Shauri dhidi ya Mbunge Gekul lasikilizwa Mahakamani, Wakili Madeleka asema DPP hakuwa na Mamlaka ya kufuta kesi

 


Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Manyara imesikiliza shauri la Jinai namba 577/2024 mbele ya Jaji Devotha Kamuzora, linalomhusu Hashim Ally ambaye ni Mrufani dhidi ya Mbunge wa Babati Mjini, Pauline Gekul ambaye ni Mrufaniwa.

Katika rufaa hiyo, Ally anapinga maamuzi yaliyofanywa na Mahakama ya Wilaya ya Babati mnamo Desemba 27, 2023 ya kuiondoa kesi hiyo Mahakamani baada ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kutokuwa na nia ya kuendelea na kesi hiyo.

Gekul alidaiwa kumshambulia na kumdhuru Ally Novemba 11, 2023 kinyume cha Kifungu cha 41 cha Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 ya 2022.

Mmoja wa Mawakili wa Mrufani, Peter Madeleka anaelezea kilichotokea kwa kusema “Shauri limesikilizwa lakini jana Machi 20, 2024 Mrufaniwa Pauline Gekul alisajili pingamizi la awali kwa kuweka mapingamizi matatu Mahakamani akipinga rufaa hii kusikilizwa.

“Mahakama ilianza kusikiliza mapingamizi ya Mrufaniwa na baada ya kusikiliza ikaendelea kusikiliza rufaa yenyewe iliyowasilishwa na Hashim Ally.

“Mahakama imepanga kutoa uamuzi Aprili 15, 2024, katika hoja za pingamizi zilizowasilishwa na Mrufaniwa, anadai Mahakama haikuwa na uwezo wa kusikiliza rufaa hii kwa kuwa sababu ya kwanza na ya pili ilihusisha hoja ya katika na hii si Mahakama ya Kikatiba.

“Pili anasema rufaa hii imekuja mapema mno, imejichanganya na haina maana yoyote, tatu anasema rufaa hii inapaswa kutozingatiwa kwa ujumla.

“Mrufani (Hashim Ally) kupitia Mawakili wake Peter Madeleka, Thadei Lista na Joseph Masanja katika kupinga mapingamizi hayo tulisema hayana mashiko kwa kuwa Mahakama hii ina uwezo wa kisheria chini ya Kifungu cha 300 (59) na 300 (61) kupokea rufaa zote zinazotokana na maamuzi ya Mahakama za chini.”

Upande wa Wakili Ephraim Kisanga ambaye ni Wakiliwa Mahakama Kuu aliyekuwa akimuwakilisha Pauline Gekul amesema:

“Shauri lilipangwa kusikilizwa, limesikilizwa na Mahakama Kuu, kabla ya hapo siku moja kabla tuliwasilisha mapingamizi matatu.

“Mapingamizi yote matatu yamesikilizwa na rufaa pia imesikilizwa, Mahakama imesema Aprili 15, 2024 itatoa uamuzi mdogo wa mapingamizi na kama yatakuwa hayana mashiko, siku hiyohiyo tutarejea kwa ajili ya hukumu ya rufaa iliyowasilishwa.”

Jamii Forum

No comments