. Kuna siku wale watu waliokuwa wanamdai walimkamata na kumweka ndani, akaja huyo dada yake akamlipia na akatoka, toka siku hiyo hatunywi maji,” alisema.

 

MSIKIE MWENYEKITI WA SERIKALI YA MTAA

Ojuku Blog ilizungumza na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kihonzile, Hassan Mnondwa alisema yeye ni mkazi wa mtaa huo kwa miaka mingi na anafahamu kuhusu familia hiyo kupewa kiwanja hicho miaka ya nyuma. Alisema anatambua pia kuhusu chanzo cha mgogoro huo na ofisi yao inalifahamu vyema jambo hilo.

“Mgogoro huu tunafahamu kuwa ulikuwa mahakamani, juzi nilipigiwa simu na OCD wa Mabwepande akaniambia kama nina taarifa za nyumba ya mkazi wangu kuvunjwa, nikasema sina taarifa. Lakini cha kushangaza akasema ofisi yetu inafahamu na kwa hiyo anatuma askari ili waje kushirikiana na mimi kwenye uvunjaji.

“Nilipomwomba kama kuna nyaraka zozote za uvunjaji huo akasema tayari zilishasainiwa na mahakama tokea mwezi wa kwanza. Mimi nikasema sitashiriki zoezi hilo bila kuona nyaraka hizo. Wakaja ofisini wakanikuta, nikawapa msimamo wangu. Wakampigia Mtendaji ambaye aliwaambia alikuwa njiani, wakamsubiri na alipokuja wakaondoka naye kuja hapa bila mimi kuona hizo nyaraka,” alisema.

Alipoulizwa kama Mtendaji anaweza kufanya jambo bila ya kumshirikisha yeye, alidai jambo hilo linawezekana kwa kuwa kila mmoja ana muhuri wake na anaamini kiongozi huyo ameshiriki zoezi hilo bila kumshirikisha.

 

MWANASHERIA NAYE ASHUSHA NONDO ZAKE

Mwanasheria wa familia hiyo, Noelina Bippa alisema alianza kuisadia familia hiyo baada ya hukumu katika shauri la awali kuwa limeshahukumiwa, kitendo kilichomlazimu yeye kuomba rufaa ambayo ilikubaliwa na walikuwa wakisubiri siku ya kusikilizwa.

Alipoulizwa kama wabomoaji wanaweza kutumia hukumu ya awali kutekeleza walichokifanya, alisema kisheria inawezekana lakini katika mazingira yafuatayo:

“Hukumu ya awali ingeweza kutekelezwa kama tu mahakama ingetoa taarifa ya maandishi kwa familia juu ya nia ya kuvunja nyumba hiyo. Ingeweza kuwa siku 7 au 14. Sasa kama taarifa hiyo ingetolewa, sisi tungeitumia ili kuomba kusitishwa kwa jambo hilo kwa vile kuna rufaa.

“Nafikiri hawa walijua jambo hili, ndiyo maana waliamua kuvunja bila notisi jambo ambalo ni kinyume cha sheria. Tutafuatilia mahakamani ili tuone cha kufanya,” alisema mwanasheria huyo.

Diana Alex Tibaijuka hakuweza kupokea simu kila alipopigiwa. Blog hii itaendelea kumtafuta ili kupata maelezo ya upende wake.

No comments