Sababu tatu zinazomfanya Putin kuwa na nguvu zaidi ya awali
Rais wa Urusi Vladimir Putin ameshinda muhula wa tano madarakani na kumtengenezea njia ya kuiongoza nchi hiyo hadi angalau 2030.
Katika hotuba yake ya ushindi alisema ushindi wake utaiwezesha Urusi kustawi kwa kuwa na "nguvu na ufanisi zaidi".
Alishinda kwa kuvunja rekodi ya 87% ya kura, na kupita rekodi ya awali ya 76.7% ambayo alipata katika uchaguzi uliopita.
Ingawa hakukabiliwa na mgombea wa upinzani anayeaminika, kwa vile Kremlin inadhibiti mfumo wa kisiasa wa Urusi, vyombo vya habari na uchaguzi vinasema.
Viongozi wengi wa nchi za Magharibi walishutumu uchaguzi huo kuwa haukuwa huru na wa haki, akiwemo rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, ambaye alimwita Putin kuwa ni "dikteta" ambaye "amelewa madaraka", na kuongeza: "Hakuna uovu ambao hataufanya ili kurefusha mamlaka yake binafsi."
Putin, 71, ambaye alikua rais kwa mara ya kwanza katika siku ya mwisho ya 1999 - tayari ndiye kiongozi wa Urusi aliyekaa muda mrefu zaidi tangu Joseph Stalin, na sasa anaweza kuvuka rekodi ya dikteta wa Soviet.
Licha ya Warusi kufariki katika vita vya Ukraine, huo ni mwaka wa tatu sasa na Urusi kutengwa na nchi za Magharibi, hizi hapa sababu tatu zinazofanya Putin kuwa na nguvu zaidi kuliko hapo awali.
Kupinga na kuondoa upinzani
"Putin anajua jinsi ya kukandamiza kila aina ya mijadala ya kisiasa nchini," anaeleza Andrei Soldatov, mwandishi wa habari wa Urusi ambaye amekuwa akiishi uhamishoni London tangu alipolazimika kutoroka mwaka wa 2020 pia ni mzuri sana katika kuwaondoa wapinzani wake wa kisiasa," anaongeza.
Ni wagombea wengine watatu pekee waliojitokeza kwenye kura ya uchaguzi wa 2024, na hakuna aliyethibitisha kuwa changamoto kwa Putin.
Wote walishiriki uungaji mkono wa wazi kwa rais na vita vya Ukraine.
Vitisho vya kweli kwa wadhifa wa rais aidha ni kufungwa, kuuawa au kuondolewa kwa njia nyingine, ingawa Urusi inakanusha kuhusika.
Mwezi mmoja tu kabla ya uchaguzi kufunguliwa, mpinzani mkali wa Putin, Alexei Navalny mwenye umri wa miaka 47, alifariki katika gereza lililoko juu ya Arctic Circle.
Alikuwa akitumikia kifungo cha muda mrefu jela kwa makosa ya ulaghai, kudharau mahakama na itikadi kali, ambayo yalishutumiwa kuwa yalichochewa kisiasa.
"Putin anapuuza sana upinzani wake," anasema Soldatov.
"Majibu yake mtu muhimu kisiasa anapouawa ni kusema 'hawana maana' na anarejelea msemo wake maarufu ulioenea kwamba 'kwanini niwaue?'
Kremlin ni nzuri sana katika kutoa visingizio hivi."
Wapinzani kadhaa maarufu wa Putin wamefariki kuanzia wanasiasa hadi waandishi wa habari.
Mwaka jana, kiongozi wa kundi la mamluki binafsi la Wagner, Yevgeny Prigozhin, alifariki katika ajali ya ndege miezi michache tu baada ya jaribio kubwa la uasi.
Mnamo mwaka wa 2015, mkosoaji mkubwa na mwanasiasa, Boris Nemtsov, alipigwa risasi na kuuawa kwenye daraja karibu na Kremlin na mnamo 2006, mwandishi wa habari ambaye alikosoa sana vita huko Chechnya, Anna Politkovskaya, alipatikana ameuawa kwa kupigwa risasi huko Moscow.
"Inatisha sana kuishi katika nchi ambayo waandishi wa habari wameuawa, wanasiasa na wanaharakati kwameuawa na kufungwa," anasema Soldatov.
"Inasikitisha sana kisaikolojia, kwa hivyo watu wa kawaida wako tayari kununua simulizi la Kremlin sio kwa sababu tunaamini, lakini kwa sababu tunataka kutafuta njia ya kuishi nayo."
Putin pia amejaribu kudhibiti upinzani binafsi katika umma kwa ujumla.
Tangu 2022, kufuatia uvamizi wa Ukraine, Kremlin ilianzisha sheria mpya za udhibiti ambazo zilikandamiza hisia dhidi ya serikali, na makosa mapya kama "kudharau jeshi la Urusi" ambayo yanaadhibiwa kwa hadi miaka mitano jela.
Rais alisema maandamano wakati wa uchaguzi huu "hayakuwa na athari" na "uhalifu" wowote utaadhibiwa baada ya kura.
"Siku hizi sio kuhusu ripoti fulani kwenye BBC au Radio Free Europe" anasema Soldatov.
"Nikuhusu watu ambao wanaweza kushuhudia kitu mitaani na kukiweka mara moja na kikashirikiwa na mamilioni ya watu.
"Putin ana imani hii ya udhaifu mkubwa kwa nchi, na ndiyo maana anaamini anahitaji kufanya kila kitu ili kukandamiza kila aina ya upinzani kwa sababu mapinduzi yajayo yanaweza kuanza na wasichana wawili au watatu tu kuandamana mitaani."
Vita vya Ukraine
Vita katika Ukraine sasa vimeingia mwaka wayo wa tatu
Katika mkutano na waandishi wa habari baada ya uchaguzi, Rais Putin aliapa kuendelea na uvamizi wa Ukraine.
Sasa katika mwaka wake wa tatu, vita havikuwa na ushindi wa haraka ambao wengi nchini Urusi walikuwa wakitarajia lakini Dk Ekaterina Schulmann, mwanasayansi wa siasa wa Urusi aliyeko Berlin, anasema Putin anatumia vita hivyo kwa manufaa yake.
"Ilipoanza, ilipaswa kuwa kama mtindo wa Crimea, lakini hii ilifaa kuwa kubwa zaidi," anasema lakini "haikuwa ndogo au isiyo na kudumu na iliathiri jinsi Warusi wanavyojiona, ulimwengu wa nje na kiongozi wao".
Dk Schulmann anaamini kuwa uvamizi wa tarehe 24 Februari 2022 haukuwa jambo kubwa kwa Warusi kama ilivyokuwa kwa wale walio nje ya nchi.
Soldatov anakubali, na anaamini, kwa kupungua kwa msaada wa vita nchini Urusi, Putin alibadilisha simulizi.
"Sasa sio vita tena na Ukraine," anasema, "lakini badala yake ni vita na Magharibi, na hii inawafanya Warusi wengi wajisikie fahari kwa sababu jeshi sio tu linatekeleza jukumu lake kwa nchi ndogo, lakini badala yake bado wanajivunia kuwa katika mapambano dhidi ya mpinzani mkubwa zaidi".
Katika hotuba yake ya kila mwaka ya hali ya taifa tarehe 29 Februari, Putin alizionya nchi za Magharibi dhidi ya kutuma wanajeshi wake Ukraine na kusema Urusi inahitaji kuimarisha ulinzi wake huku Sweden na Finland zikijiunga na Nato.
"Kila mtu nchini, ikiwa ni pamoja na mimi, tulifundishwa shuleni kwamba Milki ya Urusi ndiyo milki pekee duniani ambayo ilijengwa na watu wenye amani," anasema Soldatov. "Kila mtu alitaka kutushambulia kwa hivyo unapouza simulizi kwamba Nato inaelekea kwenye mipaka yako, watu wako tayari kununua simulizi hii."
Zaidi ya hayo, Soldatov anaamini kuwa nchi za Magharibi hazijafanya kazi ya kutosha ya kuelezea ulimwengu kwa nini vita vya Ukraine ni muhimu.
"Watu wa Afrika, Amerika ya Kusini, kwa mfano, hawaelewi kwa nini wanapaswa kujali, na hili ni pengo ambalo Putin ametumia," anasema.
Ukuaji wa uchumi wa Urusi
Licha ya viwango visivyo na kifani vya vikwazo vilivyowekwa dhidi ya Urusi kufuatia uvamizi wa Ukraine, nchi hiyo imewashangaza wanauchumi wengi kwa kuwa uchumi unaokuwa kwa kasi zaidi barani Ulaya.
"Uchumi unafanya kazi vizuri, mambo yote yakizingatiwa, na umemfanya Putin kuwa maarufu kwa sababu anajionyesha tena kama mtu ambaye amepinga nchi za Magharibi katika shambulio lake kubwa la uchumi wa Urusi," anasema mwandishi wa BBC Kirusi wa biashara, Alexey Kalmykov.
Badala ya kushuka kama wengi walivyotarajia, uchumi wa Urusi umeongezeka kwa 2.6%, kulingana na makadirio ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), licha ya vikwazo vya Magharibi, ambavyo ni pamoja na kuzuia mali yenye thamani ya $ 300bn.
Lakini vikwazo hivi havijatekelezwa kwa upande mmoja kote ulimwenguni.
Hii inaruhusu Urusi kufanya biashara kwa uhuru na nchi kama vile Uchina, India na Brazil wakati majirani zake, pamoja na Kazakhstan na Armenia, wanaisaidia Urusi kukwepa vikwazo vya Magharibi.
"Urusi ni uchumi mkubwa," anasema Kalmykov, akiongeza: "Itachukua miongo kadhaa ya vikwazo na usimamizi mbaya kumaliza uchumi wa Urusi."
"Urusi inapata pesa kwa kuuza bidhaa nje na kimsingi iko huru kuuza chochote inachopenda," anaelezea Kalmykov.
"Vikwazo vya mafuta ni mapambo, na gesi asilia, nafaka na nishati ya nyuklia hazijaguswa hata kidogo na mnunuzi mkuu wa Urusi - EU."
Lakini haiwezi kudumu milele...
Ijapokuwa Putin anaonekana kuwa na nguvu zaidi kuliko hapo awali, Dk Schulmann anaonya hili hatimaye lazima lifike mwisho.
Shukrani kwa marekebisho ya 2020 ya katiba ya Urusi katika kura ya maoni ya nchi nzima, Putin anaruhusiwa kuhudumu kwa angalau mihula miwili zaidi ya miaka sita, ambayo inaweza kumfanya kuwa rais hadi 2036 - wakati atakuwa na umri wa miaka 83.
"Kustaafu halinijii akilini kama jambo linalowezekana," Dk Schulmann anasema, akiongeza: "Kwa kweli, anahitaji kufia ofisini na kurithiwa na watu ambao wana mtazamo sawa wa kiimla."
Lakini Dk Schulmann anasema kuwa hilo linaweza lisitokee. Anasema mfumo wa Urusi " unazeeka" na "unaongozwa na mtu ambaye anaendelea kuzeeka, mwenye nguvu zaidi au mvumilivu zaidi", akihitimisha, "uthabiti wote uko kwenye mtu mmoja" ambaye "hawezi kuishi milele".
bbc

Post a Comment