Mahakama ya Marekani yatupilia mbali kesi ya kuwatumikisha watoto katika migodi ya DRC
Mahakama ya rufaa ya Marekani Jumanne ilitupilia mbali kesi iliyodai kuwa kampuni tano kuu za teknolojia zilihusika katika shughuli ya ajira ya watoto kuchimba madini ya kobalti katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Kesi hiyo ilizitaja Apple, Microsoft, Tesla, Dell Technologies na kampuni mama ya Google Alphabet.
Mahakama iliamua kwamba ununuzi wa cobalt na makampuni haukumaanisha kuwa walishiriki katika ajira ya watoto.
Jaji Neomi Rao pia alisema kuwa walalamikaji walikosa kuonesha kwamba kampuni zinazoshtakiwa zilikuwa na ushawishi wa kukomesha matumizi ya watoto katika migodi.
Kesi hiyo iliwasilishwa kwa mara ya kwanza mnamo 2019 na shirika la haki za binadamu la International Rights Advocates, ambalo lilikuwa likiwakilisha watoto walionusurika ambao walipata majeraha wakifanya kazi katika migodi ya kobalti ya Congo na familia za watoto waliokufa kwenye migodi.
Ilitupiliwa mbali na mahakama ya chini mwaka wa 2021, na kusababisha kukata rufaa.
DR Congo inazalisha 60% ya cobalt duniani, madini muhimu yanayotumika katika utengenezaji wa vifaa vingi vya kielektroniki.
Takribani watoto 25,000 wanafanya kazi kwenye migodi ya kobalti nchini DR Congo, kulingana na Idara ya Kazi ya Marekani, mara nyingi katika mazingira hatari.
BBC

Post a Comment