Serikali kutumia teknolojia ya kisasa kudhibiti wanyama wakali, waharibifu
Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki (Mb) amesema Serikali itahakikisha inaendelea kutumia teknolojia ya kisasa kwa kadri inavyowezekana kudhibiti wanyama wakali na waharibifu hususan tembo ili kupunguza migogoro baina ya binadamu na wanyamapori.
Ameyasema hayo leo Februari 7,2024 katika kikao chake na Wabunge wa Mikoa ya Lindi na Mtwara kilicholenga kusikiliza changamoto wanazokabiliana nazo wananchi katika kuthibiti wanyamapori wakali na waharibifu katika maeneo yao kilichofanyika leo jijini Dodoma.
“Katika kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu hususan tembo tunatumia teknolojia ya Geofencing ambapo tutaweza kupata taarifa endapo tembo amesogea karibu na uzio uliowekwa na hivyo askari wetu watachukua hatua za haraka” Mhe. Kairuki amefafanua.
Pia, Waziri Kairuki amesema Serikali imeanza kutumia teknolojia ya kufukuza tembo kwa kutumia kamera za drones ambapo majaribio ya kwanza yamefanyika katika pori la Akiba la Selous.
Kuhusu uzio wa umeme amesema Serikali inaendelea na majaribio kuona kama njia hiyo inafaa au la ambapo kwa sasa majaribio yamefanyika Pori la Akiba la Grumet.
Credit: Bongo5

Post a Comment