Simba inamhitaji zaidi Chama kuliko Cloutus anavyoihitaji

 


Na Ojuku Abraham

Ninawasikia mashabiki wa Simba wanavyosema, kwamba Cloutous Chota Chama amemaliza enzi zake pale Msimbazi kwenye timu yao. Ninawasiki pia hata mashabiki wa watani, nao wakiimba wimbo huo.

Ni kweli kwamba Mwamba wa Lusaka ana zaidi ya misimu mitano sasa akiwa nyota pale klabuni kwao, kiasi kwamba ameshakuwa wa kawaida. Kwa ufanisi wake ndani ya dimba, wengi wanaamini hana jipya analoweza kuwapa tena.

Nimesema ninasikia hata mashabiki wa Yanga nao wanaimba wimbo huu, kwamba Tripple C hana kipya tena pale Msimbazi. Ni wakati wa kuachana naye.

Ninakubaliana na maoni ya watu wote kuhusu Chama. Lakini na mimi nina maoni yangu pia. Tofauti nao, mimi sisukumwi na mihemko wa kishabiki, chuki binafsi, wala masilahi yoyote. Kuna watu wanasukumwa na mihemko. Hawa ni wale mashabiki ambao wanaenda na upepo. Kinachotokea leo uwanjani, ndicho watakachodili nacho.

Kwao, jana haina umuhimu na wala kesho siyo ishu yao. Kuna wale wenye chuki binafsi na Chama. Sina uhakika hili linakujaje, lakini ninavyowajua wabongo, chuki bila sababu ni kawaida. Mtu anaweza kukuchukia kwa sababu tu humuombi. Sisi ni watu wa ajabu sana. Lakini kuna watu wenye masilahi.

Kwa mpira wetu, hawa ndiyo watu wabaya zaidi. Kwa sasa, hawana masilahi na Chama. Wanatamani aondoke, ili wapate nafasi ya kumleta mtu atakayenenepesha akaunti zao.

Chama bado muhimu sana pale katika kikosi cha Simba. Simba hii, wote tunaiona. Misimu miwili hii, ambayo Yanga imekuwa bora, kuna watu wana tafsiri tofauti. Ninaopingana nao ni wale wanaoamini Simba ameshuka kiwango. Ninakubaliana na wale wanaoamini Yanga ameboresha kiwango chake, ila Simba amebakia pale pale.

Katika Simba ambayo kiwango chake kimebaki kilekile, viongozi wamefanya jitihada nyingi za kujaribu kuleta wachezaji wapya ili kuifanya timu iende. Ni kipindi ambacho zimesikika kelele za kwamba Shomari Kapombe, Mohamed Hussein wamechoka, watafutiwe mbadala. From nowhere, mtu anakuambia hawa vijana wamechoka, seriously?

Ok. Turejee kwa Chama. Ninakubali kwamba Chama huyu siyo wa misimu miwili iliyopita, kama mchezaji, kama binadamu, umri unaenda. Kiasili, Chama ni slow. Si mchezaji mwenye kasi akiwa au hana mpira, lakini ni mtu mwenye maono na mpira wake.

Utaratibu wake akiwa na mpira unafichwa na umahiri wake katika kuu-hold na kujua nini cha kufanya akiwa nao. Ndiyo maana utaona katika ligi yetu, mchezaji pinzani anapokuwa na uhakika mpira upo katika miliki ya Chama, haendi ovyo ovyo kwa sababu anajua nini kitatokea akienda vibaya.

Chama akiwa Simba hii ya sasa ana vitu vingi anavyoweza kufanya ambavyo wengi wa nafasi yake hawawezi kufanya. Anatoa assist, anaifungua timu pinzani na kutoa nafasi kwa wenzake, anatengeneza nafasi, anafunga, anaunganisha timu, anapiga mipira iliyokufa kwa ufanisi!

Okay, pale Simba kuna Fabrice Ngoma, Saido Ntibanzoikiza, Kanoute, Muzamir Yasin na sasa Babakar Sarr. Ni kweli kwamba hawa wote ni wachezaji wazuri, lakini to be honest, Chama yupo mbele yao!

Kinachowasumbua Simba ni mayowe kutoka nje ambayo yanadakwa na mashabiki oya oya. Yes, kelele za kwamba Chama hana lolote zinazalishwa na wapinzani wao, ambao kwa miaka mingi, wameumizwa sana na uwezo wa kijana huyu kutoka Zambia.

Kwamba amecheza kwa muda mrefu, hana jipya. Sawa, anaweza kuwa kacheza muda mrefu, lakini je, ni kweli kwamba miaka mitano ya uchezaji kwa kiwango kikubwa inaweza kuwa sababu ya kumuacha? Unamuacha kwa sababu amecheza muda mrefu, au kwa sababu ameshuka kiwango?

Edibily Lunyamila, Mohamed Hussein ‘Chinga’, Athuman Abdalah ‘China’, Zamoyoni Mogella, Kenneth Mkapa, Malota Soma, Shaaban Ramadhan, Charles Boniface Mkwasa, George Masatu, Hussein Marsha, Khalfan Ngassa, Mrisho Ngassa na Juma Kaseja, ni baadhi ya wachezaji wazawa ambao walicheza kwa zaidi ya miaka kumi mfululizo wakiwa katika kiwango cha juu kabisa!

Na hata baada ya kucheza kwa kipindi hicho, bado walibaki kucheza Ligi Kuu kwa miaka mingine kadhaa kwa viwango vya kawaida kabla hawajatundika daruga. Leo hii, unasema Chama aliye na misimu mitano kwamba hana jipya la ku-offer kweli?

Okay, acha tukubaliane kwamba hana jipya kwa sasa. Niambie mchezaji anayekwenda kuchukua nafasi yake, ambaye angalau atakuwa na vitu kwa asilimia 75 tu ya Chama. Simuoni.

Ninajua viongozi wa Simba wanasikiliza mayowe ya mashabiki, kwa sababu ndiyo waajiri wao. Lakini katika mpira, hasa huu wa kibongo, hawa wapiga kelele hawajawahi kuwa na shukurani. Miezi michache nyuma, walikuwa wakilalamika kuwa wamepigwa kwa usajili wa mlinda mlango Ayoub, leo hii wamegeuza maneno.

 

 

No comments