Meli ya kwanza iliyobeba misaada yaondoka Cyprus kuelekea Gaza

 


Meli iliyokuwa ikipeleka karibu tani 200 za chakula hadi Gaza iliondoka bandarini nchini Cyprus mapema Jumanne, katika mradi wa majaribio wa kufungua njia mpya ya bahari ya msaada kwa wakazi wanaokabiliwa na njaa.

Meli iliyobeba msaada ya Open Arms ilionekana ikitoka katika bandari ya Larnaca huko Cyprus, ikivuta jahazi lililokuwa na unga, mchele na protini.

Meli hiyo ni ya shirika la kutoa misaada la Uhispania.

Ni wapi inapanga kutia nanga itakapofika Gaza haijafichuliwa.

Misheni hiyo, inayofadhiliwa zaidi na Umoja wa Falme za Kiarabu, inaandaliwa na shirika la kutoa misaada la World Central Kitchen (WCK) lenye makao yake makuu nchini Marekani, huku shirika la misaada la Uhispania likitoa meli hiyo.

"Lengo letu ni kuanzisha barabara kuu ya baharini ya boti na mashua zilizojaa mamilioni ya milo inayoendelea kuelekea Gaza," mwanzilishi wa WCK Jose Andres na afisa mkuu mtendaji Erin Gore walisema katika taarifa.

Mpango huo ni tofauti na mpango wa Marekani wa kujenga na kuendesha gati inayoelea karibu na pwani ya Gaza, ambayo itaruhusu utoaji wa haraka wa misaada ya kibinadamu.

Mashirika ya misaada yananuia kuchukua misaada moja kwa moja hadi Gaza, ambayo imefungiwa kutoka kwa ulimwengu wa nje tangu Israeli ilipoanza mashambulizi ya kulipiza kisasi kutokana na shambulizi lililotekelezwa na Hamas dhidi ya Israel Oktoba 7.





No comments