MTENDAJI MKUU TARURA: DARAJA LA MINYUGHE, WILAYANI IKUNGI, SINGIDA LITAFUNGUA FURSA ZA KIUCHUMI

 Ikungi -Singida,

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini Nchini Mhandisi Victor H. Seff amesema Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan imekamilisha ujenzi wa daraja linalounganisha Kata ya Minyughe na Makilawa,katika wilaya ya Ikungi mkoani Singida, lililokatika miaka mitatu iliyopita, na hivyo kuathiri shughuli za kiuchumi na upatikanaji wa huduma za kijamii ikiwemo afya na elimu.

Kukamilika kwa daraja hilo la chuma (Mabey Bridge) lenye urefu wa mita 30 katika barabara ya Mtamaa-Minyughe hadi Mtavira, Wilayani Ikungi, litaenda kufungua fursa ya kiuchumi kwa wananchi wa kata hızo.

Naye meneja wa Wakala ya Barabara Vijijini na Mijini (TARURA), Mkoa wa Singida, Mhandisi Ibrahim Kibasa, alisema kukamilisha uunganishaji wa vyuma kwa ajili ya daraja hilo, kumewezesha mto Minyughe kufunguka, na hivyo kutoa fursa kwa shughuli za uchukuzi kuendelea kati ya maeneo ya vijijini na makao makuu ya mkoa.

Mhandisi Kibasa alisema kuwa, sasa wananchi wa kata tatu zinazounganishwa na daraja hilo, wataweza kuzikabili changamoto mbalimbali zilizokwamisha shughuli zao hususani wakati wa masika kutokana na mto kufurika maji kiasi cha kutishia usalama wao wakati wa kuvuka.


" Sehemu ya fedha hizo ni bajeti ya mwaka huu ambapo tumejenga madaraja ikiwemo daraja hili la Minyughe, daraja hili limekuwa likiwasumbua wananchi takribani miaka mitatu na hivyo kukwamisha utekelezaji wa shughuli za kiuchumi kwa wananchi wa Kata tatu pamoja na Mkoa wa jirani wa Tabora, katika wilaya ya Uyui, inayopakana na wilaya hii ya Ikungi, "alisema.

Aidha, Mhandisi Kibasa alisema, ujenzi wa daraja hilo umetokana na bajeti ya mwaka iliyotengwa kiasi cha Sh. Bilioni 4.4/- katika wilaya ya Ikungi kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya barabara na madaraja katika halmashauri ya Wilaya hiyo.


Baadhi ya wananchi walioshuhudia kukamilika kwa kazi hiyo, akiwemo Bi. Elizabeth Bakari wa Kijiji cha Minyughe, na diwani wa Kata Minyughe , Mhe. Nelson Kiwesi, waliishukuru Serikali kwa mradi huo ambao baada ya kukamilika unakwenda kuondoa adha ya usafiri hasa kwa wajawazito.

Bi. Elizabeth alibainisha kuwa, iliwalazimu kukosa huduma muhimu ikiwemo zile za afya katika kituo cha afya kilichopo ng'ambo ya pili.

No comments