Urusi yamshikilia mwanamume wa Korea Kusini kwa tuhuma za ujasusi

 


Mwanaume mmoja raia wa Korea Kusini amezuiliwa nchini Urusi kwa tuhuma za ujasusi, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali ya Urusi.

Wizara ya mambo ya nje ya Korea Kusini pia imethibitisha kukamatwa kwa watu hao, ikisema walikuwa wakijaribu kutoa msaada wa kibalozi.

Baek Won-soon alikamatwa katika jiji la mashariki ya mbali la Vladivostok "mwanzoni mwa mwaka", shirika la serikali la Tass liliripoti, na sasa yuko katika jela ya Moscow.

Anaaminika kuwa raia wa kwanza wa Korea Kusini kuzuiliwa nchini Urusi kwa tuhuma za ujasusi.

Ni machache yanayojulikana kuhusu kesi yake, huku wizara ya mambo ya nje ya Korea Kusini ikisema "maelezo" yanachunguzwa na "ni vigumu kutoa maoni".

Lakini vyombo vya habari vya serikali ya Urusi Tass vilimnukuu afisa ambaye hakutajwa jina katika ripoti yao akisema Bw Baek anadaiwa kupitisha taarifa "zinazounda siri za serikali kwa idara za kijasusi za kigeni."

Vyombo vya habari vya Korea Kusini vimeripoti kuwa Seoul iliarifiwa rasmi tu na mamlaka ya Urusi juu ya kukamatwa kwake mwezi uliopita.

Yonhap, kituo cha Korea Kusini, kinaripoti kwamba Bw Baek alikamatwa na Huduma ya Usalama ya Shirikisho la Urusi mnamo Januari baada ya kuwasili Vladivostok kutoka Uchina.

Kituo hicho kilisema yeye ni mfanyakazi wa kidini na alikuwa ameandamana na mkewe, ambaye pia alizuiliwa lakini baadaye aliachiliwa. Inaaminika kuwa amerejea Korea Kusini, chombo hicho kiliripoti.

Kuzuiliwa kwa Bw Baek ni tukio la hivi punde zaidi katika msururu wa kukamatwa kwa raia wa kigeni uliofanywa na mamlaka ya Urusi tangu vita vya Ukraine vianze miaka miwili iliyopita. Moscow imeshutumiwa kwa kuwakamata raia wa nchi nyingine ili kuwatumia kwa misingi ya kisiasa na kubadilishana wafungwa.

BBC

No comments