Jaji Mkuu, Waziri Jerry Silaa na Paul Makonda wasikilizwe
KWA nyakati tofauti, viongozi wawili wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM) na Serikali wameonyesha kutoridhishwa kwao na namna Idara ya Mahakama
inavyoshughulikia migogoro ya Ardhi nchi nzima.
Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Paul Makonda akiwa
katika ziara yake ya kusikiliza kero za wananchi katika mikoa mbalimbali, wengi
wakionekana kusononeshwa na namna watu wenye fedha wanavyowadhulumu viwanja,
mashamba na ardhi kupitia hukumu zinazotolewa na mahakama za ngazi mbalimbali.
Katika kile alichoonyesha kukubaliana nao, Makonda aliwashauri
wananchi kutokimbilia mahakamani mara wapatapo matatizo kwenye migogoro ya
ardhi, kwani huko watu wenye fedha wana nafasi nzuri za kushinda mashauri hayo.
Kuonyesha kwamba anamaanisha anachokisema, Mkuu huyo wa Mkoa wa
Dar es Salaam wa zamani, aliwaambia kuwa yeye binafsi aliwahi kudhulumiwa
nyumba na watu wakamshauri aende mahakamani, lakini akafikiri na kuona kuwa
kutokana na ukwasi wa mdhulumishi wake, asingeweza kushinda endapo angeenda
mahakamani.
Kana kwamba hilo halitoshi, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo
ya Makazi, Jerry Silaa, ambaye anakutana na changamoto nyingi hivi sasa katika
migogoro ya ardhi, naye amewashauri, siyo tu wananchi, bali hata maofisa ndani
ya wizara yake, kutowashauri wananchi kwenda mahakamani kwenye ishu za
migogoro.
Waziri Silaa amefafanua kuwa katika Sekta ya ardhi, ina jukumu la kitu kinaitwa
administrative justice (inatoa haki ya kiutawala), kwamba yapo mambo na
wataalam wa wizara ya ardhi ameshawaagiza waache tabia ya kugeuka washauri wa
sheria wa wananchi.
Anasema unakuta raia anakuja na vielelezo vyote muhimu vya umiliki wa ardhi,
lakini eneo lake anakalia mtu mwingine, hivyo anavyokutana na wataalam wa
wizara, badala ya kutoa haki ya kiutawaka, wanageuka kuwa washauri wa sheria,
wanawaambia wananchi waende mahakamani, ameongeza kuwa jambo hilo ameshalipiga
marufuku.
Waziri Silaa amezidi kusema kwa kuwa mahakama inasikiliza kila mtu, hivyo wapo
watu ambao hutumia mwanya huo kuchelewesha haki za wengine au kuwasumbua watu
wengine hasa ambao hawajui sheria au hawana nguvu ya kupambana kimahakama.
Hivyo suala hilo ni misuse of court process.
Amemalizia kwa kusema kuwa Wizara ya Ardhi itamsikiliza mwananchi yeyote na
maadam atakuwa na vielelezo vyote na pale penye haki za watu watazitoa.
Hawa ni viongozi wawili wenye dhamana kubwa ndani ya chama na
serikali. Wanatoa kauli hizi, siyo kwa ajili ya kubeza kazi na wajibu wa
mahakama katika kutenda haki, lakini kimsingi, wanatoa ishara ya kutokuwepo kwa
uwiano mzuri wa haki kuonekana imetendeka.
Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma Hamis anaweza kuwa, huko aliko,
akawa na mawazo tofauti juu ya kauli za viongozi hawa. Lakini kwa manufaa yake
binafsi kama binadamu na kiongozi wa Idara nyeti kabisa ya uhai wa binadamu, ni
vyema tukamweleza kuwa pamoja na lugha ya kistaarabu iliyotumiwa na viongozi
hao, ukweli ulio wazi ni kuwa mahakama zetu zinatenda haki kwa wenye fedha.
Ni ngumu kuthibitisha kauli yangu hii, kwa sababu mimi si
mwanasheria na hukumu hutolewa kwa vifungu vya sheria. Pamoja na kwamba kila
hukumu sisi wengine hutajiwa vifungu hivyo vilivyopelekea hukumu iliyotolewa,
lakini tumeshuhudia mara nyingi, kwenye kesi inayomhusu mlalahoi na mwenye
nazo, matajiri huibuka videdea.
Si mara zote hushinda kwa rushwa. Isipokuwa kwa uwezo wao
kifedha, huweza kuweka mawakili wazuri, wakati mwingine zaidi ya mmoja na hivyo
kupelekea kuwa na nguvu katika mwenendo mzima wa kesi.
Lakini upo ushahidi wa kimazingira kuwa katika migogoro ya
ardhi, watu wenye fedha, huwahonga baadhi ya watumishi wa serikali wasio
waaminifu, ambao hutoa nyaraka za uongo zinazowaongoza kwenye katika mabaraza
ya ardhi na mahakama, ambako huko nako, watumishi wenye tamaa, hushawika kwa
fedha na kukuta shauri ambalo lingeisha siku moja, linachukua miaka mingi na
hukumu kutolewa kwa uonevu.
Tumeshuhudia, jeuri ya wenye fedha, wakivunja nyumba za watu
wakati suala likiwa mahakamani. Hii ni katika kuwavuruga tu na mara nyingi,
jambo hili hulindwa na vyombo vya dola.
Ninao mfano kuthibitisha hili. Familia ya Charles Forodha,
inayoishi katika Mtaa wa Kihonzile, Bunju B jijini Dar es Salaam, wiki
iliyopita ilivunjiwa nyumba yao, wakati shauri linalohusu mgogoro baina yao na
jirani, ambaye anamiliki fedha nyingi, likiwa bado mahakamani.
Mwathirika huyo hakutaarifiwa kimaandishi kama sheria
zinavyotaka juu ya kusudio la kuvunjwa kwa nyumba hiyo na wala hakupewa hata
ruhusa ya kutoa vitu vyake ndani. Matokeo yake vibaka wakagawana vitu vyake,
ikiwa ni pamoja na kuibiwa kiasi cha shilingi milioni nne zilizokuwa ndani.
Dalili kwamba kulikuwa na rushwa katika jambo hilo, wavunjaji
hao walisimamiwa na maofisa wa polisi pamoja na mtendaji wa mtaa, ambao
wanafahamu vyema sheria zinasema nini kwa tukio kama hili.
Ujumbe wa Waziri na Katibu wa Uenezi wa chama, siyo kubeza kazi
za idara hii muhimu kabisa katika uhai wa wananchi, lakini ni kuutaka uongozi
wa Mahakama kuliona tatizo hili kwa ukubwa wake na kulifanyia kazi.
Zile kauli za ‘si uende mahakamani’ ni kama kejeli tu, kwa
sababu katika hali halisi, mtu akiwa hana fedha, hakufai.
Ukishafikishwa mahakamani, ili mtuhumiwa aweze kupata dhamana,
inatakiwa barua kutoka serikali ya mtaa, ambayo hawezi kupewa bila kutoa hela.
Akifika nayo mahakamani, ni lazima pia atoe hela ili aachiwe kwa dhamana, licha
ya kumpeleka mtu wa kumdhamini.
Huu umeshakuwa kama utamaduni. Haki inayopatikana mahakamani ni
pale wanaposhtakiana wakubwa kwa wakubwa, maana hapo sheria zitafuatwa kwa
sababu wote wana uwezo, lakini mnyonge anapohusika, ni uonevu.
Na hii ipo mahakama zote, nchi nzima kwa kesi za aina zote.
Matajiri na wakubwa serikalini huwabambikia kesi watu waliokosana nao,
wanaochukuliana mabwana au mabibi mitaani na kwa nguvu zao, wengi wanafungwa.

Post a Comment