Mbunge Viti Maalum CCM apendekeza picha ya Rais Samia iwekwe kwenye fedha



Mbunge wa viti maalumu (CCM), Ng’wasi Kamani ameihoji Serikali kuwa, haioni haja ya yakuweka kumbukumbu ya kudumu ya Rais Samia Suluhu Hassan kwenye fedha za Tanzania.

Ng’wasi amehoji hayo leo Alhamisi Februari 8, 2024 katika kipindi cha maswali ya papo kwa hapo kwa Waziri wa Mkuu Kassim Majaliwa bungeni.

Mbunge huyo amesema mwaka 2006 Bunge lilipitisha Sheria ya Benki ya Tanzania ambayo chini ya kifungu acha 27 (1b) cha sheria hiyo, inaipa mamlaka benki hiyo kutengeneza (ku-design) fedha kwa kuweka nembo na mambo mbalimbali.

Amesema mwaka 2021 Tanzania imepata Rais wake wa kwanza mwanamke anayefanya kazi nzuri na anatambulika duniani kama Rais madhubuti na wa mfano.

Akijibu swali hilo, Majaliwa amesema awali suala la uwekaji wa picha za viongozi mbalimbali katika fedha ulikuwa ni uamuzi uliofanyika kwa lengo la kukumbuka mchango wa viongozi hao wa Tanzania hasa zinazotumika hivi sasa za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Aman Karume.

“Ni kutambua mchangao wao walioutoa katika Taifa hili, kwa hiyo picha zao zilitumika kama sehemu ya kumbukumbu zao. Na tunazo aina ya fedha za noti na sarafu tunazotumia kuweka alama za wanyama wetu, hii ilikuwa ni kuenzi tunu ya Taifa lakini pia kuboresha hamasa kwenye utalii,”amesema Majaliwa.

Amesema mara nyingi uamuzi wa kuweka picha hufanywa na kiongozi mwenyewe kwa kushirikiana na Benki Kuu (BoT) na kwa sababu mbunge huyo ameleta hoja hiyo na wao wanatambua mchango mkubwa uliotolewa na Rais Samia, wameupokea ushauri huo.

No comments