Je, huu ndio mwanzo wa mgogoro wa Marekani na Israel?
Rais wa Marekani Joe Biden na maafisa wake wakuu, wanaonekana sasa kukosa subira kwa jinsi Israel inavyoendesha vita huko Gaza.
Maafisa wa Marekani walitumia lugha kali zaidi kuelezea Israel na kwa ulimwengu mzima, kutoridhishwa kwao na kile kinachotokea Gaza.
Marekani kuruhusu azimio la kusitisha mapigano kupitishwa katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa - inaonyesha kuwa Rais Biden ameamua kuwa maneno makali kwa Israel hayatoshi.
Kuondoa ulinzi wa kidiplomasia juu ya mwenendo wa Israel katika vita hivyo ni hatua muhimu, huku mpasuko kati ya Ikulu ya White House na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ukionekana kuzidi kupanuka.
Waziri Mkuu Netanyahu alijibu uamuzi huo kwa kumkosoa vikali mshirika huyo ambaye ni muhimu zaidi kwa Israel.
Netanyahu alilaani kushindwa kwa Marekani kutumia mamlaka yake ya kura ya turufu dhidi ya azimio hilo, akisema "imeathiri juhudi za vita na majaribio ya kuwakomboa mateka waliochukuliwa na Hamas Oktoba 7, mwaka jana.''
Biden na maafisa wake wakuu wanaweza kuzitafsiri kauli hizi kama "kukosa shukrani kulikopindukia."
Rais Biden anaunga mkono sana Israel, anajiita Mzayuni, na amewapa watu wa Israel misaada yote ya kijeshi na kidiplomasia ambayo nchi yao inahitaji tangu Oktoba 7 mwaka jana.
Anataka mateka waachiliwe huru pamoja na Hamas kama jeshi livunjwe. Lakini anataka Israel ifanye hivyo kwa "njia sahihi," kama alivyosema.
Katika wiki za kwanza za vita vya Gaza, Rais Biden alionya Israel kutopofushwa na hasira, kama Marekani ilivyopofuka baada ya mashambulizi ya al-Qaeda Septemba 11, 2001.
Rais wa Marekani mwenyewe alisafiri hadi Israel, kuzifariji familia za wahanga wa mashambulizi ya Hamas, na hata kumkumbatia Netanyahu.
Biden na Waziri wake wa Mambo ya Nje, Anthony Blinken, ambaye ameitembelea Israel mara sita tangu mashambulizi ya Oktoba, mara kadhaa wameiomba Israel kuheshimu sheria za kimataifa, ambazo ni pamoja na wajibu wa kuwalinda raia.
Mwanzoni mwa vita, wakati Marekani ilipokuwa ikifuatilia vita na kuandaa maonyo yake ya kwanza, Waziri Mkuu Netanyahu aliwaahidi Waisraeli kile alichokiita "kisasi kikubwa."
Tangu wakati huo, zaidi ya Wapalestina 30,000, wengi wao wakiwa raia, wameuawa kwa silaha ambazo baadhi zinazotolewa na Marekani.
Huku Gaza ikiwa magofu, njaa inawakabili raia wa Palestina, na uwezekano wa wengine wengi kuuawa katika mashambulizi ya Israel huko Rafah kusini mwa Gaza, Rais Biden anaonekana kuchoshwa kutokana na ushauri wake kupuuzwa.
Israel inadai siku zote imekuwa ikiheshimu sheria za vita na inakanusha kuwa inazuia misaada ya kibinadamu kuwafikia watu wa Gaza.
Lakini kuna ushahidi mkubwa kwamba Israel haisemi kweli, huku watoto wakifa kwa njaa – kutoka maili chache kwenye maduka ya chakula huko Israel na Misri.
Marekani, pamoja na mataifa mengine ya dunia, wanaona ushahidi uliotolewa na Umoja wa Mataifa na mashirika ya misaada, ambayo yote yanasema Gaza iko kwenye ukingo wa njaa ni wa kweli
Jeshi la Marekani linatoa misaada kupitia anga na kuweka bandari ya muda katika Bahari ya Atlantiki ili mahitaji yaweze kufika Gaza kwa njia ya bahari, huku Israel ikiruhusu kiasi kidogo tu kuingia katika bandari ya Ashdod, kituo kilicho umbali wa nusu saa tu kwa gari kaskazini mwa Gaza.
Uamuzi wa Washington kutotumia kura yake ya turufu dhidi ya azimio la kusitisha mapigano katika mwezi wa Ramadhani - ni jaribio la Marekani kujibu tuhuma kwamba wameipa Israel uhuru wa kufanya itakavyo huko Gaza.
Haya yanajiri baada ya Netanyahu kukataa vikali mipango ya utawala wa Biden kutafuta njia ya kutatua mzozo mbaya zaidi katika Mashariki ya Kati kwa miongo kadhaa.
Marekani inajaribu kuonesha kuwa kutokujali kwa Israel mbele ya shinikizo la kimataifa kuna mipaka.
Zaidi ya nyumba 70,000 zimeharibiwa kabisa katika Ukanda wa Gaza tangu kuanza kwa vita
Maazimio ya Baraza la Usalama kwa kawaida huchukuliwa kuwa na nguvu sawa na sheria za kimataifa. Israel lazima iamue sasa iwapo itaheshimu azimio hilo, ambalo lilikaribishwa na Hamas na mwakilishi wa Palestina katika Umoja wa Mataifa.
Lakini serikali ya mseto ya Netanyahu inayoungwa mkono na watu wa itikadi kali za kitaifa za Kiyahudi, watamtaka Netanyahu kupuuza uamuzi huo. Ikiwa atafanya hivyo, itabidi Marekani ijibu.
Na ikiwa kauli za Marekani hazitatosha kwa Netanyahu, njia muhimu kwa Rais Biden ni udhibiti wa anga inayosambaza silaha kwa Israel - kupitia makumi ya ndege kubwa za usafirishaji zinazoleta silaha kwa Israel. Na Israel inataka silaha hizo ili kusonga mbele na mpango wake wa kupanua vita vya ardhini hadi Rafah.
Urafiki kati ya Marekani na Israel ni mkubwa, na ulianza mwaka 1948 wakati Rais wa Marekani Harry Truman alipotambua uhuru wa Israel dakika 11 baada ya kutangaza kuanzishwa kwake, lakini urafiki huu wakati mwingine una changamoto zake.
Migogoro hutokea kati ya pande hizo mbili wakati Israel inapokaidi matakwa ya marais wa Marekani na kudhuru kile kinachoonekana kuwa maslahi ya Marekani.
Hii si mara ya kwanza kwa Benjamin Netanyahu kuwakasirisha maafisa wa Ikulu ya Marekani, kwani amekuwa akifanya hivyo mara kwa mara tangu alipokuwa waziri mkuu wa Israel kwa mara ya kwanza mwaka 1996.
Lakini mvutano wake na Marekani haujawahi kuwa mkubwa na mgumu kama wakati huu, na urafiki wa muda mrefu wa Marekani na Israel haujawahi kukabiliwa na mzozo mkubwa kama unaozuka wakati huu wa vita vya Gaza.
bbc

Post a Comment