Rais William Ruto wa Kenya na Bola Tinubu wa Nigeria Wakosolewa kwa kusafiri sana
Rais William Ruto wa Kenya na Rais Bola Tinubu wa Nigeria, wanakabiliwa na ukosoaji kwa safari zao za mara kwa mara nje ya nchi.
Wawili hao wamekuwa wakikosolewa kutokana na gharama zinazohusiana na safari nyingi za ndege wakati kuna hali ngumu ya kiuchumi nyumbani.
Gazeti la Kenya, Standard, lilimtaja Ruto kuwa "Rais Anayepaa." Gazeti hilo limeandika "kupenda kwake kusafiri, anaonekana hawezi kuacha fursa yoyote" licha ya mahitaji makubwa ya nyumbani, kama vile kukabiliana na gharama ya juu ya maisha.
Mwezi uliopita, Tinubu alifanya safari nyingine barani Ulaya, kiongozi wa upinzani wa Nigeria Atiku Abubakar alisema kwenye mitandao ya kijamii, Nigeria haihitaji "mkuu wa utalii." Alikosoa ziara ya rais "wakati Nigeria inazama katika bahari ya ukosefu wa usalama."
Ni ukweli kuwa, Marais wanapaswa kuhudhuria mikutano ya wakuu wa nchi na kukuza uhusiano wa kigeni. Ni muhimu sio tu kwa sababu za kidiplomasia, lakini pia za kiuchumi, kwani mikataba yenye faida kubwa ya uwekezaji inaweza kujadiliwa.
Lakini baadhi wameeleza kuwa marehemu Rais wa Tanzania John Magufuli hakuwahi kusafiri nje ya Afrika katika miaka yake sita madarakani.
Safari zao ni muhimu?
Mchambuzi wa sera za kigeni kutoka Kenya, Prof Macharia Munene anakiri baadhi ya safari ni muhimu lakini anasema bila shaka nyingine ni "ufujaji".
"Kuna marais wanaopenda kuwa angani. Baadhi ya safari hizi ni za kibinafsi, sio kwa ajili ya nchi," ameiambia BBC.
Wasemaji wa Ruto na Tinubu wanatetea safari zao kuwa muhimu kusaidia kutatua matatizo ambayo wanadaiwa kupuuza.
Katika muda wa miezi minane tangu kuapishwa kwake, Tinubu amefanya safari 14 - wastani ni safari mbili kwa mwezi - lakini hizo ni kidogo ukilinganisha na Ruto, amefunga safari 50 nje ya nchi tangu awe rais 2022 - wastani wa safari tatu kwa mwezi.
Kwa kulinganisha na mtangulizi wa Ruto, Uhuru Kenyatta, alikuwa na wastani wa safari moja ya nje kwa mwezi katika muongo wake wa uongozi, sawa na rekodi ya rais wa Nigeria, Muhammadu Buhari.
Viongozi wengine wa ulimwengu pia husafiri, lakini Ruto na Tinubu wanakabiliwa na maswali ikiwa kila safari ni muhimu. Ofisi ya rais wa Nigeria imesema safari hizo ni muhimu kwa kuvutia wawekezaji wa kigeni.
"Katika kila safari ya nje, ujumbe wangu kwa wawekezaji na wafanyabiashara ni ule ule. Nigeria iko tayari na iko wazi kwa biashara," Rais Tinubu alisema katika ujumbe wake wa Mwaka Mpya 2024.
Swali sio tu safari hizo kuwa za mara kwa mara, pia kuna swali la gharama.
Tinubu inasemekana alitumia naira bilioni 3.4 (dola za kimarekani milioni 2.2) kwa usafiri wa ndani na nje katika miezi sita ya kwanza ya urais wake - 36% zaidi ya kiasi kilichopangwa kwa 2023, gazeti la Punch la Nigeria liliripoti.
Nchini Kenya, Mdhibiti wa Bajeti, ofisi huru inayosimamia matumizi ya serikali, ilionyesha ongezeko kubwa la matumizi ya ofisi ya usafiri wa rais.
Jumla ya matumizi kwa safari za ndani na nje kwa mwaka 2023 yalikuwa zaidi ya shilingi bilioni 1.3 za Kenya (dola za kimarekani milioni 9.2), ikizidi bajeti ya safari ya mwaka uliopita kwa zaidi ya 30%.
Msemaji wa serikali ya Kenya hakujibu maswali ya BBC kuhusu safari za Ruto, ingawa rais na msemaji huyo mara nyingi wamezihalalisha.
Ruto mwenyewe amesema "hasafiri kama mtalii" na safari hizo ni muhimu ili kupata uwekezaji wa kigeni na kutengeneza ajira kwa Wakenya - hivi karibuni alisema amepata nafasi zaidi ya 300,000 za kazi kupitia mazungumzo.
Baada ya safari ya hivi karibuni nchini Japan, Ruto alisema amepata makubaliano ya zaidi ya dola za kimarekani bilioni 2.3.
Huku marais hao wakitilia mkazo faida za safari hizo, Nigeria na Kenya pia zimechukua hatua za kukabiliana na ukosoaji kwa wafanyakazi wa serikali wanaosafiri nje ya nchi.
Kenya imesema imepunguza bajeti yake ya usafiri kwa utumishi wa umma kwa asilimia 50 kutokana na shutuma za "upotevu" wa pesa katika safari za ndani na nje ya nchi. Lakini hii haionekani kumuathiri rais mwenyewe, ambaye amesema hatakwepa safari maadamu zina manufaa.
Mwezi uliopita, rais wa Nigeria alitangaza kupunguzwa kwa ujumbe rasmi wa safari za rais kwa karibu 60%. Maagizo yaliyotangazwa na msemaji wake Ajuri Ngelale ni pamoja na kupunguza msafara wa rais, lakini hakusema iwapo atapunguza idadi ya safari zake.
Baadhi ya mataifa ambayo pia yamelazimika kushughulikia matumizi ya usafiri ya maafisa wa serikali tangu mwaka jana ni pamoja na Uganda, Gambia, Namibia na Sierra Leone, huku viongozi wa Namibia na Sierra Leone nao wakiitwa "marais wanaopaa."

Post a Comment