Familia iliyovunjiwa nyumba yamlilia Mtendaji wa Mtaa

 

Rose Forodha, mama ambaye pamoja na familia yake wanaishi nje zaidi ya wiki sasa baada ya nyumba yao kubomolewa kwenye zoezi lililosimamiwa na Ofisa Mtendaji wa Mtaa wa Kihonzile, Bunju B, Bwana Jackson Mwilima.

Na Mwandishi Wetu

FAMILIA ya Charles Forodha, mkazi wa mtaa wa Kihonzile, Bunju B Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, imemlilia Ofisa Mtendaji wa mtaa huo, Jackson Mwilima wakimwita msaliti, kwani licha ya kujua haki yao, aliungana na mtu aliyewavunjia nyumba yao wiki iliyopita.

Akizungumza huku akibubujika machozi nyumbani kwake, mama wa familia hiyo, Rose Forodha, alisema ofisi ya mtaa ilikuwa inafahamu kila kitu kuhusu mgogoro uliokuwepo kati yao na jirani yao, ambaye ni tajiri wa baba wa familia hiyo aitwaye Diana Alex Kajumulo.

“Huyu mama alitupatia hiki kiwanja kama zawadi kwa binti yetu wakati huo akiwa mdogo baada ya mume wangu kuwa amefanya kazi ya kumlindia hili shamba kwa zaidi ya miaka 20, lakini ghafla tukashangaa anaanza kusema sisi ni wavamizi. Majirani wanafahamu kuhusu jambo hili na tulienda serikali ya mtaa tukashinda hili shauri.

“Akaanza chokochoko. Kwanza akajenga ukuta ambao uliziba kabisa madirisha ya nyumba yetu. Tukaenda ofisi ya serikali ya mtaa kulalamika akaamriwa abomoe. Mwenyekiti wa Mtaa na Ofisa Mtendaji walikuwa upande wetu kwa sababu wote wanajua jinsi tulivyokipata kiwanja hiki.

Ukuta uliojengwa na Diana Alex Kajumulo kuziba madirisha ya nyumba ya Bwana Charles Forodha, ambaye baadaye aliivunja nyumba hiyo licha ya kuwa kesi ilikuwa mahakamani zoezi ambalo linadaiwa kusimamiwa na ofisa Mtendaji wa mtaa huo 

“Baadaye sijui nini kilitokea, yule Ofisa Mtendaji akahamishwa. Ndipo akaletwa huyu mtendaji ambaye tangu amekuja, tunaona yupo upande wa huyu mama, wakati hata hajui historia ya jambo hili. Amekataa kushirikiana na Mwenyekiti wa Mtaa anayefahamu kuhusu jambo hili, yeye hata sijui amepewa nini,” analalamika mama huyo ambaye katika zoezi la uvunjaji wa nyumba yake, anadai kupoteza shilingi milioni nne alizokuwa amekusanya kama ‘kijumbe’ kwenye michezo ya kinamama.

Mama huyo anasema kinachowatia mashaka hadi kuamini kuwa kiongozi huyo wa serikali alinunuliwa, ni kitendo chake cha kusimamia ubomoaji bila kujali kwamba familia hiyo haikupewa taarifa kama sheria zinavyotaka na alikataa katakata kuwaruhusu kutoa mali zao wakati zoezi hilo likiendelea.

“Tulimuuliza mbona sisi hatuna taarifa ya kimaandishi, akawa hatusikilizi. Hata tulipoomba tupewe muda kidogo wa kutoa vitu vyetu ndani ya nyumba, alikataa na kuamuru mabaunsa kuendelea kuvunja nyumba yetu huku vitu vyetu vikivunjwa na vingine kuibiwa na vibaka bila msaada wowote,” alisema mama huyo.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa huo wa Kihonzile, Hassan Mnondwa alikiri kutokea kwa tukio hilo na kwamba yeye ni mkazi wa mtaa huo kwa miaka mingi na anafahamu kuhusu familia hiyo kupewa kiwanja hicho miaka ya nyuma. Alisema anatambua pia kuhusu chanzo cha mgogoro huo na ofisi yao inalifahamu vyema jambo hilo.

“Mgogoro huu tunafahamu kuwa ulikuwa mahakamani, juzi nilipigiwa simu na OCD wa Mabwepande akaniambia kama nina taarifa za nyumba ya mkazi wangu kuvunjwa, nikasema sina taarifa. Lakini cha kushangaza akasema ofisi yetu inafahamu na kwa hiyo anatuma askari ili waje kushirikiana na mimi kwenye uvunjaji.

“Nilipomwomba kama kuna nyaraka zozote za uvunjaji huo akasema tayari zilishasainiwa na mahakama tokea mwezi wa kwanza. Mimi nikasema sitashiriki zoezi hilo bila kuona nyaraka hizo. Wakaja ofisini wakanikuta, nikawapa msimamo wangu. Wakampigia Mtendaji ambaye aliwaambia alikuwa njiani, wakamsubiri na alipokuja wakaondoka naye kuja hapa bila mimi kuona hizo nyaraka,” alisema.

Alipoulizwa kama Mtendaji anaweza kufanya jambo bila ya kumshirikisha yeye, alidai jambo hilo linawezekana kwa kuwa kila mmoja ana muhuri wake.

Ojuku Blog ilifanikiwa kumpata Ofisa Mtendaji huyo, Jackson Mwilima kupitia simu yake ya mkononi na alipoulizwa kuhusu suala hilo alikata simu. Lakini alipotumiwa maswali kupitia mtandao wa What’sApp, akiulizwa kuhusu kusimamia zoezi hilo la uvunjaji bila kufuata taratibu ikiwa ni pamoja na tuhuma za kuhongwa na mvunjaji wa nyumba hiyo, alijibu kuwa asingeweza kujibu kwenye simu na badala yake waandishi wamfuate ofisini kwake.

 

 

No comments