KWAHERI THOMAS"TOM" SHEMPEMBA MCHEZAJI BORA WA BASKETBALL WA MUDA WOTE TANZANIA
Jana tarehe 5/3/2024 familia ya mpira wa kikapu Tanzania ilipokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha Tom Shempemba, mchezaji nyota wa zamani wa mpira wa kikapu wa Pazi Basketball Club. Kifo hicho kimetokea mjini Tanga.Tom ni mtoto wa Mbunge wa zamani wa Lushoto, Raphael Shempemba.
Tom alikuwa ni matunda ya uwekezaji mkubwa wa timu ya vijana ya Pazi uliofanywa na uongozi wa Pazi chini ya Mzee Serve Malai, ambaye pia alikuwa kocha na mchezaji wa zamani wa Pazi.Watu wengi tuliokuwa tunafuatilia mazoezi na mechi za timu ya Vijana ya Pazi mwanzoni mwa miaka ya 1980 tuliona mapema kipaji kikubwa cha "mfalme" huyu wa Basketball Tanzania na haikushangaza alipokuja kupandishwa timu ya wakubwa ya Pazi akiwa na umri mdogo sana kwenda kucheza na wakongwe kina Salehe Zonga (Rip), Abdallah Aboud (Rip) ,Hassan Kange, Pius Gogadi, Dkt Hassan Mtwange nk.
Wazazi wa Tom waliishi maeneo ya jirani na Gymkhana (Sheraton/Serena Hotel), ulipokuwepo uwanja wa timu ya Pazi kabla haijahamia Tanesco, hivyo ilikuwa rahisi kwake kuanza kucheza mchezo huu katika umri mdogo, yeye pamoja na mdogo wake Amani Shempemba. Baada ya kupandishwa timu kubwa aliingia moja kwa moja kikosi cha kwanza na kuwa mmoja wa wachezaji "wakubwa" Tanzania kuanzia katikati ya miaka ya 1980.
Kipaji chake kilimwezesha kupata ajira Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ambao wakati huo walikuwa wanajenga timu yao ya Basketball. Hata hivyo ndoto ya BoT kummiliki Tom iliyeyuka ghafla alipoamua kuacha kazi na kwenda kuajiriwa TANESCO.
Tom alifikia kilele cha ubora wake mwaka 1988 alipoibeba Pazi mabegani mwake na kuiwezesha kubeba ubingwa wa mpira wa kikapu Tanzania kwa kuifunga ABC iliyokuwa bingwa na kumaliza kabisa utawala wa ABC. Hii ilikuwa ni Pazi bora kabisa iliyokuwa na Tom Shempemba, Raymond Ndahshau, Mbaga Mwamboma ,Abbas Mansour wakichanganyika na Wakongwe Salehe Zonga"Zii", Hassan Kange, Abdallah Aboud, Pius Gogadi, Dkt Hassan Mtwange nk.
Baada ya ubingwa huu Tom aliiongoza Pazi kutawala Basketball ya Tanzania kwa karibu miaka minne hadi utawala wao ulipopinduliwa na Vijana"City Bulls" chini ya kocha Delphinus Penesis na wachezaji Columba Mwingira, Hamim Kissoki, Hilary Ndibalema, Bahati Mgunda, Kibo Mwingira,"Mutombo" nk
Baada ya hapo umri ulianza kusogea na kufikia mwaka 1994 Tom akastaafu kucheza Basketball
PAZI VS BOT NUSU FAINALI YA KLABU BINGWA BASKETBALL TANZANIA 1988
Hii ilikuwa mechi kali sana iliyochezwa pale Gymkhana. Kipaji kikubwa cha Tom Shempemba kilipindua matokeo dakika za mwishoni kabisa katika mechi iliyoonekana dhahiri kama vile BoT wangeshinda baada ya kuongoza kwa sehemu kubwa ya mchezo.Wakati mchezo ukielekea dakika za mwishoni huku BoT wakiongoza, ghafla taa zilizimika uwanjani na kubakia hivyo kwa karibu dakika 10. Baada ya taa kurekebishwa mechi ikageukia upande wa Pazi.Tom Shempemba alifunga basket muhimu hadi kuwakamata BoT ikiwemo ya mwisho na ya ushindi iliyoipeleka Pazi fainali ambako waliifunga ABC na kutwaa ubingwa.
Nenda Tom Shempemba Nenda.Mungu akupe pumziko la milele.
Marehemu ameacha mke na watoto kadhaa

Post a Comment